KIJANA
aitwaye Priscus Mushi, mkazi wa Mbezi jijini Dar ambaye ni muumini wa
Kanisa la Efatha linaloongozwa na Mchungaji Josephat Mwingira ameanika
masikitiko yake baada ya kutengwa na baadhi ya ndugu kufuatia kuoa
mlemavu wa ngozi ‘albino’ aitwaye Tumaini Murungu.
Akizungumza
katika Ukumbi wa Maji uliopo maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
ambapo sherehe za ndoa zilifanyika, Mushi alisema alipotangaza nia ya
kumuoa Tumaini baadhi ya ndugu zake walimtenga lakini hakukata tamaa
kwani aliendelea na taratibu za ndoa.
“Nilimpenda
sana Tumaini na niliamini ndiye mwanamke wa maisha yangu lakini
nilipowaambia ndugu zangu kuwa nataka kumuoa, baadhi walinitenga kwa
uamuzi wangu huo wa kumuoa Tumaini ambaye ni mlemavu wa ngozi eti
nitakuwa nimeleta balaa nyumbani.
“Nilimuomba Mungu anisaidie na nikaongea na waumini wenzangu ambao walikubali kunifanyia sherehe.
Nawashukuru
sana wakwe zangu ambao walinipokea na kunipa ushirikiano katika
kulitimiza tukio hili. Pia nimshukuru mama yangu kwani uwepo wake
umenipa faraja kubwa,” alisema Mushi.
Wakizungumzia
kitendo cha Mushi kutengwa na baadhi ya ndugu zake, baadhi ya waumini
walilaani wakieleza kuwa, si jambo zuri hata kidogo.
“Inaumiza
sana, unajua binadamu wote ni sawa, kwani msichana albino hastahili
kuolewa? Tuache ubaguzi usiyo na maana ambao unamchukiza hata Mungu.
"Eti
kuoa albino ni mkosi kwenye familia, nani kasema? Imani hizi potofu
zikemewa kwa nguvu zote,” alisema muumini mmoja aliyejitambulisha kwa
jina la Eliza.
GPL