Monday, June 17, 2013

TRA mkoa wa Singida yakusanya Mapato zaidi ya 2bn



Afisa habari wa TRA mkoa wa Singida Bw. Zacharia Gwagilo akitoa mada yake iliyohusu matumizi ya mashine za kodi (EFDs) kwa wafanyabiashara wasiosajiliwa na VAT kwenye semina iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kanisa la katoliki mjini Singida.

Meneja msaidizi wa TRA mkoa wa Singida Bw.Jacob (kulia) na mwenyekiti wa TCCIA mkoa wa Singida, Bw. Francis Mashuda wakifuatilia kwa makini semina ya uhamasishaji wa wafanyabiashara wasiosajiliwa na VAT kujiunga na mfumo wa kutumia mashine za kodi (EFDs).

Baadhi ya wafanyabishara wa manispaa ya Singida ambao hawajasajiliwa na VAT,wakifuatilia mada zilizokuwa zinatolewa na afisa habari wa TRA mkoa wa Singida Bw. Zacharia Gwagilo (hayupo kwenye picha).Mada hizo zilihusu matumizi ya mashine za kodi (EFDs).(Picha kwa hisani ya Mo blog).


Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Singida, imekusanya mapato mbalimbali ya zaidi ya shilingi 2.7 bilioni kati ya mwezi Julai mwaka jana na Mei mwaka huu.

Akizungumza kwenye semina ya siku moja iliyohudhuriwa na wafanyabiashara wasiosajiliwa na VAT, iliyohusu matumizi ya mfumo wa mashine za kodi (EFDs), Afisa habari wa TRA mkoa wa Singida Zacharia Gwagilo, amesema makusanyo hayo ya kujivunia ni sawa na asilimia 86.21 ya lengo la kukusanya shilingi 3,147,100,000.

Zacharia alisema kuwa juhudi zaidi zinaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha wanakusanya mapato zaidi ya lengo walilojiwekea.

Katika hatua nyingine, Afisa huyo amesema awamu ya pili ya matumizi ya mashine za kodi (EFDs), inaanza mwaka huu na itahusu wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa na VAT.

Amesema lengo ni kuleta uwiano katika ulipaji wa kodi mbalimbali.

Zacharia ametaja baadhi ya faida zitokanazo na matumizi ya mashine hizo kuwa ni kutoa uhakika na usalama wa taarifa, na taarifa hutunzwa katika kifaa maalum (fiscal memory).

Wakati huo huo, Zacharia ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wafanyabiashara kukakikisha wanatoa risiti kwa bidhaa wanazouza na mnunuzi pia ahakikishe anadai risiti pindi anaponunua bidhaa kama sheria inavyodai.