Wednesday, December 5, 2012
Shilingi ya Tanzania ndio chanzo cha kupanda bei ya mafuta..!!!
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya za jumla na rejareja kwa mafuta aina zote. Bei ya petroli, dizeli na ya taa zimeongezeka kwa mwezi huu
Ewura amesema kuwa mabadiliko hayo ya bei yametokana na ongezeko la bei ya mafuta katika soko la dunia na kushuka kidogo kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani.
Katika taarifa ya Ewura jana kwa umma, bei ya petroli na dizeli zimeongezeka kwa viwango tofauti huku petroli imepanda kwa Sh 70 kwa lita sawa na asilimia 3.4 wakati dizeli imepanda kwa Sh 10 kwa lita sawa na asilimia 0.53 na mafuta ya taa bei imepungua kwa Sh 3 kwa lita sawa na asilimia 0.1.
Katika Mkoa wa Dar es Salaam, petroli itauzwa kwa Sh 2,119 kutoka Sh 2,049, dizeli Sh 1,999 kutoka Sh 1,989 za Novemba na mafuta ya taa yatauzwa kwa Sh 2,023 kutoka Sh 2,020. Mkoani Kigoma, petroli itakuwa Sh 2,350, dizeli Sh 2,230 na mafuta ya taa Sh 2,254 wakati Tunduru petroli itauzwa Sh 2,301, dizeli Sh 2,181 na mafuta ya taa Sh 2,105.
Wilayani Nyasa katika Mkoa wa Ruvuma, petroli itauzwa kwa Sh 2,278, dizeli Sh 2,181 na mafuta ya taa ni Sh 2,182. Mpanda petroli itauzwa kwa Sh 2, 326, dizeli Sh 2,207 na mafuta ya taa yatakuwa ni Sh 2,231.
Mkoani Kagera katika Mji wa Bukoba petroli itauzwa Sh 2,334, dizeli Sh 2,214 na mafuta ya taa yatakuwa Sh 2,238, katika Wilaya ya Karagwe petroli itauzwa Sh 2,350, dizeli Sh 2,231 na mafuta ya taa Sh 2,253; wakati Kyerwa, petroli itauzwa kwa Sh 2,356, mafuta ya taa Sh 2,236 na dizeli itauzwa Sh 2,260.
Kuhusu bei za jumla, petroli imeongezeka kwa Sh 69.56 kwa lita sawa na asilimia 3.52; dizeli bei imeongezeka kwa Sh 10.04 kwa lita sawa na asilimia 0.52. Bei ya mafuta ya taa imepungua kwa Sh 3 kwa lita sawa na asilimia 0.15.