Simba wamng'ang'ania Yondani |
|
|
Clara Alphonce KLABU ya Simba imeendelea kumng'ang'ania beki wake, Kelvin Yondani licha ya kuachana na timu hiyo na kwenda kujiunga na Yanga.
Hatua
ya Simba kumng'ang'ania mchezaji huyo ni baada ya kutangaza wachezaji
iliyowaacha akiwemo kipa wa akiba. Ally Mustapha 'Barthez', beki raia wa
Uganda, Derick Walulya, mashambuliaji raia wa Ivory Coast, Gervais Kago
na Juma Jabu.
Beki mwingine ambaye ametangazwa kuachwa ni Salum Kanoni ambaye hata hivyo, mkataba wake umebakisha siku mbili kumalizika.
Wachezaji
ambao klabu hiyo inakusudia kuwatoa kwa mkopo ni Rajab Isihaka, Salum
Machaku, Haruna Shamte na Shija Mkina. Mkina bado anacheza kwa mkopo
Kagera Sugar.
Mwishoni mwa wiki, baadhi ya wadau wa Simba
walikuwa wakihaha kutaka kumrejesha mchezaji huyo kundini baada ya
kuanza mazoezi Yanga Ijumaa iliyopita lakini mwanzoni mwa wiki hii,
Mwananchi ilitonywa na chanzo cha habari kikisema kuwa baadhi ya watu
wanaohusika na usajili wameamua kuachana na mchezaji huyo.
Chanzo
kimoja ndani ya klabu ya Simba, kilipasha kuwa uamuzi wa Yondani kwenda
Yanga ni sahihi kwani uzembe wa viongozi ndiyo uliosababisha yote hayo
kutokea.
"Mchezaji alikuwa akiwaambia juu ya mkataba wake,
viongozi wako kimya, akisafiri na timu ya Taifa akirudi anawakumbusha
lakini kimya, tumerudi na Simba kutoka Setif, Algeria akawakumbusha,
tumetoka Al Shandy kote kimya, sasa uamuzi wake ni sahihi," kilisema
chanzo hicho.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage
alikaririwa akisema kuwa Simba haitamwacha mchezaji huyo kwa kuwa ni
mchezaji wake halali na itamtangaza katika orodha yake ya mwisho Juni
30.
Alisema: "Yondani ni mchezaji halali wa Simba aliye na
mkataba hadi Mei 31, 2014 mkataba ulioongezwa Desemba 23, 2011 ikiwa ni
sehemu ya kuundeleza mkataba wa awali uliokuwa unaisha Mei 31, 2012."
Yondani
ambaye tayari amevuta 'fungu' kutoka kwa Yanga, alisema juzi kuwa
hawezi kurudi nyuma na uamuzi wake ni sahihi kwenda klabu hiyo ya
Jangwani.
"Mimi nimesajili Yanga na nimeshachukua changu...mpira
ni maisha yangu na isitoshe haya ni maisha na siwezi kuchezea bahati
yangu. Mimi nimeshaamua kuchezea Yanga na nataka Simba wajue hivyo,"
alisema Yondani akizungumza na kipindi cha Sports Extra cha Clouds TV
katikati ya wiki hii.
Akizungumza jana, Ofisa Habari wa
Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Boniface Wambura alikiri kupokea
majina ya wachezaji walioachwa na Simba huku likikosekana jina la
Yondani.
Mbali na Simba, wageni wa Ligi Kuu, Polisi Morogoro
imeacha wachezaji 17 wakati Tanzania Prisons ambayo nayo imepanda Ligi
Kuu imeacha wachezaji 11.
Walioachwa na Tanzania Prisons ni Adam
Mtumwa, Dickson Oswald, Exavery Mapunda, Ismail Selemani, Lwitiko
Joseph, Mbega Daffa, Mwamba Mkumbwa, Mussa Kidodo, Rajab Ally, Richard
Mwakalinga na Sweetbert Ajiro.
Polisi Morogoro imewaacha Abdul
Ibadi, Ally Moshi, Benedict Kitangita, Hassan Kodo, Hussein Lutaweangu,
Hussein Sheikh, Juma Maboga, Mafwimbo Lutty na Makungu Slim.
Pia
wamo Mbaraka Masenga, Method Andrew, Moses Mtitu, Ramadhan Kilumbanga,
Ramadhan Toyoyo, Said Kawambwa, Salum Juma na Thobias John.
Kwa
upande wa Azam FC, imewasilisha majina ya wachezaji watatu iliyoamua
kukatisha mkataba wao ambao ni Tumba Swedi, Mau Bofu na Sino Augustino.
Kagera
Sugar imewaacha Cassian Ponera, Hamis Msafiri, Hussein Swedi, Ibrahim
Mamba, Martin Muganyizi, Mike Katende, Moses Musome, Msafiri Davo, Said
Ahmed, Said Dilunga, Steven Mazanda na Yona Ndabila.
Alisema
uhamisho wa wachezaji kwa msimu huu ulianza Juni 15 mwaka huu na
utamalizika Julai 30 mwaka huu wakati kipindi cha kuanza wachezaji (kwa
wasio wa Ligi Kuu) ni kati ya Juni 15 na 30 mwaka huu.
Wambura
alisema kuwa klabu za Ligi Kuu kutangaza wachezaji watakaositishiwa
mikataba yao ni kuanzia Juni 15-30 mwaka huu na usajili wa wachezaji
unafanyika kuanzia Juni 15 hadi Agosti 10 mwaka huu. |
Kikosi cha timu ya Taifa Hispania bajeti ya Wizara Michezo miaka 31 |
|