Thursday, August 29, 2013

MCH. MOSES KULOLA AFARIKI.


Nimesoma kwa masikitiko ktk chanzo kimoja cha habari kuwa mtumishi halisi wa Mungu baba Moses Kulola amefariki dunia kwa ugonjwa wam mapafu (mwenye taarifa zaidi atujuze). Mtumishi huyu wa ukweli (ukifananisha na hawa wanaoota ka uyoga siku hizi) alizaliwa 1928, aliilinda imani kwa uthabiti na ni mchango mkubwa sana kwa wokovu wa wengi Tanzania na nje ya mipaka.
Hakika mwendo ameumaliza, imani ameilinda na amevipiga vita vilivyo vizuri. Hakika mbingu imempokea shujaa huyu! Amina.

Majambazi yavamia bank jijini dar, wamevaa sare za polisi

 
 Majambazi baadhi yao wakiwa wamevalia sare za jeshi la polisi, wamevamia Benki ya Habib African iliyopo Mtaa wa Livingstone Kariakoo, Jijini Dar es Salaam na kupora kiasi kikubwa cha fedha.

Source: EATV

Funny photo effects

Funny photo effects

Waliopitisha ‘unga’ watimuliwa

MWAKTEMBE 
Dkt. Harrison Mwakyembe- Waziri wa Uchukuzi
 
Wapigwa marufuku kukanyaga uwanja wa ndege

HATIMAYE maofisa usalama wanne katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wamepewa barua zao za kuachishwa kazi.
Hatua hiyo imekuja baada ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyemba kuagiza waachishwe kazi mara moja kutokana na kutuhumiwa kuhusika kwao katika kusaidia watu kusafirisha dawa za kulevya kilo 180.
Maofisa hao kwa mujibu wa Dk. Mwakyembe ni Yusufu Issa, Jackson Manyonyi, Juliana Thadei na Mohamed Kalungwana. Baada ya kukabidhiwa barua zao wamepigwa marufuku wasionekane katika uwanja huo.
Hata hivyo, maofisa hao wataendelea kupata mishahara yao kama kawaida hadi kesi yao ambayo inayoshughulikiwa na Jeshi la Polisi itakapofikishwa mahakamani na kutolewa hukumu.
Kauli ya maofisa hao kukabidhiwa barua zao ilitolewa Dar es Salaam jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Ramadhan Maleta.   “Sisi upande wetu tumewaambia waandike charge sheet mambo mengine tumewachia polisi wenyewe,” alisema Maleta.
Katika hatua nyingine, mmoja wa walinzi katika uwanja huo alidokeza gazeti hili kuwa mashine mpya zimefungwa kwa ajili ya kuongeza ulinzi eneo hilo.
Pia alisema mbwa wa ukaguzi wataendelea kuwepo uwanjani hapo kama kawaida ili kudhibiti wanaoingiza au kusafirisha dawa hizo. Alisema mbwa hao hawajaondolewa kama inavyovumishwa mitaani.
Ulinzi umeimarishwa katika uwanja huo ambapo kuna sehemu ambazo watu wanalazimika kuvua viatu na kupitishwa katika mashine maalumu za kukaguliwa ili kuhakikisha hakuna anayepita eneo hilo na kitu kisichotakiwa.
Pia kitengo cha kusindikiza au kupokea watu mashuhuri katika uwanja huo pamefungwa mashine maalumu.
Pamoja na mambo mengine, Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) lina mpango wa kuingia ubia na Kampuni ya Alhayat Investment and Development L.L.C The Sultanate of Oman ili kuleta ndege nane kwa safari za ndani na nje.
Katika suala hilo, Maleta alisema mipango hiyo ipo mbioni na wahusika wakuu wa jambo hilo ni Wizara ya Uchukuzi.
Maleta alikuwa na wageni wa kampuni hiyo kutoka Oman ambao walikuja nchini kwa ajili ya kukagua viwanja vya ndege kabla hawajasaini mkataba rasmi wa kujikita katika sekta hiyo.   “Kwa kuanzia kampuni hiyo ina mpango wa kuleta ndege nane kubwa zitakazorushwa kwa nembo ya Air Tanzania,” alisema Maleta.
Alisita kutaja aina ya ndege pamoja na gharama zake kutokana na suala hilo kushughulikiwa zaidi na wizara husika.

Source: Jambo Leo

Vigogo madawa ya kulevya mali zao zakamatwa


VIGOGO 111 wanaosadikiwa kujihusisha na biashara yharamu ya madawa ya kulevya nchini wameanza kuonja 'joto ya jiwe' kufuatia Jeshi la Polisi Tanzania Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola kukamata mali zao, Uwazi lina mpango mzima.
Kamanda Nzowa.
Kwa mujibu wa vyanzo makini ndani ya jeshi hilo, pia vigogo wengi wanaojihusisha na biashara hiyo  walikamatwa na kiasi kikubwa cha ‘unga’ ndani ya kipindi cha miaka minne iliyopita.
Kuhusu mali ambazo ni magari, ilidaiwa kuwa kufuatia taarifa zilizowataja wauza unga, jeshi la polisi liliamua kushikilia magari hayo na kufanya uchunguzi wa uhalali wake.
“Kuna watu walitajwa majina, wakafuatiliwa, magari yao yakakamatwa na kufanyiwa uchunguzi, lakini cha kushangaza baadhi yao  wameingia mitini na kutelekeza magari yao,” kilisema chanzo.
Chanzo kilisema baadhi ya magari hayo ni Mercedes Benz, Jeep, Toyota Spacio, Toyota Galsira, Toyota Mark II, Nissan Patrol 4x4 GL, Toyota Land Cruiser na Toyota Prado. 
Uwazi lilifanikiwa kunasa majina ya vigogo waliokamatwa wakiwa na unga  na kiasi walichokamatwa nacho.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika mahakama mbalimbali nchini na ndani ya jeshi la polisi umebaini kuwa, kesi za watuhumiwa hao zinaendelea kuunguruma kortini  japokuwa kasi yake si ya kuridhisha.
Madawa ya kulevya.
POLISI WABUNI MBINU MPYA
Vyanzo hivyo viliendelea kudai kwamba polisi wamebuni mbinu mpya ya kuwakamata vigogo wa madawa ya kulevya wakiamini itawapa mafanikio zaidi.
“Siku hizi si kama zamani, jeshi la polisi tumebuni mbinu mpya ya kuwakamata hawa jamaa (vigogo). Mbinu hii italeta mafanikio makubwa zaidi,” alisema mtoa habari wetu.
WAPAMBANAJI WA UNGA HATARINI
Taarifa zaidi zinadai kwamba usalama wa viongozi wanaopambana na wahusika wa unga nchini upo shakani kutokana na vitisho vinavyotolewa na mtandao huo duniani kote.
Inaaminika kuwa wengi wanaopambana au kupiga vita madawa ya kulevya, hususan viongozi na waandishi wa habari, hutendwa vibaya wakati mwingine kuuawa kabisa.
UWAZI LAMSAKA KAMANDA NZOWA
Kufuatia taarifa hizo za kiuchunguzi, katikati ya wiki iliyopita, mapaparazi wetu walimtafuta Kamanda wa Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa na kumuuliza kuhusu zoezi zima la kamatakamata ya wanamtandao hao.
Kamanda Nzowa alisema zoezi la kuwakamata wanaojihusisha na biashara hiyo linaendelea vizuri.

Alisema mpaka Mei, mwaka huu kikosi chake kimeshakamata kiasi kikubwa cha unga na kuongeza kuwa anaamini kasi ya biashara hiyo nchini imepungua sana.
Aliongeza kuwa askari wake wamejipanga vizuri na wana mafunzo maalum ya kuwatambua watu hao hatari.
Baadhi ya magari ya watuhumiwa wa madawa ya kulevya yakiwa kituoni.
VIGOGO HUWALISHA KIAPO KIBAYA  WANAOWABEBESHA
“Tumewakamata ‘mapapa’ (wauza unga wadogo) wengi sana na tunahakikisha kwamba ‘nyangumi’ (wauza unga vigogo)  nao hawachomoki.
“Mara nyingi vigogo wamekuwa wakiwalisha kiapo kibaya vijana wanaowabebesha unga kwamba  ikitokea wakakamatwa wasiwataje lakini nao tunawabana kitaalam mpaka wanawataja, kwa sasa bado tunaendelea kuwadaka,” alisema Kamanda Nzowa.
Kamanda huyo aliwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi lake dhidi ya wauza madawa ili kutokomeza kabisa biashara hiyo.

ULINZI VIWANJA VYA NDEGE NCHINI SASA NI MOTO
Katika maongezi yake, Afande Nzowa alisema ulinzi umeimarishwa katika viwanja vya ndege, bandarini, mipaka ya nchi na sehemu zote zinazohisiwa kuweza kupitishwa madawa hayo.

AANIKA MAJINA 111
Kamanda Nzowa alikwenda mbele zaidi kwa kuweka wazi takwimu ya ukamataji wa watuhumiwa hao kutoka mwaka 2009 hadi Mei, 2013.

Agness Gerald ‘Masogange’.
Orodha chini inabainisha kiasi na aina ya madawa waliyokamatwa nayo katika mabano.
Steven  Gwaza, (heroin gramu 825.7), Rebecca Wairimu Mwangi (heroin gram 1,800), Khatibu Bakari Khatibu, Khalid Salim Maunga, (cocaine gramu 1,007.4), Dhoulkefly  Awadh, (cocaine gramu 893.58), Abdallah Pashua Kipevu (heroin gramu 31,000), Diaka Brama Kaba (heroin gramu 31,000), huyu alikamatwa akiwa na Ndjane Abubakar, Sylivia Kaaya Namirembe, Farid Kisuule, Robinson Dumba Teise na Ismail Mugabi.

Melisa Edward.
Wengine ni Rashid Salim Mohamed, (cocaine gramu 1,374.32), Mini Thabo Hamza (cocaine gramu 1,595.74), Hamis Mohamed Mtou (cocaine gramu 850), Kwako Sarfo, Mnigeria (cocaine gramu 1,1951.80), Mustapha Musa (cocaine gramu 286), alikuwa na Aman Saidfadhil Daruweshi na Afshin  Jalal.
Kamanda Nzowa akaendelea kuwaanika, Jack Vuyo, (heroin gramu 42,000) huyu alikuwa na Anastazia Elizabeth Cloete. Simon Eugenio Fadu    (cocaine gramu 8,000), Assad  Aziz, (heroin gramu 50,000), alikuwa na Isamil Shebe Ismail, Rashid Salim na Majed Gholamghader.


Joseph Chukwumeka Nwabunwane.
Wengine kwenye orodha hiyo ni, Anna  Jamaniste Mboya, (cocaine gramu 1,140), Fredy William Chonde (heroin gramu 175,000),  Kambi Zuber, Abdul Ghan na Shahbaz Malik, Livinus Malik (Wapakistani) (cocaine gramu 804.7), Chukwudu  Denis Okechukwu, Paulo Ekechukwu na Hycenth Stan (Wanigeria) (cocaine gramu 81,000).
Aidha wapo, Shoaib S.O. Mohammed, Fedro Alfredo Chongo, (cocaine gramu 1,530), Kadiria  Said Kimaro (heroin gramu 1,365.91),  Abdallah Rajab Mwalimu (cocaine gramu 716.5), Mwiteka Godfrey Mwandemele (cocaine gramu 1,112),  Abbas Kondo Gede (cocaine gramu 1,112), Mwanaidi  Ramadhan Mfundo (cocaiane gramu 5,000), alikuwa na Sarah David Munuo,  Antony  Karanja, Benny Ngare,  Almasi Hamis Said, Yahya Haroun Ibrahim, Aisha Said Kungwi, Rajab Juma Mzome na John  William Mwakalasya.

Kwaku Safo.
Wengine ni Ally Mirzai Pirbakhshi (cocaine gramu 97,000) alikuwa na Aziz Juma Kizingiti, Said Mashaka Mrisho, Abdulahman  Mtumwa na Hamidu Kitwana Karimu.
Ramadhan Athuman (heroin gramu 3,000) alikuwa na Rashid Mohammed, Ally Mohammed Kichaa na Issa Abdulahman. Rashid  Ally Mtopea (heroin gramu 12,000) alikuwa na Idd Adam Mwaduga, Nurdin Adam. Maurine Amatus Lyumba, John  Adams Igwenma  wa (Mnaijeria) ( cocaine gramu 830.19).
Upendo Mohammed Cheusi, Abdallah Omar Salum (cannabis sativa gramu 1,000) alikuwa na Cosmos Chukwumezie, Ifeanyi  Malven Kalu Oko (Wanaijeria)  (heroin gramu 3,185.38), Allan Duller (cocaine gramu 3,882.92), Alberto Mendes kutoka Ghana, (gramu 1,277.10 za heroin)
Wengine ni Joseph Chukwumeka Nwabunwanne Minigeria, (gramu 1,245.96 za heroin) Kwaku Safo Brobbey Mghana (gramu 13,781.78 za heroin), Princewill Ejike Mnigeria (gramu 981.12 za heroin),Mary  Mvula Mzambia (gramu 391.51 za cocaine), Waziri Shaban Mizongi, (gramu 2,013 za heroin) akiwa na Santos Joseph Mpondela, Kelvin Kelven Mwazeni.
Wengine ni Emmanuela Adom, Mghana (gramu 9,838.1 za cocaine), Asha Omary Ramadhan, (gramu 1.56), Mariam Mohammed Said, (gramu 9,857.54 za bangi) akiwa na Abdullatif A. Fundikira
Aliendelea kuwataja Marceline Koivogui, Mghana (gramu 1,073.82 za heroin),  Edwin Cheleh Swen Mliberia (gramu 1,509.35 za heroin),  akiwa na Benjamin Obioma Onuorah  wa Nigeria, Sofia Seif Kingazi, (gramu 3,379.54 za cocaine), Josephine Mumbi Waithera Mkenya (gramu 3,249.82 za cocaine), Iddi Juma Mfaume,( gramu 563.25 za heroine), Amina Kassim Ramadhani,( gramu 1,980.11 za heroine) na Vivian Edigin Mnigeria ( gramu 797.56 za cocaine), Hadija Tambwe,( gramu 33,507.04 Za cannabis),  Sasha Farhan  na Mnyeke Sativa, na Mychel Andriand Takahindangeng Muindonesia,( gramu 3,932.44 za cocaine).
Wengine ni Kristina Biskavevskaja Mluthenia (gramu 4,000 za cocaine), Stephen Basil Ojiofor Mnigeri (gramu 1,173 za cocaine), Judith Marko Kusekwa, ( gramu 1,793 za heroin), Khamis Said Bakari,( gramu 1,793 za heroin).
Kundi la mwisho ni Tabia Omary au Neema Omary (gramu 994.97 za  heroin), Masesa au Habiba Andrew Joseph, ( gramu 1,037.9 za heroin).
Hivi karibuni Agness Gerald ‘Masogange’ na mwenzake walikamatwa Afrika Kusini wakiwa na kilo 150 za dawa za kulevya.



SOURCE: UWAZI-GPL

Wednesday, August 28, 2013

Atengwa kwa kumuoa mlemavu wa ngozi(Albino)

KIJANA aitwaye Priscus Mushi, mkazi wa Mbezi jijini Dar ambaye ni muumini wa Kanisa la Efatha linaloongozwa na Mchungaji Josephat Mwingira ameanika masikitiko yake baada ya kutengwa na baadhi ya ndugu kufuatia kuoa mlemavu wa ngozi ‘albino’ aitwaye Tumaini Murungu.

Akizungumza katika Ukumbi wa Maji uliopo maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo sherehe za ndoa zilifanyika, Mushi alisema alipotangaza nia ya kumuoa Tumaini baadhi ya ndugu zake walimtenga lakini hakukata tamaa kwani aliendelea na taratibu za ndoa.

“Nilimpenda sana Tumaini na niliamini ndiye mwanamke wa maisha yangu lakini nilipowaambia ndugu zangu kuwa nataka kumuoa, baadhi walinitenga kwa uamuzi wangu huo wa kumuoa Tumaini ambaye ni mlemavu wa ngozi eti nitakuwa nimeleta balaa nyumbani.

“Nilimuomba Mungu anisaidie na nikaongea na waumini wenzangu ambao walikubali kunifanyia sherehe. 

Nawashukuru sana wakwe zangu ambao walinipokea na kunipa ushirikiano katika kulitimiza tukio hili. Pia nimshukuru mama yangu kwani uwepo wake umenipa faraja kubwa,” alisema Mushi.

Wakizungumzia kitendo cha Mushi kutengwa na baadhi ya ndugu zake, baadhi ya waumini walilaani wakieleza kuwa, si jambo zuri hata kidogo.

“Inaumiza sana, unajua binadamu wote ni sawa, kwani msichana albino hastahili kuolewa? Tuache ubaguzi usiyo na maana ambao unamchukiza hata Mungu. 


"Eti kuoa albino ni mkosi kwenye familia, nani kasema? Imani hizi potofu zikemewa kwa nguvu zote,” alisema muumini mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Eliza.


GPL

Mama ajifungua watoto wawili walioungana Dar, mmoja hana kichwa


Mkazi wa Zanzibar, Pili Hija akiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam jana na watoto wake walioungana.

Kwa ufupi
  • “Kuna pacha ambao wanakuwa kwenye mifuko tofauti na wengine wanakuwa kwenye mfuko mmoja, hawa wanaokuwa kwenye mfuko mmoja ndio mara nyingi wanashindwa kuachiana na hivyo wanazaliwa  wakiwa wameungana.”Dk Edna Majaliwa, Msimamizi Wodi ya Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili

Mtoto huyo ambaye hana kichwa anapumua pia akiguswa anapata hisia na kutingisha mguu mmoja.
Mkazi wa Jang’ombe Visiwani Zanzibar, Pili Hija (24), amejifungua watoto walioungana huku mmoja akiwa hana kichwa.
Watoto hao ambao wapo Wodi namba 36 katika Jengo la Wazazi la Hospitali ya Taifa Muhimbili mbali na kuzaliwa mmoja akiwa hana kichwa, wameungana sehemu ya uti wa mgongo, mkono mmoja na wanatumia njia moja ya haja kubwa.
Akizungumza  jana, mama wa watoto hao, alisema: “Nilijifungulia nyumbani, nilisikia uchungu mara moja na hapo hapo nikajifungua kwa njia ya kawaida na jirani yangu ndiye aliyenisaidia,”alisema na kuongeza:
“Nilijifungua saa moja  asubuhi, nilijua nitazaa pacha kwa kuwa nilishafanya kipimo katika Hospitali ya Makunduchi, wakaniambia nitajifungua pacha lakini mmoja si binadamu ni kiwiliwili.
“Nimeolewa, mume wangu ni mwanajeshi, nina watoto wengine wawili mmoja wa kike na mwingine wa kiume, mume wangu hajui tukio hili kwani yupo kambini Zanzibar na hatuna mawasiliano yoyote kwa sasa,” alisema.
Daktari wa Upasuaji wa Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Zaituni Bokhary alisema; “Hii ni mara ya kwanza kwa jambo hili kutokea katika miaka ya hivi karibuni. Mara ya mwisho lilitokea mwaka 1984.
“Tulikuwa tufanye upasuaji leo lakini tumeahirisha na utafanyika Alhamisi (kesho) asubuhi katika Kitengo cha Mifupa cha Muhimbili (Moi).”
Msimamizi wa Wodi ya Watoto walikolazwa, Dk Edna Majaliwa  alisema: “Hakuna sababu maalumu kitaalamu  inayosababisha watoto kuungana, mara nyingi zinapokutana mbegu za X na Y na kutengeneza mimba kunakuwa na hatua za ukuaji wiki nne, wiki nane, wiki 12, 16 na kuendelea.

Lukuvi: Wabunge wengi wamo orodha ya dawa za kulevya



Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi  

Lakini asema Serikali haiwezi kukurupuka kuwataja kwa kuwa haina ushahidi wa kutosha
 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi amesema baadhi ya majina ya wabunge yametajwa miongoni mwa watu wanaoshukiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya lakini Serikali haiwezi kuwataja hadharani kwa haraka.

Majibu hayo ya Waziri Lukuvi yamekuja baada ya wabunge kumbana na wengine wakizomea baada ya kueleza ugumu wa kutaja majina ya washukiwa pasi na ushahidi wa kutosha.

“Serikali haiwezi kutaja majina haraka kiasi hicho kwani inaogopa kukurupuka na kushindwa mahakamani, hivyo lazima tuwe makini sana na jambo hilo. Hatuwezi kukurupuka tu eti ni fulani wakati hatuna vithibitisho.

“Kumbukeni wengine mpo humu ndani ya Bunge na tukianza wengi mtakwisha maana katika orodha hiyo kubwa na ninyi mmo na orodha ni kubwa kweli ambayo wakati mwingine inatakiwa umakini wa hali ya juu,” alisema Lukuvi alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Karatu (Chadema), Mchungaji Israel Natse.

Katika swali lake ambalo lilisababisha kelele za kuzomea, Natse alitaka majina hayo yatajwe hadharani. Hata hivyo, hali ilitulia baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuingilia kati na kusema: “Hii tabia ya zomeazomea siitaki humu ndani, acheni tabia hiyo lazima mumsikilize mtu kwa kile anachokisema kwanza lakini mtindo huu si mzuri...”

Patashika hiyo ilitokana na swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Catherine Magige aliyetaka kujua iwapo Serikali inaweza kuwaambia Watanzania ukubwa wa biashara hiyo nchini na kama haioni kama kuna tatizo katika ukaguzi wa abiria na mizigo katika viwanja vya ndege na juhudi za Serikali kumaliza tatizo hilo.

Akijibu swali hilo, Lukuvi alisema ukubwa wa biashara hiyo hapa nchini unadhihirishwa na idadi ya Watanzania 274 waliokamatwa kati ya mwaka 2008 hadi Julai mwaka huu kwa kosa la kujihusisha na dawa za kulevya katika nchi mbalimbali za nje.

Alisema Serikali inafahamu ukubwa wa tatizo la matumizi ya biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya nchini na alitaja takwimu za ukamataji wa dawa hizo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000 hadi Machi, 2012.

Alisema pamoja na kukamatwa kwa Watanzania hao nje ya nchi, wageni 31 wanashikiliwa mahabusu katika Magereza ya Keko na Ukonga, Dar es Salaam ambao ni raia wa Iran, Pakistan, Senegal na Afrika Kusini.

Hata hivyo, katika swali lake la nyongeza, Magige alisema uteketezaji wa dawa zinazotajwa kukamatwa umekuwa wa siri kiasi cha kutiliwa shaka kuwa huenda zinachukuliwa na maofisa waliozikamata ndiyo maana hakuna uwazi.

Kuhusu hilo, Waziri Lukuvi alisema suala la uteketezaji wa dawa hizo hauko wazi kutokana na sheria zilizopo kutotoa nafasi ya kuteketezwa mapema kwa kuwa zinatumika kwa ajili ya ushahidi akisema wakati mwingine hukaa zaidi ya miaka 10.

Tuesday, August 27, 2013

Mwanamke wa kitanzania akamatwa na madawa ya kulevya Dubai

Mwanamke wa kitanzania amekamatwa na madawa ya kulevya Uarabuni akitokea huko Brazil, amedai kuwa mume wake ndio amemponza kwa kumfanya punda (mbebaji) bila ya ridhaa yake, madawa hayo yalikamatwa kwenye begi lake uwanja wa ndege wa Dubai huko uarabuni
kwa maelezo zaidi soma hii habari hapa chini, inayopatikana katika mtandao wa Yahoo.com


Photo of a woman caught with Dhs3 million of drugs.Photo: Yahoo! News
--
A cross-post from Yahoo! News — A woman caught with Dhs3 million of drugs in her suitcase claims she was unwittingly being used as a mule by her husband, Dubai Police said.

The Tanzanian woman was arrested at Dubai International Airport in transit to her home country from Brzail. She claims her husband arranged for her to go on a three-month trip to Brazil so that she could unwind.

However, she told officers that while on holiday, a friend of her husband asked her to take some bags back to Tanzania. She was arrested in Dubai after officers at the airport became suspicious of her behavior. They found 3kg of cocaine in her luggage, worth Dhs3 million.

“She claimed that her husband got her in trouble as he offered her a relaxing trip to Brazil and she went for three months. Her husband’s friend asked her to deliver the bags to her husband in Tanzania,”an official in anti-narcotics said. The suspect has been referred to public prosecution.

Majaji wanaolinda wauza madawa ya kulevya yatajwa!

Majina ya Majaji wanaolinda wauza madawa ya kulevya yatajwa! Wamo Pendo Msuya na Dr Fauz Twalib

Vita dhidi madawa ya kulevya inayoangamiza mamilioni ya watanzania inaendelea.
Gazeti la Jamhuri leo limekuja na story ndefu ya kesi na majina ya majaji wanaolinda wauza unga hao mahakamani. Majaji Pendo Msuya na Dr Fauz Twalib wametajwa na mifano ya kesi waliyochakachua ambayo huhitaji kuwa mwanasheria kujua kuwa kesi hii imechakachuliwa.

Aidha mahakimu wa mahakama ya Temeke, Kisutu bila kuacha nyuma ofisi ya DPP ni miongoni mwa wahusika wa kulinda mtandao wa wauza unga hapa nchini kwa mujibu wa gazeti hilo.

Chanzo: Gazeti la Jamhuri

Majaji wanaowalinda wauza 'unga' wabainika
* Gazeti hili sasa limeamua kuwataja kwa majina
* Mahakimu nao wanawaachia mapapa kienyeji
* Kigogo ofisi ya DPP, Mahakama Temeke, Kinondoni balaa


Na Waandishi Wetu, Dar na Zanzibar

Mahakama kupitia baadhi ya majaji na mahakimu wasio waadilifu imebainika kuwa kikwazo kikubwa katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.
Pamoja na Mahakama, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP), nayo imelaumiwa kwa kufuta kesi katika mazingira ambayo hata mtu ambaye hakusoma sheria, anaweza kuyatilia shaka.
Wakati vyombo hivi vikikwamisha vita hii, lawama zimekuwa zikielekezwa kwa polisi na vyombo vingine vya usalama, ambavyo watendaji kazi wake wanafanya kazi usiku na mchana.
Juhudi zote zinazofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama zinagonga mwamba mahakamani kwa msaada wa ofisi hiyo ya DPP.
Wakati kesi nyingine zikifutwa, nyingine hazisikilizwi, kiasi cha kusababisha zirundikane mahakamani tangu mwaka 2005. Kesi chache zinazohusu watuhumiwa wakubwa wa kuuza ‘unga’ zinamalizwa haraka kwa utaratibu wa ofisi ya DPP kuwasilisha nia ya kutoendelea na mashtaka mahakamani (nolle prosequi) au wasimamizi hao wa utoaji haki kutoa hukumu zinazoacha wengi vinywa wazi na kuwakatisha tamaa polisi.
Katika hali ya kushangaza, majaji na mahakimu wamekuwa wakikiuka wazi Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya Na, 9 ya Mwaka 1995 inayozuia mtu yeyote aliyekamatwa na dawa zenye thamani kuanzia Sh milioni 10 asipewe dhamana, lakini hilo halizingatiwi. JAMHURI haikubahatika kufahamu bayana nini kinawapofusha majaji na mahakimu wakati ‘mapapa’ wanapofikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuuza unga, lakini ni wazi kuwa kuna mtandao mkubwa wa kulindwa kwa watuhumiwa hao wenye ukwasi mkubwa.
Wakati polisi wanafanya kazi ya hatari usiku muda wote, wakipambana na wauaji, wahongaji na watu wanaouza dawa za kulevya, kesi za mapapa zinamalizwa kienyeji mahakamani.
Moja ya kesi inayotia shaka ni Na. 47 ya Mwaka 2011. Kesi hii ilifunguliwa dhidi ya watuhumiwa Fredy William Chonde, Kambi Zuberi Seif; ambao ni Watanzania na Abdulghan Peer Bux na Shaaban Malik ambao ni raia wa Pakistani.
Hawa walikamatwa eneo la Mbezi Beach, Dar es Salaam wakiwa na kilo 175 za heroin, ambako kesi dhidi yao ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini humo. Wakati kesi inaendelea Kisutu, mawakili wa vigogo hawa walikwenda Mahakama Kuu wakafungua shauri la kuomba wapewe dhamana chini ya Jaji Pendo Msuya, wakitambua kuwa sheria inazuia.
Bila kuchukua jalada wala kuwasiliana na Mahakama ya Kisutu, huku Jaji Msuya akijua fika kuwa kilo 175 ambazo thamani yake ni zaidi ya Sh bilioni tano, na watuhumiwa hawapaswi kupewa dhamana; yeye kwa mamlaka aliyonayo kama Jaji aliamua kuwapa dhamana watuhumiwa hawa. Baada ya kupata dhamana, Wapakistani walirejeshewa pasipoti zao na wakakimbia nchi. Hawajakamatwa hadi leo.
“Cha kusikitisha kesi iliendelea bila kujua kuwa watuhumiwa wamekwishapewa dhamana na hadi Aprili 8, mwaka huu 2013 kesi hiyo ilitajwa… baadaye Mahakama ikapewa taarifa kuwa watuhumiwa walishapewa dhamana na Mahakama Kuu ndiyo maana hawaonekani mahakamani. Tulishangaa sana,” kilisema chanzo chetu kutoka Mahakama ya Kisutu.
Kesi nyingine iliyomalizwa kienyeji ni ya Mwinyi Rashid Mkoko. Vyanzo vya JAMHURI vinaonesha kuwa huyu na familia karibu yote wanatuhumiwa kufanya biashara ya dawa za kulevya. Ndugu zake waliokamatwa kwa nyakati tofauti na baba yao, ambako mmoja alidhulumiana, na ‘mzigo’ na wauza unga, hali iliyofanya wamuue kwa kumpiga risasi.
Katika familia hii, Rashid Ismail Mkoko ndiye aliyeuawa na wauza unga wenzake eneo la Ilala, Dar es Salaam. Huyu alipata kukamatwa kuhusiana na dawa za kulevya, ila pia kwa kosa la mauaji. Shuhuda wa tukio la Rashid Ismail Mkoko anasimulia kama ifuatavyo:

“Huyu ndiye wa kesi ile ambayo kijana aliyemtuma mzigo Pakistan pipi zilipasukia tumboni akafia gesti kule Tabata, Dar es Salaam. Mmoja wa ndugu wa kijana huyu aliyefariki, alimpigia simu akamwambia ‘si unajua alikuwa na mzigo wako ndiyo umemuua? Sasa mbona umetususa? Hata maji ya kunywa hutupatii msibani?’
“Mkoko akamwambia nitakuja jioni. Na kweli jioni iliyofuata akampigia simu kuwa anakwenda hapo nyumbani msibani. Alipofika akampigia simu, akamwambia njoo tuonane. Huyu ndugu wa kijana aliyefariki akatoka nje, akaenda kwenye gari kuonana na Mkoko.

“Alipofika Mkoko akamuuliza ndiye wewe uliyenipigia simu jana, yule ndugu wa marehemu akajibu ‘ndiyo’, basi Mkoko alichofanya akatoa bastola akampiga risasi ya usoni yule kijana…akafariki papo hapo, Mkoko akaondoka.

“Polisi walimkamata wakamfikisha mahakamani. Mahakama ikamwachia kwa mizengwe. Ila Mungu si Athumani, ikatokea naye akadhulumu wauza unga wenzake huko Ilala, nao wakamuwinda wakampiga risasi akafa mwaka juzi.

“Huyu alikuwa muuza dawa za kulevya mkubwa. Mdogo wake Mwinyi Rashid Mkoko, naye anauza dawa. Tulimkamata na heroin gramu 250 zenye thamani ya Sh milioni 11, ikafunguliwa kesi Temeke Na. PI 26 chini ya Hakimu Mkwawa, lakini ajabu wakati kesi inaendelea kutajwa Temeke hadi leo, huyu Mwinyi Mahakama Kuu imekwishamwachia huru bila vielelezo vyovyote,” kilisema chanzo chetu kutoka mahakamani.

Uchunguzi wa JAMHURI umeonesha kuwa awali mawakili wa Mwinyi waliwasilisha ombi la dhamana kwa Jaji Munisi, ambaye aliwaelekeza mawakili wa Serikali kuwa badala ya kumshtaki Mwinyi kwa kukutwa na dawa za kulevya, waiondoe kesi mahakamani na kuifungua upya kama kesi ya kusafirisha dawa za kulevya. Kwa kawaida tuhuma za aina hiyo huwa hazina dhamana.

Mawakili walivyopata mwanya huo, wanajua jinsi walivyozungumza na wanasheria wa Serikali. Kesi hiyo badala ya kuiondoa kama alivyoelekeza Jaji Munisi wakaihamishia kwa Jaji Dk. Fauz Twalib, ambaye katika hukumu yake ya Julai 30, 2012 alikiri kuwa mbele yake halikufikishwa jalada la kesi hiyo na wala hakuwa na mamlaka ya kuisikiliza kwani yeye si hakimu, ila akasema kwa kuwa Mahakama ya Temeke haina mamlaka ya kusikiliza kezi za dawa za kulevya kama cocaine, basi akatoa fursa ya kumsikiliza mtuhumiwa.

“Kwa kasi ya aina yake, siku hiyo hiyo ya Julai 30, 2012 baada ya Jaji Dk. Fauz kutoa hukumu hiyo ya ajabu, mawakili wa Serikali ambao ni upande wa mashitaka wakawasilisha nolle chini ya Section 91 ya CPA (Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka), hivyo Mwanasheria wa Serikali Mpembo kwa niaba ya DPP akawasilisha hati hiyo, na Jaji Fauz akaifuta kesi dhidi ya Mwinyi.

“Kisichoeleweka na kufahamika ni nini kilitokea na nini kiliendelea siku hiyo hiyo kutoa hukumu, na siku hiyo hiyo Mpembo akawasilisha nolle na kesi ikafutwa siku hiyo hiyo. Hapa kuna maswali mengi. Mwinyi amekimbilia Zanzibar. Yupo anaponda raha, kesi bado ipo Temeke na hakuna kinachoendelea,” kimesema chanzo chetu.

Baba yao Mwinyi na Rashid, naye kwa nyakati tofauti anadaiwa kukamatwa na polisi akituhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Mtoto wake mwingine, Abubakar Mkoko, yeye alitolewa dawa za kulevya tumboni, lakini Mahakama ikampiga faini ya Sh milioni 1 na kumwachia huru.

Kesi nyingine inayowakosesha usingizi polisi ni ile ya Dhoulkefly Awadh Abdallah Na. 238 ya Mwaka 2010. Kesi hii ilimhusisha Abdallah na mkewe Asha Seif Kiluvya. Asha ndiye aliyekamatwa na dawa za kulevya. Hata hivyo, katika mazingira ya kutatanisha, ofisi ya DPP ilipeleka nolle prosequi mahakamani Asha akaachiwa huru, na sasa anashitakiwa Abdallah ambaye hakukutwa na kitu chochote.

Kioja kinginge kilifanywa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kinondoni anayetajwa kwa jina la Msongo. Kesi hii ilianza mwaka 2005 na kumalizika mwaka 2008. Mshitakiwa alikuwa Yusufu Hassan Yossye, mkazi wa Kinondoni A, Mtaa wa Togo, aliyekutwa na gramu 1,244 za heroin ambazo alikamatwa nazo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam. Aliwekwa chini ya ulinzi kwa lengo la kumfanya atoe ‘pipi’ kwa njia ya haja kubwa. Katika hukumu ambayo inatia shaka Hakimu Msongo aliandika hivi:

“Katika ushahidi wote uliotolewa, hakuna ubishi kuwa ni kweli amekutwa na dawa za kulevya. Pia ushahidi unaonesha kuwa mshitakiwa alitoa madawa hayo kwa njia ya haja kubwa. Hata hivyo, upande wa mashitaka umeshindwa kueleza ni dalili zipi zilipelekea (zilisababisha) kushukiwa kuwa mshitakiwa ana madawa ya kulevya. Na pia hawakushirikishwa watu au wataalamu wa afya ya binadamu.

“Upande wa mashitaka katika ushahidi wao umeonesha walipishana kutoa idadi [ya pipi alizotoa kwa haja kubwa]. Kutokana na hilo, ushahidi hautoshelezi na mshitakiwa namwachia chini ya Kifungu cha 235 cha CPA (Kanuni ya Mwenendo wa Mashitaka) katika mashitaka yote mawili.” Hukumu hii ilitolewa na Hakimu Msongo Mei 2, 2008. Yossye alikuwa akishitakiwa kwa kukutwa na dawa; na pia kwa kuwaambia polisi uongo kuwa hakuwa na dawa, lakini baadaye akazitoa kwa njia ya haja kubwa.

Katika Mahakama ya Kisutu, mwanamke mwingine aliyetambuliwa kwa jina la Pilly, alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa na zawadi ya kinyago ambacho ndani yake kilikutwa na dawa za kulevya, lakini Mahakama ya Kisutu wakati inatoa taarifa ilimwachia huru Pilly kwa maelezo kuwa wakati polisi wanamkamata, hakuwapo mwanamke, hivyo ni kosa mhalifu mwanamke kukamatwa na polisi mwanaume. Akaachiwa huru!
Kesi nyingine ni ya Kwaku Sarfo, raia wa Ghana, alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere mnamo Novemba 14, 2010. Thamani ya dawa ilikuwa Sh milioni 390. Kesi ilipelekwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Samora kwa Hakimu Mkazi Luago.

“Tulishangaa, kwamba kwanza Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza kesi hii, lakini pia baada ya kupita siku 60; bila mamlaka kisheria, Hakimu Luago akaifuta. Hakimu huyu ni kero. Amehamishiwa Lindi akagoma kwenda. Hatujui anapewa jeuri na nani. Tungeomba Rais Kikwete na mhimili wa Mahakama waingilie kati suala hili vinginevyo nchi inateketea,” kimesema chanzo chetu.

Uchunguzi umebaini kuwa kati ya kesi 423 zilizofikishwa Mahakama Kuu kati ya mwaka 2005 na 2013 hadi leo kesi iliyokwisha ni moja tu ya Shaaban Mintanga, ambayo nayo imeisha kutokana na mashahidi muhimu kufariki dunia kabla kesi haijasikilizwa. Kati ya mashahidi waliofariki dunia ni Mkemia Mkuu, Dk. Ernest Mashimba, aliyefariki Septemba 2010.
Kamanda wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, alikiri matukio hayo kuwapo na akasema: “Mimi mamlaka yangu ni kukamata, na kuwafikisha mahakamani. Sasa huko kama mmekuta hali iko hivyo, ambayo ni kweli kimsingi inasikitisha na kukatisha tamaa, inabidi muwaulize huko mahakamani au kwa DPP wao ndiyo waeleze nini kinatokea.”
JAMHURI haikufanikiwa kuzungumza na Msajili wa Mahakama Kuu kwani mara zote kila mwandishi wetu alipofika aliambiwa yuko kwenye vikao kwa wiki nzima, na hata alipoacha ujumbe wa maandishi haukujibiwa.
Baada ya juhudi za kumpata Msajili wa Mahakama Kuu kugonga mwamba, JAMHURI iliwasiliana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi, ambaye Kamisheni ya Dawa za Kulevya iko chini yake. Yeye alisema ni kweli tatizo hilo lipo, na kwamba kuna mengi zaidi ya hayo.
“Mimi nasema sheria zinapaswa kubadilishwa, na Serikali tayari imeanza mchakato. Mtu akipatikana na pipi za dawa za kulevya zikatolewa tumboni mwake, nataka sheria irahisishwe na kuwezesha ashitakiwe na kufungwa maisha ndani ya siku saba.
“Hali ilivyo sasa ambapo unapaswa kuhifadhi ushahidi kwa miaka hadi 10 ukiendesha kesi moja, ushahidi unapoteza ubora. Wakati mwingine mtuhumiwa anashindwa kesi anatozwa faini ya Sh 500,000. Hatuwezi kupambana na dawa za kulevya tukashinda vita hii kwa utaratibu huo.
“Sasa Serikali imejipanga, ipo kwenye mchakato wa kuanzisha mahakama maalum ya kudhibiti dawa za kulevya na kwa kweli katika hili tunataka mchakato uwe mfupi kadiri inavyowezekana. Ndani ya muda mfupi kadiri inavyowezekana tupitishe sheria hii ili sheria iwe kali itoe adhabu itakayowazuia wengine kufanya biashara hii,” alisema Lukuvi.
Hivi karibuni, Tanzania imeanza kuzungukwa na sura ya kuwa Taifa la wauza dawa za kulevya baada ya Watanzania wengi kukamatwa ndani na nje ya nchi wakiwa na dawa hizo. Taarifa za uhakika zilizoifikia JAMHURI zinasema Rais Jakaya Kikwete ametoa maelekezo ya dhati kuhakikisha linafanyika jambo kubwa litakalowezesha kukamata mtandao wa wauza dawa za kulevya na kumaliza tatizo hili nchini.
Kwa mwezi mmoja sasa, JAMHURI imekuwa ikichapisha orodha ya wauza unga ‘dagaa’ na ‘mapapa’ hapa nchini, ambako hadi sasa gazeti hili limekwishatangaza hadharani majina ya wauza unga 504 katika matoleo manne yaliyotangulia.
Attached Thumbnails Attached Thumbnails Click image for larger version. 

Name: Majaji wanaolinda wauza unga_Page_2.jpg 
Views: 0 
Size: 156.2 KB 
ID: 109354   Click image for larger version. 

Name: Majaji wanaolinda wauza unga_Page_1.jpg 
Views: 0 
Size: 159.7 KB 
ID: 109353  

Friday, August 23, 2013

Taarifa ajali ya ndege iliyotokea Manyara


 
Ajali ya ndege iliyotokea jana mkoani manyara, ambapo ndege ya shirika la ndege la Tanzanair ilipata na kuangukia ziwa manyara, ndege hiyo iliyokua ikitokea Bukoba kuelekea Zanzibar ilipata ajali hiyo muda wa saa 2 asubuhi , ndani ya ndege kulikua na watu 7, wote waliokolewa, kati ya hao saba waili hawakuumia kabisa na wengine walijeruhiwa lakini walikimbizwa hospitali ya Serian iliyopo mjini arusha kwa ajili ya matibabu.