Kwa ufupi
- “Kuna pacha ambao wanakuwa kwenye mifuko tofauti na wengine wanakuwa kwenye mfuko mmoja, hawa wanaokuwa kwenye mfuko mmoja ndio mara nyingi wanashindwa kuachiana na hivyo wanazaliwa wakiwa wameungana.”Dk Edna Majaliwa, Msimamizi Wodi ya Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili
Mkazi wa Jang’ombe Visiwani Zanzibar, Pili Hija (24), amejifungua watoto walioungana huku mmoja akiwa hana kichwa.
Watoto hao ambao wapo Wodi namba 36 katika Jengo
la Wazazi la Hospitali ya Taifa Muhimbili mbali na kuzaliwa mmoja akiwa
hana kichwa, wameungana sehemu ya uti wa mgongo, mkono mmoja na
wanatumia njia moja ya haja kubwa.
Akizungumza jana, mama wa watoto
hao, alisema: “Nilijifungulia nyumbani, nilisikia uchungu mara moja na
hapo hapo nikajifungua kwa njia ya kawaida na jirani yangu ndiye
aliyenisaidia,”alisema na kuongeza:
“Nilijifungua saa moja asubuhi, nilijua nitazaa
pacha kwa kuwa nilishafanya kipimo katika Hospitali ya Makunduchi,
wakaniambia nitajifungua pacha lakini mmoja si binadamu ni kiwiliwili.
“Nimeolewa, mume wangu ni mwanajeshi, nina watoto
wengine wawili mmoja wa kike na mwingine wa kiume, mume wangu hajui
tukio hili kwani yupo kambini Zanzibar na hatuna mawasiliano yoyote kwa
sasa,” alisema.
Daktari wa Upasuaji wa Watoto Hospitali ya Taifa
Muhimbili, Dk Zaituni Bokhary alisema; “Hii ni mara ya kwanza kwa jambo
hili kutokea katika miaka ya hivi karibuni. Mara ya mwisho lilitokea
mwaka 1984.
“Tulikuwa tufanye upasuaji leo lakini tumeahirisha
na utafanyika Alhamisi (kesho) asubuhi katika Kitengo cha Mifupa cha
Muhimbili (Moi).”
Msimamizi wa Wodi ya Watoto walikolazwa, Dk Edna
Majaliwa alisema: “Hakuna sababu maalumu kitaalamu inayosababisha
watoto kuungana, mara nyingi zinapokutana mbegu za X na Y na kutengeneza
mimba kunakuwa na hatua za ukuaji wiki nne, wiki nane, wiki 12, 16 na
kuendelea.