Majaji wanaowalinda wauza 'unga' wabainika
* Gazeti hili sasa limeamua kuwataja kwa majina
* Mahakimu nao wanawaachia mapapa kienyeji
* Kigogo ofisi ya DPP, Mahakama Temeke, Kinondoni balaa
Na Waandishi Wetu, Dar na Zanzibar
Mahakama kupitia baadhi ya majaji
na mahakimu wasio waadilifu imebainika kuwa kikwazo kikubwa katika vita
dhidi ya dawa za kulevya nchini, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.
Pamoja na Mahakama, Ofisi ya
Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP), nayo imelaumiwa kwa kufuta kesi
katika mazingira ambayo hata mtu ambaye hakusoma sheria, anaweza
kuyatilia shaka.
Wakati vyombo hivi vikikwamisha
vita hii, lawama zimekuwa zikielekezwa kwa polisi na vyombo vingine vya
usalama, ambavyo watendaji kazi wake wanafanya kazi usiku na mchana.
Juhudi zote zinazofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama zinagonga mwamba mahakamani kwa msaada wa ofisi hiyo ya DPP.
Wakati kesi nyingine zikifutwa,
nyingine hazisikilizwi, kiasi cha kusababisha zirundikane mahakamani
tangu mwaka 2005. Kesi chache zinazohusu watuhumiwa wakubwa wa kuuza
‘unga’ zinamalizwa haraka kwa utaratibu wa ofisi ya DPP kuwasilisha nia
ya kutoendelea na mashtaka mahakamani (nolle prosequi) au wasimamizi hao wa utoaji haki kutoa hukumu zinazoacha wengi vinywa wazi na kuwakatisha tamaa polisi.
Katika hali ya kushangaza, majaji
na mahakimu wamekuwa wakikiuka wazi Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya
Na, 9 ya Mwaka 1995 inayozuia mtu yeyote aliyekamatwa na dawa zenye
thamani kuanzia Sh milioni 10 asipewe dhamana, lakini hilo
halizingatiwi. JAMHURI haikubahatika kufahamu bayana nini
kinawapofusha majaji na mahakimu wakati ‘mapapa’ wanapofikishwa
mahakamani kwa tuhuma za kuuza unga, lakini ni wazi kuwa kuna mtandao
mkubwa wa kulindwa kwa watuhumiwa hao wenye ukwasi mkubwa.
Wakati polisi wanafanya kazi ya
hatari usiku muda wote, wakipambana na wauaji, wahongaji na watu
wanaouza dawa za kulevya, kesi za mapapa zinamalizwa kienyeji
mahakamani.
Moja ya kesi inayotia shaka ni Na.
47 ya Mwaka 2011. Kesi hii ilifunguliwa dhidi ya watuhumiwa Fredy
William Chonde, Kambi Zuberi Seif; ambao ni Watanzania na Abdulghan
Peer Bux na Shaaban Malik ambao ni raia wa Pakistani.
Hawa walikamatwa eneo la Mbezi
Beach, Dar es Salaam wakiwa na kilo 175 za heroin, ambako kesi dhidi
yao ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini humo.
Wakati kesi inaendelea Kisutu, mawakili wa vigogo hawa walikwenda
Mahakama Kuu wakafungua shauri la kuomba wapewe dhamana chini ya Jaji
Pendo Msuya, wakitambua kuwa sheria inazuia.
Bila kuchukua jalada wala
kuwasiliana na Mahakama ya Kisutu, huku Jaji Msuya akijua fika kuwa
kilo 175 ambazo thamani yake ni zaidi ya Sh bilioni tano, na watuhumiwa
hawapaswi kupewa dhamana; yeye kwa mamlaka aliyonayo kama Jaji aliamua
kuwapa dhamana watuhumiwa hawa. Baada ya kupata dhamana, Wapakistani
walirejeshewa pasipoti zao na wakakimbia nchi. Hawajakamatwa hadi leo.
“Cha kusikitisha kesi iliendelea
bila kujua kuwa watuhumiwa wamekwishapewa dhamana na hadi Aprili 8,
mwaka huu 2013 kesi hiyo ilitajwa… baadaye Mahakama ikapewa taarifa
kuwa watuhumiwa walishapewa dhamana na Mahakama Kuu ndiyo maana
hawaonekani mahakamani. Tulishangaa sana,” kilisema chanzo chetu kutoka
Mahakama ya Kisutu.
Kesi nyingine iliyomalizwa kienyeji ni ya Mwinyi Rashid Mkoko. Vyanzo vya JAMHURI
vinaonesha kuwa huyu na familia karibu yote wanatuhumiwa kufanya
biashara ya dawa za kulevya. Ndugu zake waliokamatwa kwa nyakati tofauti
na baba yao, ambako mmoja alidhulumiana, na ‘mzigo’ na wauza unga,
hali iliyofanya wamuue kwa kumpiga risasi.
Katika familia hii, Rashid Ismail
Mkoko ndiye aliyeuawa na wauza unga wenzake eneo la Ilala, Dar es
Salaam. Huyu alipata kukamatwa kuhusiana na dawa za kulevya, ila pia
kwa kosa la mauaji. Shuhuda wa tukio la Rashid Ismail Mkoko anasimulia
kama ifuatavyo:
“Huyu ndiye wa kesi ile
ambayo kijana aliyemtuma mzigo Pakistan pipi zilipasukia tumboni akafia
gesti kule Tabata, Dar es Salaam. Mmoja wa ndugu wa kijana huyu
aliyefariki, alimpigia simu akamwambia ‘si unajua alikuwa na mzigo wako
ndiyo umemuua? Sasa mbona umetususa? Hata maji ya kunywa hutupatii
msibani?’
“Mkoko akamwambia nitakuja jioni.
Na kweli jioni iliyofuata akampigia simu kuwa anakwenda hapo nyumbani
msibani. Alipofika akampigia simu, akamwambia njoo tuonane. Huyu ndugu
wa kijana aliyefariki akatoka nje, akaenda kwenye gari kuonana na
Mkoko.
“Alipofika Mkoko akamuuliza
ndiye wewe uliyenipigia simu jana, yule ndugu wa marehemu akajibu
‘ndiyo’, basi Mkoko alichofanya akatoa bastola akampiga risasi ya usoni
yule kijana…akafariki papo hapo, Mkoko akaondoka.
“Polisi walimkamata wakamfikisha mahakamani. Mahakama ikamwachia kwa
mizengwe. Ila Mungu si Athumani, ikatokea naye akadhulumu wauza unga
wenzake huko Ilala, nao wakamuwinda wakampiga risasi akafa mwaka juzi.
“Huyu alikuwa muuza dawa za
kulevya mkubwa. Mdogo wake Mwinyi Rashid Mkoko, naye anauza dawa.
Tulimkamata na heroin gramu 250 zenye thamani ya Sh milioni 11,
ikafunguliwa kesi Temeke Na. PI 26 chini ya Hakimu Mkwawa, lakini ajabu
wakati kesi inaendelea kutajwa Temeke hadi leo, huyu Mwinyi Mahakama
Kuu imekwishamwachia huru bila vielelezo vyovyote,” kilisema chanzo
chetu kutoka mahakamani.
Uchunguzi wa JAMHURI
umeonesha kuwa awali mawakili wa Mwinyi waliwasilisha ombi la dhamana
kwa Jaji Munisi, ambaye aliwaelekeza mawakili wa Serikali kuwa badala
ya kumshtaki Mwinyi kwa kukutwa na dawa za kulevya, waiondoe kesi
mahakamani na kuifungua upya kama kesi ya kusafirisha dawa za kulevya.
Kwa kawaida tuhuma za aina hiyo huwa hazina dhamana.
Mawakili walivyopata mwanya
huo, wanajua jinsi walivyozungumza na wanasheria wa Serikali. Kesi hiyo
badala ya kuiondoa kama alivyoelekeza Jaji Munisi wakaihamishia kwa
Jaji Dk. Fauz Twalib, ambaye katika hukumu yake ya Julai 30, 2012
alikiri kuwa mbele yake halikufikishwa jalada la kesi hiyo na wala
hakuwa na mamlaka ya kuisikiliza kwani yeye si hakimu, ila akasema kwa
kuwa Mahakama ya Temeke haina mamlaka ya kusikiliza kezi za dawa za
kulevya kama cocaine, basi akatoa fursa ya kumsikiliza mtuhumiwa.
“Kwa kasi ya aina yake, siku
hiyo hiyo ya Julai 30, 2012 baada ya Jaji Dk. Fauz kutoa hukumu hiyo
ya ajabu, mawakili wa Serikali ambao ni upande wa mashitaka
wakawasilisha nolle chini ya Section 91 ya CPA (Sheria ya
Mwenendo wa Mashitaka), hivyo Mwanasheria wa Serikali Mpembo kwa niaba
ya DPP akawasilisha hati hiyo, na Jaji Fauz akaifuta kesi dhidi ya
Mwinyi.
“Kisichoeleweka na
kufahamika ni nini kilitokea na nini kiliendelea siku hiyo hiyo kutoa
hukumu, na siku hiyo hiyo Mpembo akawasilisha nolle na kesi
ikafutwa siku hiyo hiyo. Hapa kuna maswali mengi. Mwinyi amekimbilia
Zanzibar. Yupo anaponda raha, kesi bado ipo Temeke na hakuna
kinachoendelea,” kimesema chanzo chetu.
Baba yao Mwinyi na Rashid,
naye kwa nyakati tofauti anadaiwa kukamatwa na polisi akituhumiwa
kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Mtoto wake mwingine,
Abubakar Mkoko, yeye alitolewa dawa za kulevya tumboni, lakini Mahakama
ikampiga faini ya Sh milioni 1 na kumwachia huru.
Kesi nyingine inayowakosesha
usingizi polisi ni ile ya Dhoulkefly Awadh Abdallah Na. 238 ya Mwaka
2010. Kesi hii ilimhusisha Abdallah na mkewe Asha Seif Kiluvya. Asha
ndiye aliyekamatwa na dawa za kulevya. Hata hivyo, katika mazingira ya
kutatanisha, ofisi ya DPP ilipeleka nolle prosequi mahakamani Asha akaachiwa huru, na sasa anashitakiwa Abdallah ambaye hakukutwa na kitu chochote.
Kioja kinginge kilifanywa na
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kinondoni anayetajwa kwa jina la Msongo.
Kesi hii ilianza mwaka 2005 na kumalizika mwaka 2008. Mshitakiwa
alikuwa Yusufu Hassan Yossye, mkazi wa Kinondoni A, Mtaa wa Togo,
aliyekutwa na gramu 1,244 za heroin ambazo alikamatwa nazo katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam. Aliwekwa
chini ya ulinzi kwa lengo la kumfanya atoe ‘pipi’ kwa njia ya haja
kubwa. Katika hukumu ambayo inatia shaka Hakimu Msongo aliandika hivi:
“Katika ushahidi wote
uliotolewa, hakuna ubishi kuwa ni kweli amekutwa na dawa za kulevya.
Pia ushahidi unaonesha kuwa mshitakiwa alitoa madawa hayo kwa njia ya
haja kubwa. Hata hivyo, upande wa mashitaka umeshindwa kueleza ni
dalili zipi zilipelekea (zilisababisha) kushukiwa kuwa mshitakiwa ana
madawa ya kulevya. Na pia hawakushirikishwa watu au wataalamu wa afya
ya binadamu.
“Upande wa mashitaka katika
ushahidi wao umeonesha walipishana kutoa idadi [ya pipi alizotoa kwa
haja kubwa]. Kutokana na hilo, ushahidi hautoshelezi na mshitakiwa
namwachia chini ya Kifungu cha 235 cha CPA (Kanuni ya Mwenendo wa
Mashitaka) katika mashitaka yote mawili.” Hukumu hii ilitolewa na
Hakimu Msongo Mei 2, 2008. Yossye alikuwa akishitakiwa kwa kukutwa na
dawa; na pia kwa kuwaambia polisi uongo kuwa hakuwa na dawa, lakini
baadaye akazitoa kwa njia ya haja kubwa.
Katika Mahakama ya Kisutu,
mwanamke mwingine aliyetambuliwa kwa jina la Pilly, alikamatwa Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa na zawadi ya kinyago
ambacho ndani yake kilikutwa na dawa za kulevya, lakini Mahakama ya
Kisutu wakati inatoa taarifa ilimwachia huru Pilly kwa maelezo kuwa
wakati polisi wanamkamata, hakuwapo mwanamke, hivyo ni kosa mhalifu
mwanamke kukamatwa na polisi mwanaume. Akaachiwa huru!
Kesi nyingine ni ya Kwaku Sarfo,
raia wa Ghana, alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere mnamo
Novemba 14, 2010. Thamani ya dawa ilikuwa Sh milioni 390. Kesi
ilipelekwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Samora kwa Hakimu Mkazi Luago.
“Tulishangaa, kwamba kwanza
Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza kesi hii, lakini pia baada ya
kupita siku 60; bila mamlaka kisheria, Hakimu Luago akaifuta. Hakimu
huyu ni kero. Amehamishiwa Lindi akagoma kwenda. Hatujui anapewa jeuri
na nani. Tungeomba Rais Kikwete na mhimili wa Mahakama waingilie kati
suala hili vinginevyo nchi inateketea,” kimesema chanzo chetu.
Uchunguzi umebaini kuwa kati
ya kesi 423 zilizofikishwa Mahakama Kuu kati ya mwaka 2005 na 2013
hadi leo kesi iliyokwisha ni moja tu ya Shaaban Mintanga, ambayo nayo
imeisha kutokana na mashahidi muhimu kufariki dunia kabla kesi
haijasikilizwa. Kati ya mashahidi waliofariki dunia ni Mkemia Mkuu, Dk.
Ernest Mashimba, aliyefariki Septemba 2010.
Kamanda wa Kikosi Maalumu cha
Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, alikiri matukio hayo kuwapo na
akasema: “Mimi mamlaka yangu ni kukamata, na kuwafikisha mahakamani.
Sasa huko kama mmekuta hali iko hivyo, ambayo ni kweli kimsingi
inasikitisha na kukatisha tamaa, inabidi muwaulize huko mahakamani au
kwa DPP wao ndiyo waeleze nini kinatokea.”
JAMHURI
haikufanikiwa kuzungumza na Msajili wa Mahakama Kuu kwani mara zote
kila mwandishi wetu alipofika aliambiwa yuko kwenye vikao kwa wiki
nzima, na hata alipoacha ujumbe wa maandishi haukujibiwa.
Baada ya juhudi za kumpata Msajili wa Mahakama Kuu kugonga mwamba, JAMHURI
iliwasiliana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu
wa Bunge), William Lukuvi, ambaye Kamisheni ya Dawa za Kulevya iko
chini yake. Yeye alisema ni kweli tatizo hilo lipo, na kwamba kuna
mengi zaidi ya hayo.
“Mimi nasema sheria zinapaswa
kubadilishwa, na Serikali tayari imeanza mchakato. Mtu akipatikana na
pipi za dawa za kulevya zikatolewa tumboni mwake, nataka sheria
irahisishwe na kuwezesha ashitakiwe na kufungwa maisha ndani ya siku
saba.
“Hali ilivyo sasa ambapo unapaswa
kuhifadhi ushahidi kwa miaka hadi 10 ukiendesha kesi moja, ushahidi
unapoteza ubora. Wakati mwingine mtuhumiwa anashindwa kesi anatozwa
faini ya Sh 500,000. Hatuwezi kupambana na dawa za kulevya tukashinda
vita hii kwa utaratibu huo.
“Sasa Serikali imejipanga, ipo
kwenye mchakato wa kuanzisha mahakama maalum ya kudhibiti dawa za
kulevya na kwa kweli katika hili tunataka mchakato uwe mfupi kadiri
inavyowezekana. Ndani ya muda mfupi kadiri inavyowezekana tupitishe
sheria hii ili sheria iwe kali itoe adhabu itakayowazuia wengine
kufanya biashara hii,” alisema Lukuvi.
Hivi karibuni, Tanzania imeanza
kuzungukwa na sura ya kuwa Taifa la wauza dawa za kulevya baada ya
Watanzania wengi kukamatwa ndani na nje ya nchi wakiwa na dawa hizo.
Taarifa za uhakika zilizoifikia JAMHURI zinasema Rais Jakaya
Kikwete ametoa maelekezo ya dhati kuhakikisha linafanyika jambo kubwa
litakalowezesha kukamata mtandao wa wauza dawa za kulevya na kumaliza
tatizo hili nchini.
Kwa mwezi mmoja sasa, JAMHURI
imekuwa ikichapisha orodha ya wauza unga ‘dagaa’ na ‘mapapa’ hapa
nchini, ambako hadi sasa gazeti hili limekwishatangaza hadharani majina
ya wauza unga 504 katika matoleo manne yaliyotangulia.