Wednesday, September 26, 2012

Mwalimu amropokea Waziri



NAIBU Waziri wa Elimu na Ufundi Stadi, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi kwa muda Mwalimu wa Sekondari ya vipaji maalumu Ilboru, Potin Sumawe kwa madai ya kulewa kazini na kuropoka.

Majaliwa ambaye jana alilazimika kwenda shuleni hapo kuzungumza na wajumbe wa Bodi ya Shule, walimu na wanafunzi ili kufahamu kiini cha matatizo yaliyosababisha juzi wanafunzi kuandamana, alimsimamisha mwalimu huyo wakati kikao kikiendelea.

Wakati Naibu Waziri akihoji sababu za hali iliyoikumba shule, mwalimu huyo aliingilia kati na kuzungumza katika hali iliyosadikiwa kuwa ya ulevi akisema, “mkuu tupo hapa walimu, hawa wanafunzi wanaleta ugomvi sisi walimu tunafundisha”.

“Kwa nini unazungumza wakati hujapewa nafasi ya kuzungumza,” alihoji Majaliwa na kuamuru apelekwe hospitalini apimwe kubaini kama amechanganyikiwa au ni ulevi.

“Nimemwagiza Ofisa Utumishi kumpeleka hospitalini, kupimwa kama amechanganyikiwa na ripoti itakayotolewa iletwe kwangu, ili nijue ni ulevi au la; hivyo namsimamisha kazi na kuanza kupitia jalada lake, tuone kama anaweza kuonywa au la … tutachukua hatua,” alisema Majaliwa. Kutokana na tukio hilo, alionya watumishi dhidi ya unywaji pombe saa za kazi, huku akiwataka kuheshimu kazi kwa kufuata sheria ya utumishi wa umma.

“Kama mtumishi wa umma unavunja sheria kwa kunywa pombe kazini, utachukuliwa hatua, kwa kuwa hata yule mtoto uliyekabidhiwa kumfundisha, hutaweza kumfundisha kwa misingi mizuri, hivyo mfanye kazi kwa maadili,” alionya.

Alisema tabia ya ulevi kazini haikatazwi shuleni tu, bali sehemu yoyote mfanyakazi wa Serikali au sekta binafsi, haruhusiwi kufanya kazi huku amelewa, hivyo mtu akikutwa katika hali hiyo atafukuzwa kazi.

Baadhi ya walimu ambao hawakuwa tayari majina yao yaandikwe gazetini, walimwomba Naibu Waziri aifunge shule hiyo kwa muda, hadi wanafunzi watakapoandikiwa barua za kuitwa, kwa sababu walimu wamepoteza imani nao wakidai wanafunzi wanachochewa na viongozi wa juu serikalini, kuandamana.

Nao wanafunzi walimwomba Naibu Waziri, amhamishe Mkuu wa Shule, Jovinus Mutabuzi wakimtuhumu kwa ubadhirifu na kuwatishia wanapofuatilia taarifa za shule.

Mkuu wa Shule alisema kwa sasa hawezi kuongelea kitu chochote, kwa sababu bado yuko kwenye mazungumzo na Naibu Waziri na uamuzi wa kitakachoafikiwa utatolewa.

Juzi wanafunzi wa shule hiyo waliandamana hadi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakishinikiza Mkuu wa Shule aondolewe.