Msikiti wajengwa Kanisani Dar
TUKIO la kipekee zaidi nchini linalogusa vibaya mahusiano kati ya dini
ya Kikristo na ya Kiislamu limetokea jijini Dar es Salaam. Tukio hilo ni
la Waislamu kununua nyumba iliyokuwa usoni mwa kanisa moja la kilokole
na kisha kuamua kujenga msikiti papo hapo, kiasi ambacho mapaa yanaweza
hata kugusana.
Kanisa hilo la Assemblies of God, Keko, limekuwepo hapo na
linatumiwa kwa ibada kwa zaidi ya miaka miwili ingawa ujenzi wake
haujakamilika, lakini ujenzi wa msikiti unaokwenda kwa kasi kubwa ya
usiku na mchana umeanza kiasi cha majuma mawili hivi yaliyopita.
Msimamizi wa ujenzi huo aliyejitambulisha kwa
ufupi tu kama Sheikh Lukinga, alisema mwishoni mwa wiki
kuwa fedha zinazotumika kujengea msikiti huo zimetolewa na kampuni moja
ya mafuta kutoka Uarabuni iliyoko nchini iitwayo Oil-Com.
Sheikh huyo alisema, Oil-Com, ndio waliowanunulia kiwanja katika
eneo hilo baada ya wao kupendekeza kuwa wanapapenda zaidi hapo
"kanisani" kwani kuko barabarani na pia wanataka kutekeleza alichokiita
"agizo la Serikali" kwamba dini zote zisali pamoja kuonyesha umoja na
mshikamano.
"Hujasikia Bwana serikali ikisisitiza watu kusali pamoja? Wao
(Wakristo) kama wana hofu ni juu yao sisi hatuna cha kuhofia; tutaswali
na tunaamini kuwa hakuna mwenye kuweza kutubughudhi," alisema Sheikh
Lukinga.
Imamu Lukinga,pia alisema, miaka ishirini iliyopita Waislamu
walikuwa na msikiti katika maeneo ya karibu na hapo, lakini Serikali
iliuza eneo hilo kwa "kalasinga" mmoja ambaye alitakiwa awalipe fidia
wenyeji akashindwa, na ndipo baadaye kampuni ya Oil-Com, ikajitokeza
kupanunua na kuwalipa wananchi.
Alisema(Lukinga) kuwa hapo Waislamu, walikataa kupokea fedha
taslimu na wakataka wajengewe msikiti, ndipo wakapendekeza wajengewe
katika eneo hilo.
"Baada ya wamiliki wa Oil-Com kukubaliana na masharti yetu
walitutaka tupendekeze eneo ambalo tunataka tujengewe msikiti mpya na
eneo hili lilikuwa na nyumba ya kawaida ambayo tuliinunua na kisha
tukapendekeza kujengewa msikiti hapa," alisema Sheikh huyo.
kufuatia ujenzi wa msikiti huo Mchungaji wa Kanisa hilo Paulo
Shemsanga, amewatangazia waumini wake kuendesha maombi maalum ya kufunga
na kumlilia Mungu aingilie kati hali hiyo. Maombi yalianza rasmi
Jumapili iliyopita.
Kwa mujibu wa Waumini wa Kanisa hilo lililopo eneo la Keko
Molem, Jumapili iliyopita Mchungaji wao aliwatangazi kuwa nyumba
inayojengwa umbali wa kama hatua moja tu kutoka kwenye mlango wa kanisa
lao ni msikiti, hivyo waumini wote waendeshe maombi maalum ili kumlilia
Mungu kwa kuwa inaonekana kuwa hivyo ni vita vya kiroho.
Nyakati" lilipotembelea kanisani hapo Jumatano na Alhamisi ya
wiki iliyopita liliwakuta mafundi wakiendelea kujenga msikiti huo huku
baadhi ya kuta zikiwa zimefika usawa wa madirisha na wakisimamiwa na
baadhi ya Waislamu waliokuwa wamevalia kanzu na "baraghashia".
Sheikh Lukinga, alisema kuwa iwapo kuna haja ya kundi moja
kuhamisha nyumba yao ya ibada, basi Wakristo ndio wafanye hivyo,lakini
si wao (Waislamu) kwa kuwa eneo hilo wao wamekuwa wakiswali kwa muda
mrefu sana, japo sio hapo hapo wanakojenga sasa.
Nyakati ilipofika nyumbani kwa mchungaji Shemsanga kuzungumzia
suala hilo haikumkuta lakini mkewe, Mama Shemsanga, alisema kuwa ni
kweli kuwa hali kwa sasa ni ya wasiwasi na Jumapili iliyopita
walitangaziwa kuomba ili Mungu aingilie kati.
Alisema kuwa ingawa yeye si msemaji wa kanisa lakini kama
muumini ameshuhudia mambo mbalimbali ambayo yanadhihirisha wazi kuwa
eneo hilo lina vita ya kiroho na wapo watu wasiopenda wao wasali hapo.
Alisema katika siku za karibuni mmoja wa vijana wa kanisa hilo
aliokota karatasi iliyoandikwa maandishi waliyohisi ni ya lugha ya
kiarabu na kuwekwa kanisani hapo na hawakujua ni nani kafanya hivyo,
ambapo waliyateketeza kwa moto kwa jina la Yesu.
"Si hivyo, tu kwani juzi kuna mmoja wa akinamama wa kanisani
ambaye awali alikuwa Muislamu kabla ya kufunuliwa neno na kisha kumpokea
Bwana Yesu, alituambia kuwa Waislamu walifika kwa shemeji yake jirani
na nyumbani anakoishi wakihoji na kisha kuandikisha majina ya Waislamu
wote kwenye eneo hilo kwa kile walichodai kuwa wanahitaji ushirikiano
maalum katika kipindi hiki,," alisema Mama Mchungaji, na kuongeza kuwa
wanaamini uandikishaji huo ni sehemu ya mapambano hayo ya kiroho.
"Nyakati" liliambiwa kuwa Mchungaji Shemsanga, Alihamisi
iliyopita alikuwa amekwenda ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
kufuatilia taarifa alizopeleka huko kuhusu ujenzi wa msikiti huo nje ya
kanisa.
Hata hivyo, kwa kuwa Mchungaji mwenyewe hakupatikana hadi
tunakwenda mitambani, haikuweza kufahamika kuwa alipata jibu gani kuhusu
suala hilo ambalo linaonekana kuwa ni jipya katika mitafaruku ya kidini
nchini.