Msikiti wajengwa Kanisani Dar
TUKIO la kipekee zaidi nchini linalogusa vibaya mahusiano kati ya dini ya Kikristo na ya Kiislamu limetokea jijini Dar es Salaam. Tukio hilo ni la Waislamu kununua nyumba iliyokuwa usoni mwa kanisa moja la kilokole na kisha kuamua kujenga msikiti papo hapo, kiasi ambacho mapaa yanaweza hata kugusana.
Kanisa hilo la Assemblies of God, Keko, limekuwepo hapo na linatumiwa kwa ibada kwa zaidi ya miaka miwili ingawa ujenzi wake haujakamilika, lakini ujenzi wa msikiti unaokwenda kwa kasi kubwa ya usiku na mchana umeanza kiasi cha majuma mawili hivi yaliyopita.
Msimamizi wa ujenzi huo aliyejitambulisha kwa ufupi tu kama Sheikh Lukinga, alisema mwishoni mwa wiki kuwa fedha zinazotumika kujengea msikiti huo zimetolewa na kampuni moja ya mafuta kutoka Uarabuni iliyoko nchini iitwayo Oil-Com.
Sheikh huyo alisema, Oil-Com, ndio waliowanunulia kiwanja katika eneo hilo baada ya wao kupendekeza kuwa wanapapenda zaidi hapo "kanisani" kwani kuko barabarani na pia wanataka kutekeleza alichokiita "agizo la Serikali" kwamba dini zote zisali pamoja kuonyesha umoja na mshikamano.
"Hujasikia Bwana serikali ikisisitiza watu kusali pamoja? Wao (Wakristo) kama wana hofu ni juu yao sisi hatuna cha kuhofia; tutaswali na tunaamini kuwa hakuna mwenye kuweza kutubughudhi," alisema Sheikh Lukinga.
Imamu Lukinga,pia alisema, miaka ishirini iliyopita Waislamu walikuwa na msikiti katika maeneo ya karibu na hapo, lakini Serikali iliuza eneo hilo kwa "kalasinga" mmoja ambaye alitakiwa awalipe fidia wenyeji akashindwa, na ndipo baadaye kampuni ya Oil-Com, ikajitokeza kupanunua na kuwalipa wananchi.
Alisema(Lukinga) kuwa hapo Waislamu, walikataa kupokea fedha taslimu na wakataka wajengewe msikiti, ndipo wakapendekeza wajengewe katika eneo hilo.
"Baada ya wamiliki wa Oil-Com kukubaliana na masharti yetu walitutaka tupendekeze eneo ambalo tunataka tujengewe msikiti mpya na eneo hili lilikuwa na nyumba ya kawaida ambayo tuliinunua na kisha tukapendekeza kujengewa msikiti hapa," alisema Sheikh huyo.
kufuatia ujenzi wa msikiti huo Mchungaji wa Kanisa hilo Paulo Shemsanga, amewatangazia waumini wake kuendesha maombi maalum ya kufunga na kumlilia Mungu aingilie kati hali hiyo. Maombi yalianza rasmi Jumapili iliyopita.
Kwa mujibu wa Waumini wa Kanisa hilo lililopo eneo la Keko Molem, Jumapili iliyopita Mchungaji wao aliwatangazi kuwa nyumba inayojengwa umbali wa kama hatua moja tu kutoka kwenye mlango wa kanisa lao ni msikiti, hivyo waumini wote waendeshe maombi maalum ili kumlilia Mungu kwa kuwa inaonekana kuwa hivyo ni vita vya kiroho.
Nyakati" lilipotembelea kanisani hapo Jumatano na Alhamisi ya wiki iliyopita liliwakuta mafundi wakiendelea kujenga msikiti huo huku baadhi ya kuta zikiwa zimefika usawa wa madirisha na wakisimamiwa na baadhi ya Waislamu waliokuwa wamevalia kanzu na "baraghashia".
Sheikh Lukinga, alisema kuwa iwapo kuna haja ya kundi moja kuhamisha nyumba yao ya ibada, basi Wakristo ndio wafanye hivyo,lakini si wao (Waislamu) kwa kuwa eneo hilo wao wamekuwa wakiswali kwa muda mrefu sana, japo sio hapo hapo wanakojenga sasa.
Nyakati ilipofika nyumbani kwa mchungaji Shemsanga kuzungumzia suala hilo haikumkuta lakini mkewe, Mama Shemsanga, alisema kuwa ni kweli kuwa hali kwa sasa ni ya wasiwasi na Jumapili iliyopita walitangaziwa kuomba ili Mungu aingilie kati.
Alisema kuwa ingawa yeye si msemaji wa kanisa lakini kama muumini ameshuhudia mambo mbalimbali ambayo yanadhihirisha wazi kuwa eneo hilo lina vita ya kiroho na wapo watu wasiopenda wao wasali hapo.
Alisema katika siku za karibuni mmoja wa vijana wa kanisa hilo aliokota karatasi iliyoandikwa maandishi waliyohisi ni ya lugha ya kiarabu na kuwekwa kanisani hapo na hawakujua ni nani kafanya hivyo, ambapo waliyateketeza kwa moto kwa jina la Yesu.
"Si hivyo, tu kwani juzi kuna mmoja wa akinamama wa kanisani ambaye awali alikuwa Muislamu kabla ya kufunuliwa neno na kisha kumpokea Bwana Yesu, alituambia kuwa Waislamu walifika kwa shemeji yake jirani na nyumbani anakoishi wakihoji na kisha kuandikisha majina ya Waislamu wote kwenye eneo hilo kwa kile walichodai kuwa wanahitaji ushirikiano maalum katika kipindi hiki,," alisema Mama Mchungaji, na kuongeza kuwa wanaamini uandikishaji huo ni sehemu ya mapambano hayo ya kiroho.
"Nyakati" liliambiwa kuwa Mchungaji Shemsanga, Alihamisi iliyopita alikuwa amekwenda ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kufuatilia taarifa alizopeleka huko kuhusu ujenzi wa msikiti huo nje ya kanisa.
Hata hivyo, kwa kuwa Mchungaji mwenyewe hakupatikana hadi tunakwenda mitambani, haikuweza kufahamika kuwa alipata jibu gani kuhusu suala hilo ambalo linaonekana kuwa ni jipya katika mitafaruku ya kidini nchini.