Kaimu Mkurugenzi wa manispaa ya Singida,William Haalyakitoa taarifa yake ya utendaji kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya serikali za mitaa.
Mkuu wa wilaya ya Singida mwalimu Queen Mlozi, akifurahia jambo na kaimu mstahiki meya wa manispaa ya Singida,Pantaleo Sorongai muda mfupi kabla DC huyo hajaanza kuhutubia wakazi wa manispaa ya Singida (hawapo kwenye picha)wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku za serikali za mitaa.Maadhimisho hayo yalifanyika kwenye viwanja vya Ipembe.
Mkuu wa wilaya ya Singida Mwalimu Queen Mlozi akihutubia wananchi waliohudhuria maadhimisho ya siku ya serikali za mitaa (hawapo kwenye picha).
Baadhi ya viongozi waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya siku ya serikali za mitaa.
Kikundi cha burudani cha Nyota njema kikitoa burudani kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya serikali za mitaa zilizofanyika kwenye viwanja vya Ipembe mjini Singida.
Serikali wilayani Singida, imewaagiza madiwani wa manispaa ya Singida kuhakikisha wanabana mianya yote ya ufujaji wa fedha na mali za umma ili pamoja na mambo mengine,manispaa iweze kuwa imara kiuchumi.
Wito huo umetolewa na mkuu wa wilaya ya Singida,mwalimu Queen Mlozi,wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya serikali za mitaa zilizofanyika kwenye viwanja vya Ipembe mjini hapa.
Alisema madiwani wana jukumu kubwa la kuhakikisha lengo la ukusanyaji mapato linafikiwa na wakati huo huo,fedha zinatumika kama zilivyokusudiwa na si vinginevyo.
Mlozi alisema hilo liende sambamba na kuwahimiza wananchi kuchangia kwa hali na mali miradi yote ya maendeleo yao.
“Hapa niwaombe wananchi waondokane na dhana potofu kuwa serikali inao uwezo wa kuwaletea wananchi wake maendeleo endelevu. Kutokana na na ufinyu wa bajeti,serikali pekee haiwezi kukidhi mahitaji yote ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.Maendeleo ya kweli,yataletwa na wananchi wenyewe”,alifafanua DC huyo.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ya mwaka huu ni “shiriki sensa ya watu,toa maoni kuhusu katiba mpya ili kuimarisha ugatuaji wa madaraka kwa wananchi kwa maendeleo yao”.