Tuesday, July 17, 2012

Dk. Slaa: CCM wachochezi

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema kuwa wamebaini mpango wa makusudi unaofanywa na Chama cha Mapinduzi (CCM) ndani na nje ya Bunge kwa lengo la kuwahujumu.
Akizungumza na Tanzania Daima jana jioni, Dk. Slaa, alisema kuwa amelazimika kutoa tahadhari hiyo kutokana na dalili na njama alizoziona zikifanywa na CCM bungeni kupitia kwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Uchumi na Fedha, Mwigulu Mchemba, ambaye pia ni mbunge wa Iramba Magharibi.
“Leo nimemwona Mwigulu bungeni anadai eti Chedema tumefanya vurugu Singida juzi na kumuua kada wao, halafu mchana Mwenyekiti wa UVCCM wa Vyuo Vikuu, Abubakar Asenga, alizungumza na waandishi akaonyesha waraka feki na kudai ni maazimio ya Kamati Kuu ya chama chetu,” alisema Dk. Slaa.
Katibu huyo, alisisitiza kuwa CCM ndiyo waliofanya vurugu kwenye mkutano wa CHADEMA uliofanyika huko mkoani Singida na kwamba taarifa za uwepo wa vujo hizo zilikuwepo mapema lakini akashangazwa na Mwigulu, kukimbilia bungeni na kusema uongo.
Kuhusu madai ya Spika Makinda kudai kuwa amepokea majina ya wabunge wa CHADEMA wanaodaiwa kumtumia ujumbe wa vitisho Mwigullu, Dk. Slaa alisema anamshangaa kwa kuligeuza Bunge kuwa mahakama na hivyo, akashauri kuwa madai hayo lazima yaripotiwe polisi si bungeni.
“Sasa hizi ni mbinu zimeandaliwa kwa kuwakodi watu kufanya vurugu kwenye mikutano yetu na kueneza maneo ya uchochezi ili CHADEMA tuonekane ni chama cha vujo. Nimeseme kwamba hatuko tayari kufanyiwa mchezo huo na hao wanaotumika kufanya hivyo waache mara moja,” alionya.
Kuhusu waraka uliosambazwa jana na Asenga, ukidaiwa ni maazimio ya CC ya CHADEMA ya hivi karibuni unaokihusisha na kuchochea mgomo wa madaktari na ule wa walimu unaofukuta, Dk. Slaa, alisema kuwa aliyeuandaa ni mpumbavu kwa vile mambo yaliyoandikwa humo yanaihusu CCM.
“Kwanza wewe ni shahidi na mchango wa Mwigulu bungeni kila mtu anaufahamu, sasa leo kuandika waraka wa kijinga kama huu ukisema CHADEMA inataka kumdhoofisha kwa kuwa ni mtetezi makini wa watu, napata shida sana huyu ana umakini gani na amemtetea nani bungeni,” alihoji Dk. Slaa.
Mbali na mengi aliyozungumza kuhusu waraka huo, Dk. Slaa alishangazwa kuona ukihusishwa kuwa umetoka kwake lakini hakuna saini ya kuonyesha ukweli kuwa aliiandika yeye badala yake limewekwa jina na salamu ambayo si ya CHADEMA.
“Sisi salamu yetu ni ‘People’s Power’…hiyo ya Idumu Nguvu ya Umma, iliyotumika kwenye waraka huo ni dhahiri kuwa imetoka CCM kwani wao husalimiana ‘Kidumu Chama cha Mapinduzi’. Mimi nyaraka zangu zote zina saini yangu na hata jina langu huwa naliandika lote kwa kirefu nikitanguliza cheo changu Dr. na si Dk. kama walivyoghushi,” alisema.