Wednesday, June 27, 2012

Wasomali 43 wakutwa wamekufa kwenye lori Dodoma

WATU 43 wenye asili ya Kisomali, wamekutwa wamekufa ndani ya lori wakati wakisafirishwa kutoka Arusha kwenda mkoani Mbeya kupitia Dodoma.
Taarifa za awali zimeeleza kuwa watu hao waliokufa kutokana na kukosa hewa kwa muda mrefu ndani ya lori la mizigo na walibainika wamekufa katika Kijiji cha Chitego wilayani Kongwa mkoani Dodoma umbali wa kilometa mbili kutoka wilayani Kiteto mkoani Manyara.
Gazeti hili lilipata taarifa za vifo hivyo jana kutoka eneo la tukio ambazo zilithibitishwa na mmoja wa viongozi wa Wilaya ya Kongwa ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa kuwa si msemaji.
Mtoa habari huyo alisema dereva wa gari hilo ndiye aliyegundua vifo hivyo baada ya kusikia kelele ya watu na kuamua kusimama na kwenda kufungua lori hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, baada ya dereva wa lori hilo kugundua watu wameshakufa, aliamua kukimbia na kutelekeza gari kwenye eneo la tukio na kuacha maiti na majeruhi.
Alidai maiti hao 43 wamehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kiteto mjini Kibaya na majeruhi zaidi ya 70 wote wanaume, wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi mjini Kiteto kwa mahojiano zaidi huku wengi wao wakiwa katika hali mbaya.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dodoma ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Dk Rehema Nchimbi na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Zelothe Stephen wamekwenda eneo la tukio ili kupata taarifa zaidi.
Hata hivyo, viongozi hao hawakupatikana jana kuthibitisha tukio hilo. Gazeti hili lilimtafuta Msemaji wa Polisi, Advera Senso, ambaye alikiri kusikia taarifa hizo, lakini alisema ameshindwa kumpata Kamanda Zelothe kutokana na shida ya mawasiliano