WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amelieleza
Bunge kuwa, kesho Serikali itatoa msimamo wake kuhusu mgomo wa madaktari
na litakalokuwa na liwe.
Pinda amewaeleza wabunge kwa, jana
Serikali ililazimika tena kwenda tena mahakamani kupinga mgomo huo,
Mahakama imetoa amri ya kuusitisha, hivyo madaktari waheshimu amri ya
Mahakama.
“Tutatoa kauli yetu kesho kwamba
tumeamua nini, Serikali imeamua kuchukua hatua gani…na waswahili
wanasema, litakalokuwa na liwe” amesema Waziri Mkuu wakati anatoa kauli
ya Serikali baada ya Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM)
kuomba mwongozo wa Spika kuhusu mgomo wa madaktari unaoendelea nchini.
Zambi amewaeleza wabunge kuwa madaktari
katika hospitali za rufaa wamegoma ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili
na Hospitali ya Rufaa Mbeya, na kwamba, suala hilo lipo mahakamani
lakini wananchi wanaumia.
Amesema, wabunge hawawezi kujadili suala
hilo kwa kuwa lipo mahakamani, lakini alitaka kufahamu Serikali
imechukua hatua gani za ziada.
Baada ya Waziri Mkuu kutoa msimamo huo,
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika(Chadema) aliomba kutoa taarifa, akasema,
kwa mujibu wa vyombo vya habari, kimeshitakiwa Chama Cha Madaktari
lakini Jumuiya ya madaktari haijashitakiwa.
Mnyika amesema, Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Huduma za Jamii inapaswa kutoa taarifa kuhusu mgomo uliopita wa
madaktari sanjari na kauli ya Serikali kesho ili wabunge wawe na
taarifa kamili kuhusu mgororo kati ya Serikali na madaktari.
“Serikali inakuja na kutupa maelezo yake
hapa bungeni…tusubiri maelezo ya Serikali kesho na kama kuna kipya
tujue kinachoendelea” amesema Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai wakati
anajibu ombi la mwongozo wa Spika la Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge.
Chenge alitaka kufahamu kama ilikuwa
sahihi kwa Mnyika kutoa taarifa bungeni wakati aliyekuwa ameomba
mwongozo kabla, Zambi, alikuwa ameshakaa.
Juni 22, mwaka huu , Bunge lilielezwa
Serikali na madaktari wameshindwa kuafikiana kuhusu madai ya watuhumishi
wa sekta ya afya hivyo Mahakama Kuu Tanzania ndiyo itakayotoa uamuzi
kuhusu mgogoro huo.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk.
Hussein Mwinyi alisema bungeni kuwa, Serikali na madaktari wamekubaliana
kuupeleka mgogoro huo Mahakama Kuu kitengo cha kazi.
Kwa mujibu wa Dk. Mwinyi, suala hilo
sasa lipo chini ya Mahakama kupitia Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA)
hivyo pande hizo zinatakiwa kufuata taratibu.
Amewaeleza wabunge kuwa, Juni 19, 2012,
Serikali na Chama cha Madaktari (MAT) walipeleka CMA taarifa ya mgogoro
huo na hatua zilizokuwa zimefikiwa hadi wakati huo.
“Baada ya msuluhishi kusikiliza maelezo
yao, alitoa maoni yafuatayo: Kuwa mgogoro umekosa suluhu, pande mbili
kwa pamoja wamekubaliana kwamba mgogoro huo umekosa suluhu katika hatua
iliyopo ya usuluhishi, na kuwa wamekubaliana kupeleka mgogoro huo
Mahakama Kuu” amesema.
Ametoa mwito kwa madaktari kote nchini
kuacha mpango wa kuanza mgomo kwa kuwa ni kinyume cha sheria na pia
watakiuka kiapo cha kazi hiyo.
“Hii ni kwa sababu madhara yatokanayo na
mgomo wa madaktari ni makubwa na yanayogharimu maisha ya watu moja kwa
moja tofauti na migomo inayofanywa na kada nyingine za wafanyakazi” Dk.
Mwinyi amesema bungeni mjini Dodoma.
Amewataka madaktari kabla ya kuendelea
na mpango wa kugoma wafikirie kwa kina ili kuepuka madhara
yatakayogharimu maisha ya Watanzania wasio na hatia.
“Hivyo kwa mara nyingine ninawasihi sana
wasichukue hatua ya kugoma, na wawe na subira hadi muafaka
utakapopatikana” alisema. Amelieleza Bunge kuwa, pamoja na ufinyu wa
bajeti, Serikali imekuwa ikiithamini taaluma ya udaktari na imejitahidi
kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya nchini.
“Kutokana na jitihada hizi za Serikali ,
ninawasihi madaktari wote nchini waone kuwa Serikali ina nia njema
katika suala hili na kuwa, wakubaliane na mapendekezo yanayotolewa na
Serikali kwa kuwa bado ina nia ya kuboresha mazingira ya kazi zao na
kuyapatia ufumbuzi madai yao ili kuwepo ufanisi katika utoaji wa huduma
bora za afya kwa wananchi kadri ya uwezo wake” alisema.