WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amelieleza Bunge kuwa, kesho Serikali itatoa msimamo wake kuhusu mgomo wa madaktari na litakalokuwa na liwe.
Pinda amewaeleza wabunge kwa, jana Serikali ililazimika tena kwenda tena mahakamani kupinga mgomo huo, Mahakama imetoa amri ya kuusitisha, hivyo madaktari waheshimu amri ya Mahakama.
“Tutatoa kauli yetu kesho kwamba tumeamua nini, Serikali imeamua kuchukua hatua gani…na waswahili wanasema, litakalokuwa na liwe” amesema Waziri Mkuu wakati anatoa kauli ya Serikali baada ya Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM) kuomba mwongozo wa Spika kuhusu mgomo wa madaktari unaoendelea nchini.
Zambi amewaeleza wabunge kuwa madaktari katika hospitali za rufaa wamegoma ikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Rufaa Mbeya, na kwamba, suala hilo lipo mahakamani lakini wananchi wanaumia.
Amesema, wabunge hawawezi kujadili suala hilo kwa kuwa lipo mahakamani, lakini alitaka kufahamu Serikali imechukua hatua gani za ziada.
Baada ya Waziri Mkuu kutoa msimamo huo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika(Chadema) aliomba kutoa taarifa, akasema, kwa mujibu wa vyombo vya habari, kimeshitakiwa Chama Cha Madaktari lakini Jumuiya ya madaktari haijashitakiwa.
Mnyika amesema, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii inapaswa kutoa taarifa kuhusu mgomo uliopita wa madaktari sanjari na kauli ya Serikali kesho ili wabunge wawe na taarifa kamili kuhusu mgororo kati ya Serikali na madaktari.
“Serikali inakuja na kutupa maelezo yake hapa bungeni…tusubiri maelezo ya Serikali kesho na kama kuna kipya tujue kinachoendelea” amesema Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai wakati anajibu ombi la mwongozo wa Spika la Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge.
Chenge alitaka kufahamu kama ilikuwa sahihi kwa Mnyika kutoa taarifa bungeni wakati aliyekuwa ameomba mwongozo kabla, Zambi, alikuwa ameshakaa.
Juni 22, mwaka huu , Bunge lilielezwa Serikali na madaktari wameshindwa kuafikiana kuhusu madai ya watuhumishi wa sekta ya afya hivyo Mahakama Kuu Tanzania ndiyo itakayotoa uamuzi kuhusu mgogoro huo.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi alisema bungeni kuwa, Serikali na madaktari wamekubaliana kuupeleka mgogoro huo Mahakama Kuu kitengo cha kazi.
Kwa mujibu wa Dk. Mwinyi, suala hilo sasa lipo chini ya Mahakama kupitia Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) hivyo pande hizo zinatakiwa kufuata taratibu.
Amewaeleza wabunge kuwa, Juni 19, 2012, Serikali na Chama cha Madaktari (MAT) walipeleka CMA taarifa ya mgogoro huo na hatua zilizokuwa zimefikiwa hadi wakati huo.
“Baada ya msuluhishi kusikiliza maelezo yao, alitoa maoni yafuatayo: Kuwa mgogoro umekosa suluhu, pande mbili kwa pamoja wamekubaliana kwamba mgogoro huo umekosa suluhu katika hatua iliyopo ya usuluhishi, na kuwa wamekubaliana kupeleka mgogoro huo Mahakama Kuu” amesema.
Ametoa mwito kwa madaktari kote nchini kuacha mpango wa kuanza mgomo kwa kuwa ni kinyume cha sheria na pia watakiuka kiapo cha kazi hiyo.
“Hii ni kwa sababu madhara yatokanayo na mgomo wa madaktari ni makubwa na yanayogharimu maisha ya watu moja kwa moja tofauti na migomo inayofanywa na kada nyingine za wafanyakazi” Dk. Mwinyi amesema bungeni mjini Dodoma.
Amewataka madaktari kabla ya kuendelea na mpango wa kugoma wafikirie kwa kina ili kuepuka madhara yatakayogharimu maisha ya Watanzania wasio na hatia.
“Hivyo kwa mara nyingine ninawasihi sana wasichukue hatua ya kugoma, na wawe na subira hadi muafaka utakapopatikana” alisema. Amelieleza Bunge kuwa, pamoja na ufinyu wa bajeti, Serikali imekuwa ikiithamini taaluma ya udaktari na imejitahidi kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya nchini.
“Kutokana na jitihada hizi za Serikali , ninawasihi madaktari wote nchini waone kuwa Serikali ina nia njema katika suala hili na kuwa, wakubaliane na mapendekezo yanayotolewa na Serikali kwa kuwa bado ina nia ya kuboresha mazingira ya kazi zao na kuyapatia ufumbuzi madai yao ili kuwepo ufanisi katika utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi kadri ya uwezo wake” alisema.