WATU 43 wenye asili ya Kisomali, wamekutwa wamekufa ndani ya lori
wakati wakisafirishwa kutoka Arusha kwenda mkoani Mbeya kupitia Dodoma.
Taarifa za awali zimeeleza kuwa watu hao waliokufa kutokana na kukosa
hewa kwa muda mrefu ndani ya lori la mizigo na walibainika wamekufa
katika Kijiji cha Chitego wilayani Kongwa mkoani Dodoma umbali wa
kilometa mbili kutoka wilayani Kiteto mkoani Manyara.
Gazeti hili lilipata taarifa za vifo hivyo jana kutoka eneo la tukio
ambazo zilithibitishwa na mmoja wa viongozi wa Wilaya ya Kongwa ambaye
hakutaka kutaja jina lake kwa kuwa si msemaji.
Mtoa habari huyo alisema dereva wa gari hilo ndiye aliyegundua vifo
hivyo baada ya kusikia kelele ya watu na kuamua kusimama na kwenda
kufungua lori hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, baada ya dereva wa lori hilo kugundua
watu wameshakufa, aliamua kukimbia na kutelekeza gari kwenye eneo la
tukio na kuacha maiti na majeruhi.
Alidai maiti hao 43 wamehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya
Kiteto mjini Kibaya na majeruhi zaidi ya 70 wote wanaume, wanashikiliwa
katika Kituo cha Polisi mjini Kiteto kwa mahojiano zaidi huku wengi wao
wakiwa katika hali mbaya.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dodoma ikiongozwa na Mkuu wa
Mkoa, Dk Rehema Nchimbi na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Zelothe Stephen
wamekwenda eneo la tukio ili kupata taarifa zaidi.
Hata hivyo, viongozi hao hawakupatikana jana kuthibitisha tukio hilo.
Gazeti hili lilimtafuta Msemaji wa Polisi, Advera Senso, ambaye alikiri
kusikia taarifa hizo, lakini alisema ameshindwa kumpata Kamanda Zelothe
kutokana na shida ya mawasiliano