• Mwenyewe asema wananchi wa Monduli ndiyo msuli wake
SIKU chache baada ya Waziri Mkuu mstaafu, Fredereck Sumaye, kubwagwa kwenye kinyang’anyiro cha ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Hanang’ mkoani Arusha mwanasiasa huyo sasa ametangaza vita na Waziri Mkuu mwenzake mstaafu, Edward Lowassa.Sumaye ambaye hajatangaza rasmi kuwania kiti hicho, anatarajiwa kupasua jibu wakati wowote kuanzia leo kueleza kilichotokea; msimamo wake na kwamba yuko tayari kuwania urais mwaka 2015 endapo Lowassa atawania kiti hicho.
Sumaye aliangushwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, katika kuwania nafasi ya ujumbe wa NEC wilaya ya Hanang, matokeo ambayo anaamini yana mkono wa Lowassa.
Chanzo cha karibu na Sumaye, kilisema kuwa pamoja na Waziri Mkuu huyo mstaafu kushindwa na Dk. Nagu kwa zaidi ya kura 167, amepokea matokeo hayo kwa shingo upande kwa kile alichoeleza kuwa ushindi huo ni wa mafisadi.
“Hataki kuzungumza chochote leo ila atazungumza nanyi wakati wowote kuanzia leo, lakini anasema ikiwa Lowassa atawania urais, Sumaye ataingia katika mpambano huo kukabiliana naye kwa njia yoyote. Hataki kusema ataingia kwa CCM au chama gani au mgombea binafsi,” anaeleza mtu wa karibu na Sumaye.
Vyanzo vilivyo karibu na mwanasiasa huyo vimeeleza kuwa tayari Sumaye amefanya mazungumzo na baadhi ya wanasiasa wenye ushawishi wanaojipambanua kama wapiganaji wa ufisadi ili kuunganisha nguvu kwa ajili ya kukabiliana na kambi ya Lowassa.
Mbali ya kundi la Sumaye na wanasiasa wengine kuanza mkakati huo, wapo pia wanasiasa wengine wenye majina makubwa ndani ya chama, serikali na wastaafu wanaotajwa kuingia kwenye muungano huo.
Akijibu tuhuma hizo kwa kifupi, Lowassa alisema endapo Sumaye ataitisha mkutano na waandishi wa habari na kutoa tuhuma hizo, nitajibu.
Hata hivyo, baadhi ya wafuasi wa Sumaye na watendaji wa ndani ya serikali wamesema kuanguka kwa mwanasiasa huyo mkongwe katika uchaguzi wa wilaya kunamuweka vizuri zaidi kisiasa kutokana na mazingira tete ya kisiasa ndani ya CCM, chama ambacho kimechokwa na umma.
Waziri wa zamani wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora) na mbunge wa zamani wa jimbo la Makete, Dk. Hassy Kitine, alikaririwa juzi akisema kuwa kuangushwa kwa Sumaye katika nafasi ya NEC hakuwezi kumuathiri kisiasa kama atachukua uamuzi wa kuwania urais mwaka 2015 kupitia CCM.
Dk. Kitine alitoa kauli hiyo alipoombwa na gazeti moja kutoa maoni yake juu ya matokeo ya NEC wilayani Hanang’ kama yana athari kwa mustakabali wa kisiasa kwa kiongozi huyo.
“Katiba ya CCM haina kipengele kinachosema kama unataka kuwania urais ni lazima uwe mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM , kwa hiyo nasema kama kweli Sumaye anatafuta urais bado ana nafasi ya kuwania nafasi hiyo,” alikaririwa akisema Dk. Kitine.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, naye alimtia moyo Sumaye kwa kuweka bayana kuwa uchaguzi wa NEC ni wa ngazi ya wilaya tu kwa hiyo Sumaye anaweza kuwa anakubalika kitaifa kuliko katika wilaya anayotoka huku akitumia usemi kwamba ‘nabii hakubaliki kwao’.
Katika hatua nyingine, hali inaelezwa kuwa tete ndani ya CCM baada ya kuwapo kwa taarifa za ushangiliaji kutoka kwa wafuasi na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambao wameona wanazidi kusafishiwa njia.
“CHADEMA wameshangilia sana kwa kuwa sasa jimbo hilo litachukuliwa kirahisi. Walikuwa wanamuogopa Sumaye na kumheshimu hivyo kwa sasa watu wake wote wanahamia CHADEMA.
“Wanasema mafisadi walihakikisha wanampa kila mjumbe kiwango cha chini kabisa cha shilingi 100,000 kumuangusha Sumaye. Uongozi wote wa CCM wa wilaya na hata baadhi kwenye mkoa walijipanga kumuangusha,” anasema.
Katika uchaguzi huo wa Hanang, hali ilianza kuwa tete toka hatua za awali, ambapo Dk. Nagu alitajwa kushinikiza kubadilishwa kwa muhtasari wa kikao cha wilaya kilichokata jina lake na hivyo kurudishwa tena.
Taarifa kutoka Hanang zinaeleza kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ilifanya kazi katika mazingira ya aibu kutokana na kuonekana kufumbia macho vitendo vya rushwa iliyogawiwa waziwazi.
Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah, alinukuliwa akisema kwamba taasisi yake inafuatilia kwa karibu uchaguzi huo ndani ya CCM ili kubaini watu wanaotumia rushwa, kauli ambayo imeelezwa kuwa ya kisiasa zaidi.
Dk. Hoseah alitoa kauli hiyo akijibu hoja mbalimbali za washiriki wa kongamano la kujadili utekelezaji wa awamu ya pili ya mpango wa kupambana na rushwa nchini na mapendekezo yanayopaswa kuzingatiwa katika utekelezaji wa mpango wa awamu ya tatu (2012 – 2016).
Uchaguzi huo ulifanyika siku chache baada ya CCM kupitisha majina ya walioomba nafasi hizo huku wanachama wengi wakienguliwa kutokana na kukosa sifa katika kikao kilichomalizika mjini Dodoma mapema wiki hii.
Katika hatua nyingine, Lowassa ametamba kuwa wananchi wa Monduli ndiyo msuli wake wa kisiasa.
Akizungumza baada ya ushindi wa NEC alioupata, Lowassa alisema ushindi huo mkubwa umedhihirisha kuwa ana misuli ya kisiasa kwa wananchi wake.
“Kuna mzee rafiki yangu aliniambia kuwa katika kazi za siasa angalia ‘grass roots’, watu wanakuwa ndiyo msuli wako kisiasa, na mimi watu wa Monduli ndiyo msuli wangu,” alisema Lowassa ambaye anatajwa kuwa mmoja wa watu watakaowania urais mwaka 2015.
“Wananchi wa Monduli mmenithibitishia hilo na nawashukuru sana kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu, jibu la thibitisho hilo kwangu ni utumishi uliotukuka kwenu,” aliongeza.
Lowassa alipata asilimia 93 ya kura dhidi ya wapinzani wake, Dk. Sulesh Toure aliyetangaza kujitoa baada ya kuona upepo mbaya kwake na Nanai Konina.