Friday, October 5, 2012

Mjane wa Mwangosi alilia rambirambi za Slaa

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa

UTAMADUNI mpya wa siasa za misibani, unaoendana na mauaji yaliyotokana na ukaidi wa wanasiasa kwa Jeshi la Polisi, umeanza kuiumbua Chadema ambayo imejikuta ikishindwa kutimiza ahadi ndogo ndogo za kutoa rambirambi inazoahidi kwa wafiwa.

Juzi, mjane wa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, Aneti, alijikuta akiomba wanahabari wasaidie kufuatilia rambirambi iliyoahidiwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kutokana na kiongozi huyo, kukata mawasiliano baada ya msiba.

“Nina mawasiliano na Profesa Mark Mwandosya ambaye pia aliahidi kumsomesha mtoto mmoja, yeye aliniambia nitakapokuwa tayari nimjulishe ili atume fedha kwenye akaunti ya shule, lakini sina mawasiliano na Dk Slaa,” alisema Aneti.

Mwangosi aliuawa Septemba 2 mwaka huu, kwa kupigwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni bomu katika Kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi mkoani Iringa.

Aliuawa wakati Polisi ikizuia wafuasi na viongozi wa Chadema kufanya mikutano ya hadhara ambayo ilipigwa marufuku ili kuruhusu shughuli ya Sensa ya Watu na Makazi, kufanyika bila kuingiliwa.

Baada ya mauaji hayo, wakati wa maziko ya mwandishi huyo, Dk Slaa aliahidi kubeba jukumu la kusomesha mtoto wa kwanza wa Mwangosi aitwaye Nehemiah, ambaye yuko kidato cha nne katika Sekondari ya Malangali, Mufindi, Iringa.

“Mtoto huyu alifika na kutaka kujua sababu za kifo cha baba yake, kwa uchungu huku machozi yakimtoka, nimewasiliana na mdau wangu na kuahidi kubeba jukumu la kumsomesha na pia naahidi kufuatilia ahadi hiyo kwa kipindi chote cha masomo yake,” alinukuliwa Dk Slaa akiahidi.

Hata hivyo ahadi hiyo, mbali na ukweli kuwa haijatekelezwa, lakini pia hata mawasiliano kati yake na mjane wa Mwangosi hayapo mpaka mjane huyo kuamua kuomba waandishi wamfuatilie.

Mwingine aliyeahidi kusaidia familia hiyo ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais asiye na Wizara Maalumu, Profesa Mwandosya, ambaye aliiwakilisha Serikali na katika salamu zake za rambimbambi msibani, alisema atabeba jukumu la kusomesha watoto wengine wa marehemu huyo.

Aliahidi pia kufuatilia ahadi za watu wengine katika kuisaidia familia ya Mwangosi kwa kuwa ni ndugu yake na jirani. “Nitahakikisha familia hii inaishi maisha kama ambavyo angelikuwapo baba yao kwa kuhakikisha kila mtoto wa familia hiyo anasoma kwa kila hatua kwa kuzingatia kuwa hao ni sehemu ya familia yangu,” alisema Mwandosya, ambaye pia ni Mbunge wa Rungwe Mashariki (CCM).

Alipopigiwa Dk Slaa simu kujua mipango yake ya kutekeleza ahadi hiyo, simu yake ilikuwa inaita mara zote bila kupokewa.

Rambirambi zingine Wakati huo huo, wafanyakazi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoani Iringa, wametoa rambirambi zao kwa mjane huyo. Mhasibu Mkuu wa Tanroads Iringa, Alex Mgeta alikabidhi Sh 265,000 juzi katika nyumba yao iliyopo Kihesa Bwawani mjini hapa.

“Nashukuru sana lakini pia nawaomba kwa kupitia michango ambayo nimeambiwa inaendelea kukusanywa mnisaidie nimalizie nyumba hii,” alisema Aneti.

Aneti alisema nyumba hiyo yenye vyumba vinne vya kulala haijakamilika na ikikamilika, atapangisha baadhi ili kiasi cha fedha atakachopata kitumike kuendesha familia yake.

Septemba 30 katika harambee iliyofanyika Iringa kwa mujibu wa blogu ya Mjengwa, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Kabwe Zitto alijitolea kumchangia mjane huyo kwa kumlipia ada ya uanachama wa Bima ya Afya kila mwezi kwa miaka mitatu mfululizo.

Alikaririwa akisema: "Nimeona nami niunge mkono harambee hii. Pamoja na michango ya fedha iliyotolewa kumsaidia mjane kuanzisha mradi wa kujikimu, naona ni muhimu akawa na uhakika wa huduma ya afya yake na watoto wake wanne.

Hivyo, mchango wangu utakuwa ni kwenye eneo hilo la Bima ya Afya kwa miaka mitatu.

"Baadhi ya watu wengine maarufu waliojitokeza kumchangia mjane kupitia mtandao wa kijamii wa Mjengwablog.com ni pamoja na Shy-Rose Bhanji, Ananilea Nkya, John Bukuku na Mobhare Matinyi aliyepata kuwa Mhariri wa Majira.