Wednesday, September 12, 2012

‘Walimu wanaopewa mimba na wanafunzi washitakiwe’



BAADHI ya wanafunzi wa sekondari wilayani Mpanda na Mlele mkoani Katavi wamejitokeza mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kupendekeza Katiba ijayo ibane walimu wa kike ambao wanapewa ujauzito na wanafunzi wao.

Pia wanafunzi hao walipendekeza wanafunzi wanapopeana mimba, mvulana na msichana, wote wachukuliwe hatua za kisheria kwa kushitakiwa na si msichana kufukuzwa shule tu wakati mvulana anashitakiwa na baadaye kufungwa.

Wanafunzi hao pia walipendekeza mabadiliko ya mitaala ili kumpunguzia masomo mwanafunzi wa sekondari na wakapendekeza lugha ya Kiswahili iwe ya kufundishia kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne.

Sabath Katabi ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne katika Sekondari ya Kasokola wilayani Mulele, alisema maisha ya shule yana wanafunzi na walimu na mwalimu wa kiume anapompa mimba mwanafunzi wake, anafukuzwa shule na kushitakiwa.

“Naomba Katiba mpya pia iseme kuwa mwalimu wa kike anayepewa mimba na mwanafunzi wake pia afukuzwe kazi na ashitakiwe, kwani naye atakuwa amefanya kosa kufanya mapenzi na mwanafunzi wake,” alisema Katabi.

Mwanafunzi huyo alisema hajawahi kuona walimu wa kike wanaofanya mapenzi na wanafunzi wao wakichuliwa hatua, jambo ambalo alisema ni ubaguzi mkubwa wa kisheria kwa kuwaonea walimu wanaume ambao wanajikuta kwenye uhusiano na wanafunzi wao, kwa sababu ya kujaribiwa na wanafunzi hao.

Mikisedeki Nyambwago ambaye ni mwanafunzi wa Sekondari ya Milala alitaka wanafunzi wa kike ambao wanapachikwa mimba na wanafunzi wavulana nao wachukuliwe hatua za kisheria, kwa kushitakiwa ili wawe waoga wa kufanya mapenzi wakiwa shuleni.

“Sheria inabagua, mvulana akifanya mapenzi na msichana, mvulana anafukuzwa shule na kushitakiwa, lakini msichana anafukuzwa shule na hashitakiwi, kwa nini wakati wote hawa wamefanya kosa la jinai?”

Alihoji mwanafunzi huyo. Nasri Lubeba mwanafunzi wa kidato cha tatu wa Sekondari Milala, alipendekeza Katiba itamke kuwa mwanafunzi wa kike anayepata ujauzito, akishajifungua apewe fursa ya kurudi shuleni ili aendelee na masomo.

Alipoulizwa na Dk Sengondo Mvungi kama haoni kuwa hiyo itachochea wanafunzi wengi kupata ujauzito, Nasri alisema haiwezekani, kwani ujauzito unatokea kwa bahati mbaya na hakuna mwanafunzi anayedhamiria kupata ujauzito akiwa shuleni.

“Ile inatokea kwa bahati mbaya, sidhani kama kuwapo kwa sheria hiyo kutachochea ngono shuleni, ila kutampunguzia mzigo msichana, kwani maisha yake asiporudi shule yanakuwa mabaya zaidi,” alisema msichana huyo.

Pia alipendekeza wanafunzi wanapopeana mimba iangaliwe adhabu ambayo haitawakandamiza au kuumiza kichanga kinachozaliwa, bali itafutwe namna ya kuwasaidia ili waendesha maisha yao ya baadaye. Kwa upande wake, Marko Bwire alipendekeza Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia hadi kidato cha nne kwa maelezo kuwa wanafunzi wengi wanafeli mitihani ya kidato cha nne kutokana na kutoielewa vizuri lugha wanayofundishiwa.

“Unakuta mwanafunzi shule ya msingi alikuwa anafanya vizuri, akienda sekondari kwa vile huko masomo yote yanafundishwa kwa Kiingereza, lugha inakuwa kikwazo na kusababisha afeli,” alisema Bwire.

Flora Kashindye wa kidato cha pili Shule ya Milala, alipendekeza Katiba iilazimishe Serikali kujenga maabara kwenye sekondari za kata, ili kupunguza idadi ya wanafunzi wanaofeli.

Alisema wanafunzi wanaosoma shule za kata hawafanyi mitihani ya vitendo, bali wanafanya ya nadharia tu hali inayosababisha washindwe kuhimili ushindani na shule zingine.

Mwanafunzi mwingine, Peter Kalindi yeye alitaka mitaala iboreshwe na isibadilishwe mara kwa mara, kwani kufanya hivyo kumechangia kuvuruga elimu nchini, wakati Basori Masunga akipendekeza Serikali iweke viwango vya ada kwa shule binafsi ili hata wazazi wenye kipato kidogo wasomeshe watoto wao.