Wednesday, September 12, 2012
Waandishi wa habari waandamana kulaani mauaji ya mwenzao
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi amepongeza waandishi wa habari walioandama jana Dar es Salaam kwa kuzingatia sheria.
Dk Nchimbi ambaye ‘alivamia’ Viwanja vya Jangwani jana ambako maandamano hayo ya kulaani mauaji ya mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi yaliishia, alisema waandishi hao walifuata utaratibu.
“Hivi ndivyo inavyotakiwa, kufuata sheria, kwani walitoa taarifa Polisi lakini hata walipoambiwa kwamba Mnazi Mmoja njia ni nyembamba hivyo wahamie Jangwani hawakusita na walifanya hivyo.
“Ni tofauti na watu wengine ambao wakiambiwa msipite huku hali hairuhusu hulazimisha na matokeo yake ni mtafaruku na Jeshi la Polisi,” alisema Nchimbi alipozungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Jangwani. Alitoa mwito kwa makamanda wa Polisi wa mikoa kukaa na wanahabari na kujadiliana ili wafanye kazi pamoja na kuondokana na migogoro ambayo haina ulazima.
Waziri Nchimbi ambaye alipata kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, alisema yote yaliyozungumzwa na wanahabari jana Jangwani kwa Serikali yatafanyiwa kazi bila kusita.
Wahariri na waandishi wa habari wakiwamo waliopata kufanya kazi katika vyombo vya habari, waliandamana kimyakimya kulaani mauaji ya Mwangosi yaliyotokea Iringa katika maandamano ya Chadema, siku 10 zilizopita.
Mwangosi ni mwandishi wa kwanza nchini kuuawa akiwa kazini na wa 38 mwaka huu na kufikisha idadi ya waandishi 46 waliouawa wakiwa kazini duniani kote.
Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida, Waziri Nchimbi ambaye awali alilakiwa na uongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na kupanda jukwaani alijikuta akizomewa na kutakiwa kuondoka eneo hilo.
Awali akiwa peke yake, baada ya kuegesha gari mbali na eneo la mkutano, Nchimbi alitembea hadi walikokuwa wanahabari hao na kupokewa kabla ya kukumbana na kadhia hiyo.
Waandishi wa habari walipoulizwa ni wangapi wanataka Waziri ahutubie, walikataa na kumtaka aondoke huku wakihoji alichofuata.
Lakini tofauti na Nchimbi, aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayeaminika kuwa kada na mwumini wa Chadema, Dk Azaveri Lwaitama, bila kualikwa alipewa fursa ya kuhutubia mkutano huo.
Maandamano hayo yalianzia Channel Ten na kuishia Jangwani huku washiriki wakiwa na mabango ya kulaani mauaji hayo na wengine wakiwa na mfano wa silaha na baadhi yao wanaoaminika ni waandishi wa Kampuni ya HaliHalisi inayochapisha magazeti ya MwanaHalisi (lililofungiwa) na Mseto, walionekana na mabango yakilaani kufungiwa kwa gazeti hilo.
Akizungumza katika Viwanja vya Jangwani, Katibu Mkuu wa TEF, Neville Meena alisema mauaji ya Mwangosi yanaonesha kuwa mazingira ya kufanyia kazi kwa wanahabari si salama.
Alisema wahariri na waandishi wa habari walikuwa na uwezo wa kufanya jambo kubwa kupitia kalamu na kamera zao zaidi ya maandamano, lakini waliamua kutumia njia ambayo wananchi wa kawaida wanaitumia kudai haki zao.
Alisema TEF ilianza kwa kutoa tamko la kulaani na kuunda tume ya watu watatu ambayo itafanya utafiti wa kihabari kuhusu tukio hilo, utakaotumika kupata maazimio ya wadau wa habari.
Tume hiyo imeundwa na mjumbe kutoka TEF, Baraza la Habari Tanzania (MCT) na kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini. Meena alitaka waandishi wa habari kuendelea kuhabarisha wananchi kwa kufuata misingi ya taaluma ya habari.
“Tuendelee kufanya kazi, bila vyombo vya habari hakuna kitu kitakachoendelea na ndiyo maana hata Rais akitaka kuhutubia wananchi kila mwezi haendi Jangwani bali anatumia vyombo vya habari kufikia Watanzania zaidi ya milioni 40.”
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari (UTPC), Jane Mihanji pamoja na kulaani mauaji hayo kwa nguvu zote, alitaka Polisi kutambua kuwa mwandishi anapokuwa kazini anatakiwa kuheshimiwa kwa kazi yake kama inavyofanywa kwa polisi akiwa kwenye sare. Mhariri Mtendaji wa Nipashe, Jesse Kwayu alisema:
“Kama Mwangosi angekufa kwa njia nyingine, kingekuwa kifo cha Mungu, lakini kwa kuwa ameuawa kikatili ndiyo maana tuko hapa.
“Damu yake ndiyo mwanzo wa kubadilisha mwenendo wa Jeshi la Polisi nchini, wajue kuwa kodi za wananchi kama sisi ndizo zinazolipa mishahara, kuwanunulia magwanda kwa kazi ya kulinda raia na si kuua.”
Dk Lwaitama aliyetambulishwa kama rafiki wa wanahabari, alitaka waandishi kutochukia polisi wa ngazi ya chini na badala yake wachukie wanasiasa wanaowatuma na kuwatumbukiza katika siasa. Mwakilishi wa Africa Media Group, Dina Chahali alishukuru wanahabari kwa umoja wao wa kulaani mauaji ya Mwangosi na kuwa huo ndio mwanzo wa kudai haki ya habari na wanahabari.
Meena alipoulizwa baadaye na gazeti hili iweje Dk Nchimbi azuiwe kushiriki na Dk Lwaitama aruhusiwe, alisema hakuna aliyealikwa kwenye maandamano hayo zaidi ya waandishi wa habari na Dk Lwaitama alikuja kama wananchi wengine walivyojitokeza.
“Dk Lwaitama hakupata mwaliko, ila penye watu wengi panakuwa na mengi kama unavyojua ... sisi wenyewe tunashangaa, ni kupitiwa tu ila naye hakupewa mwaliko,” alisema bila kufafanua kama wananchi wengine nao walikuwa na haki ya kupanda jukwaani kuhutubia wanahabari.
Arusha Mkoani Arusha, polisi walifika eneo la Jengo la CCM la Mkoa, kuzuia maandamano ya waandishi waliokuwa wamejikusanya wakiwa na mabango yao, yenye ujumbe mbalimbali wa kulaani mauaji ya Mwangosi.
Polisi walieleza kuwa wanakabiliwa na uhaba wa askari wa kulinda maandamano hayo, kwa sababu ya ugeni mkubwa wa Mkutano wa Mazingira. Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), Eliya Mbonea aliwaomba waandishi kutii amri ya Polisi, huku akiwasomea taarifa ya Jeshi hilo iliyotolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha (OCD), Lotson Mponjoli ya kuzuia maandamano hayo.