Friday, August 31, 2012

Hawa Ngulume afariki dunia



ALIYEKUWA Mkuu wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Hawa Ngulume amefariki dunia jana asubuhi katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam, kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya mapafu kwa muda mrefu.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, alithibitisha kutokea kwa msiba huo, na kufafanua kuwa msiba uko nyumbani kwa marehemu Goba jijini Dar es Salaam.

“Ni kweli tumepokea kwa masikitiko taarifa ya msiba wa Mheshimiwa Ngulume, ila bado hatujajua sababu ya kifo hicho, tunasubiri taarifa ya madaktari wa Lugalo ambako alilazwa kwa muda wa wiki nzima,” alisema DC Rugimbana.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Msemaji wa familia hiyo, Alhaji Mwenza, Ngulume alifariki jana saa 4.25 asubuhi ambako alikuwa akitibiwa ugonjwa wa saratani ya mapafu.

Alisema kwa mujibu wa taarifa za awali alizokuwa nazo marehemu, ilikuwa azikwe leo saa saba mara baada ya sala ya Ijumaa nyumbani kwake Goba, lakini baadaye ratiba ilibadilika na leo anatarajiwa kusafirishwa kijijini kwao Kintiko mkoani Singida.

“Kwa mujibu wa watoto wake, kesho (leo) atasafirishwa kupelekwa Singida katika Tarafa ya Kintiko ambako anatarajiwa kuzikwa keshokutwa (kesho) kama mambo yote yataenda sawa,” alisema Mwenza.

Ngulume wakati wa uhai wake aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwamo ukuu wa wilaya katika wilaya za Kinondoni, Singida, Bagamoyo na Mbarali alikostaafu wadhifa huo Mei mwaka huu.

Ameacha watoto wawili na wajukuu watano. Katika hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Ngulume.

Alisema jana kuwa Ngulume, enzi za uhai wake, alikuwa kiongozi shupavu aliyesimamia uamuzi wake katika majukumu muhimu ya kitaifa kwa lengo la kuletea wananchi maendeleo sehemu zote alizotumikia.

“Nilimfahamu marehemu, enzi za uhai wake, akiwa kiongozi mwanamke shupavu aliyesimamia kikamilifu uamuzi wake na hivyo kuthibitisha ukweli, kwamba wanawake wakipewa fursa wanaweza,” alisema Rais Kikwete.

“Kutokana na msiba huo mkubwa, natuma salamu za rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa familia ya marehemu, Hawa Ngulume kwa kuondokewa na mhimili muhimu na kiongozi wa familia.

“Natambua machungu mliyonayo hivi sasa kwa kumpoteza mama wa familia, lakini nawahakikishieni kuwa niko pamoja nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa,” aliongeza Rais Kikwete.