NI takriban wiki ya tatu sasa tangu Bunge la 10 katika mkutano wake wa nane uanze kwa kuwasilishwa Bajeti ya Serikali na makadirio ya matumizi ya wizara mbalimbali ikiwamo Ofisi ya Rais inayoshughulikia Utumishi wa Umma.
Tangu kuanza kwa mkutano huo wa Bunge hali imekuwa si shwari katika mijadala kutokana na kutawaliwa zaidi na jazba, kashfa, matusi na lugha chafu hali iliyosababisha wabunge wawili kutolewa nje ya vikao vya Bunge hilo kwa utovu wa nidhamu.Lugha hizo zisizo za kuridhisha zilianza katika uchangiaji wa wabunge hao katika mjadala wa Bajeti ambapo walifikia hatua ya kuzomeana na hata kutoa lugha za kuudhi dhidi ya Rais Jakaya Kikwete.
Pamoja na hali hiyo kukemewa na kuwa gumzo kwa wananchi, bado tabia hiyo ya wabunge kutozingatia Kanuni za Bunge inazidi kujidhihirisha kadri vikao vya Bunge hilo vinavyoendelea.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, wakati wakichangia Bajeti ya Wizara ya Utumishi wa Umma, hali ilikuwa mbaya bungeni humo na kuonesha kuwa iko haja kwa wabunge hawa kujipanga na kujenga hoja zao kwa kuzingatia zaidi maslahi ya nchi bila kutanguliza matusi na kashfa wao wenyewe kwa wenyewe.
Katika uchangiaji wa baadhi ya wabunge ziliibuka hoja za maana hasa suala la mgomo wa madaktari, huku hoja kuu ikiwa chanzo cha mgomo huo na kipigo cha Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka.
Hata hivyo, katika mjadala huo ambao Watanzania walikuwa wakiutarajia, kuibuliwa na wawakilishi hao wa wananchi na kupata msimamo wa wabunge kuhusu hali mbaya za wagonjwa kutokana na mgomo wa madaktari, hali ilibadilika na ukumbi huo kugeuka eneo la malumbano na vijembe.
Wabunge hao wakaishia kunyoosheana vidole, kutuhumiana na hata kukashifiana hali ambayo kwa hali ilivyo sasa ya Watanzania katika sekta ya afya, haikutarajiwa kufanywa na waheshimiwa hao wanaowakilisha wananchi.
Hakuna asiyejua madhara ya mgomo wa madaktari ambao kwa sasa ingawa unaelekea kupungua, lakini ulitikisa wananchi wengi kutokana na ukweli kuwa huduma zilidorora na ingawa bado hakuna takwimu halisi, wapo waliopoteza maisha kutokana na janga hili.
Hivyo kutokana na ukweli huo, ni vigumu kuamini kilichotokea juzi ambapo wabunge waliishia kujibizana bila kujali Kanuni za Bunge na kufukuzana, huku mwafaka wa kile kinachotokea nchini huku afya ya Watanzania wagonjwa ikiwekwa rehani.
Majibizano ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mwenyekiti wa Bunge hilo Sylvester Mabumba hayakupendeza machoni na masikioni mwa Watanzania hata kidogo na hata kauli za Mbunge wa Iramba Magharibi Mwigulu Mchemba na wa Ubungo, John Mnyika hazikupendeza.
Na ili kuonesha hali hiyo ya matumizi yasiyo mazuri ya lugha, jana asubuhi baada ya kipindi cha maswali hali ilibadilika bungeni kwa miongozo, ambapo wabunge walilalamikia kutukanwa huku Mnyika akiomba hatua zichukuliwe dhidi ya aliyedai kuwa anawashwa.
Ukweli ni kwamba matendo haya yanasikitisha na kuzua maswali kwa wananchi kuhusu wajibu hasa wa wabunge hawa, je ni kutunishiana misuli na kutupiana kashfa au kutetea maslahi ya wananchi waliowatuma ndani ya jengo hilo la Bunge?
Ni vyema wabunge wakatambua wajibu wao na kuhakikisha masuala muhimu kama mgomo wa madaktari na maisha halisi ya Watanzania yanawasilishwa katika chombo hicho na kujadiliwa bila kuingiza itikadi wala malumbano yasiyo na tija.