VIONGOZI na wafanyabiashara nchini, wameelezwa kutorosha na kuhifadhi fedha nje ya nchi kiasi cha Sh trilioni 16.6 fedha ambazo zinazidi bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/13.
Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM) alisema hayo bungeni jana wakati akichangia hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Tume ya Mipango kwa mwaka 2012/13 na kuituhumu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuwa inajua fedha zote zilizofichwa na Watanzania nje ya nchi.
Mpina mbali na kuituhumu BoT kufahamu fedha hizo zilipo, alisema Benki Kuu ya Uswisi imekiri sehemu ya fedha hizo kuhifadhiwa katika benki za nchi hiyo na Watanzania sita.
“Taasisi ya Global Financial ilibainisha kuwa Sh trilioni 16.6 zimefichwa nje ya nchi na viongozi na wafanyabiashara wa nchini na Benki Kuu ya Uswisi imesema Sh bilioni 315 ziko nchini mwao zimefichwa na watu sita.
“Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inajua fedha za Watanzania zilizo nje ya nchi, lakini hadi leo hawajatwambia ni za nani, ziliibwa lini na zitarejeshwa lini! Mbali na kufichwa kwa fedha hizo, Mpina alisema pia kwamba Tanzania inapoteza Sh bilioni 478 kila mwaka, zaidi ya nusu ya Bajeti ya Zanzibar kutokana na fedha hizo kufichwa katika benki za nje ya nchi.
Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM), akichangia hotuba hiyo, alishauri uundwe Mfuko wa Dharura wa kulipa madai ya watumishi ikiwamo malimbikizo ya mishahara yao ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara.
Mbunge wa Lushoto, Henry Shekifu (CCM), aliitaka Serikali itangaze nyongeza ya mshahara mapema kama ilivyokuwa zamani ili watumishi wajipange na si kama inavyofanya sasa kuwa siri.
Mbunge wa Korogwe Mjini, Yusuf Nassir (CCM) alisema katika leseni 28 zilizotolewa na Serikali za utafutaji gesi, hakuna Mtanzania anayefanya kazi hata katika ngazi za chini na taarifa ya mwekezaji ndiyo inapewa Serikali kitendo ambacho si sahihi.