MADAKTARI wameanza kurejea polepole katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuhudumia wagonjwa wanaofika hapo na waliolazwa.
Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Aminiel
Aligaesha alisema jana kuwa kurugenzi za hospitali hiyo, zilifanya kazi
kwa kiwango cha kati kutokana na kuwapo wagonjwa wachache.
Kwa mujibu wa Aligaesha taarifa za utendaji kazi zilipatikana baada
ya tathmini katika kurugenzi za Tiba, Upasuaji, Tiba Shirikishi na
Uuguzi.
Kuhusu Kurugenzi ya Tiba, alisema huduma ziliendelea kutolewa kwa
kiwango cha kati kwa kuwa wagonjwa ni wachache wakati katika Idara ya
Tiba madaktari bingwa wote na wasajili wote walifika na kufanya kazi.
“Madaktari walio katika mafunzo kwa vitendo (interns) 11 walifanya
kazi, wodi muhimu zilihudumiwa na kliniki zote za jana ziliendelea
kufanya kazi na kliniki za mchana zilifanyika,” alisema Aligaesha.
Katika Idara ya Watoto, Aligaesha alisema madaktari bingwa wote
walikuwapo na walifanya kazi ingawa walikuwa na changamoto ya kufanya
kazi pia katika kliniki za wagonjwa wa nje.
Alisema katika Idara ya Magonjwa ya Nje, wahudumu wa usajili na
madaktari bingwa walikuwapo wote na walifanya kazi pamoja na Idara ya
Magonjwa ya Afya ya Akili kwani wagonjwa wote walikuwa wodini na
walionwa na madaktari.
Alisema katika Idara ya Magonjwa ya Dharura, wasajili wote walisaini
lakini waliofanya kazi ni wawili na daktari bingwa alikuwapo na Idara ya
Mazoezi ya Viungo pia wafanyakazi wote walihudhuria na walifanya kazi.
Katika Kurugenzi ya Upasuaji, alisema huduma za upasuaji zilifanyika
lakini si sawa na jinsi ilivyokuwa kabla ya mgomo, kwani wagonjwa ni
wachache katika baadhi ya kliniki na kliniki zingine wagonjwa walikuwa
wengi.
Aligaesha alisema wagonjwa wa upasuaji waliokuwa wodini walihudumiwa
ingawa ni wachache ikilinganishwa na hali ilivyokuwa wakati wa mgomo na
baadhi ya huduma za upasuaji zilifanyika ingawa wagonjwa ni wachache.
Kuhusu huduma za tiba shirikishi, alisema vipimo vya maabara na vya
uchunguzi wa radiolojia viliendelea kufanyika kama kawaida ingawa idadi
ilipungua ikilinganishwa na kabla ya mgomo. Alisema Idara ya Famasia pia
ilifanya kazi kama kawaida.
Madaktari wa Vitendo watimuliwa
Wakati madaktari wakirejea kazini taratibu na kuhudumia Watanzania,
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ilidaiwa jana kufukuza madaktari walio
katika mafunzo kwa vitendo.
Msemaji wa madaktari hao, Frank Kagoro alidai jana kuwa madaktari hao
walipewa barua za kufukuzwa, lakini walizikusanya na kuzirejesha kwa
Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Alisema waliutaka uongozi wa Muhimbili kuzipeleka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kuwa wao wako chini ya Wizara.
Hata hivyo, Aligaesha alipohojiwa kuhusu kufukuzwa kwa madaktari hao,
alisema hawezi kulizungumzia na kusisitiza kuwa halipo katika taarifa
hiyo.
Waitwa wizarani
Wakati madaktari hao wakitaka Muhimbili iwarudishe serikalini, Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii imewaagiza madaktari hao waripoti wizarani
kabla ya keshokutwa.
Msemaji wa Wizara hiyo, Nsachris Mwamwaja alisema madaktari hao wote
nchi nzima, wanatakiwa kufika wizarani siku hiyo ili kuelezwa taratibu
zingine.
Hospitali nyingine Huduma katika Hospitali ya Amana iliendelea kutolewa huku wagonjwa wakifika kwa wingi hospitalini hapo.
Amina Abdallah, mkazi wa Tabata alisema alifika hospitalini hapo
kumpeleka baba yake lakini hali haikuwa mbaya alipokewa Mapokezi na
madaktari walikuwapo wakihudumia.
Dk Mwinyi akazia Naye Veronica Mheta anaripoti kutoka Arusha kwamba,
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi alisema msimamo wa
Serikali uko pale pale kwa madaktari kuwa anayeona hawezi kufanya kazi
serikalini kwa mshahara wa Sh 957, 700 atafute sehemu nyingine.
Alisema huduma kwenye hospitali nchini zimerejea hali ya kawaida na
baadhi ya madaktari wamekubaliana na Serikali na wengine wasiokubaliana
watatafuta pa kwenda.
Akifungua mkutano wa siku tatu wa Watafiti wa Magonjwa ya Binadamu
ulioshirikisha watafiti, madaktari na maprofesa kutoka nchi mbalimbali
duniani, Dk Mwinyi alisema tamko alilotoa Rais Jakaya Kikwete,
linaeleweka.
Wanahabari wazushi
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki
amekemea tabia ya baadhi ya vyombo vya habari kuvumisha kuwapo mgomo wa
madaktari kwenye hospitali za mkoa huo, jambo ambalo si sahihi na
limekuwa likiumiza wananchi, anaripoti Hellen Mlaky.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Sadiki alisema
hali inayovumishwa si sahihi na madaktari katika hospitali za mkoa huo
ikiwamo Temeke, Amana na Mwananyamala wanaendelea na kazi kama kawaida.
Muhimbili kutathiminiwa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma, Celina Kombani, wakati
akijibu hoja za wabunge jana, alisema katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, kuna watumishi wengi na hivyo Serikali itafanya tathimini ya
kazi ya kila mtumishi ili kufahamu kama wote wanahitajika au la.
Alisema baada ya kutathimini kazi za watendaji wote, wataangalia sifa
zao kama zinawaruhusu kuendelea kufanya kazi katika hospitali hiyo na
kama haziwaruhusu, watahamishwa.
Naye Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo akizungumza na waandishi wa habari
nje ya ukumbi wa Bunge, alisema anaunga mkono hotuba ya Rais Jakaya
Kikwete ya kuwaruhusu madaktari kwenda kwa mwajiri atakayewalipa Sh
milioni 7.7.
Cheyo ambaye alitaka vyama vyote vya siasa kuunga mkono hotuba hiyo,
alisema fedha kamwe haiwezi kununua maisha ya mwanadamu na kuwataka
madaktari kurudi kazini.