Katika mapambano ya ukombozi ni lazima wengine wawe mbegu, sisi tuko tayari kufanywa mbegu.”
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kimebaini mkakati wa makusudi wa kuwadhuru viongozi wakuu wa chama hicho. Kimedai mpango unaratibiwa na baadhi ya vigogo katika idara ya usalama wa taifa, kwa lengo la kudhoofisha harakati za chama hicho kufichua ufisadi na kudhoofisha serikali na chama kinachotawala.
Viongozi wanaolengwa katika mkakati huo ni Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa, Mbunge wa Ubungo John Mnyika na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbles Lema.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema taarifa za uhakika zilizoangukia mikononi mwa intelijensia ya chama hicho zinathibitisha dhamira ya vigogo hao kuwadhuru viongozi wao. Mbowe aliwataka wananchi wasisite kupigania haki yao, hata kama dhamira hiyo chafu ingefanikiwa.
Alisema mpango huo unaratibiwa na mmoja wa viongozi wa juu kutoka Idara ya Usalama wa Taifa (jina linahifadhiwa). Vile vile, alimtaja mmoja wa watu wanaofuatilia nyendo za Mnyika na kwamba mkakati wa kwanza wa kumdhuru mbunge huyo ni kumuwekea sumu au kuvamiwa na watu watakaodhaniwa kuwa ni majambazi.
“Katika siku za hivi karibuni kumejitokeza mambo tunayoamini yamepangwa na Idara ya Usalama wa Taifa, na lengo lao kuu ni kudhoofisha harakati za kuwatetea Watanzania juu ya madhila yanayofanywa na serikali ya CCM. Wamekuwa wakiwafuatialia viongozi wetu kwa saa 24 wakidhani CHADEMA tunafanya mambo kwa siri,” alisema Mbowe.
Mbowe aliongeza kuwa idara hiyo inatumia ofisi na mamlaka yao vibaya kwa kulinda usalama wa mafisadi badala ya kuangalia maslahi ya taifa, na kwamba CHADEMA haitarudi nyuma katika kuwakosoa pale itakapokuwa inabidi.
Alisema CHADEMA ina vyanzo vingi vya kupata habari, na kwamba inafanya kazi na watu waadilifu serikalini. Alisema chama hakiwezi kukaa kimya kinapopata taarifa za kudhurika kwa viongozi au wanachama wake, ili itakapobidi hatua mwafaka zichukuliwe.
Alisema kwamba miongoni mwa sababu zinazoifanya serikali ihahe na kutumia idara hiyo vibaya, ni mgomo wa madaktari ambao serikali imeshindwa kuushughulikia, huku CHADEMA ikiibana iwasikilize madaktari badala ya kuwatisha.
Baadhi ya wanapropaganda wa CCM wamekuwa wakidai kwamba CHADEMA ndiyo inayochochea madaktari kugoma, badala ya kuishinikiza serikali isikilize madai yao na kuwapa majibu mwafaka.
“Wametoa kauli zao bungeni kuwa tuko nyuma ya mgomo huo, na hata walipomteka Dk. Ulimboka walimuuliza kama sisi tunahusika… Ninachoweza kusema ni kwamba hatuhusiki na hatufurahishwi na mgomo kwa kuwa wanaoumia ni wananchi wa kawaida, ila hatutasita kuwaunga mkono wafanyakazi wowote wenye madai ya msingi ambayo serikali imeshindwa kutekeleza,” alisisitiza Mbowe.
Alisema Kamati Kuu ya chama inakaa leo kujadili, miongoni mwa mambo mengine, harakati hizo za usalama wa taifa dhidi ya CHADEMA.
Akizungumzia tishio hilo Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa, alisema suala la yeye kufuatiliwa limeanza siku nyingi tangu akiwa Bungeni. Alikumbusha jinsi watu hao walivyomwekea kinasa sauti chumbani mwake.
Alisema licha ya tukio hilo kuripotiwa polisi na vinasa sauti hivyo kuchukuliwa, hadi leo hakuna taarifa zozote za kueleweka juu ya suala hilo; na hata walipofuatilia katika maeneo husika hakukuwa na maelezo.
“Kama mnakumbuka baadhi ya vyombo vya habari viliandika orodha ya watu wanaotaka kudhuriwa akiwamo Dk. Mwakyembe na mimi; hata baada ya tukio lililompata Mwakyembe serikali bado imekaa kimya bila kueleza imefikia wapi,” alisema Dk. Slaa.
Alisema kupitia idara hiyo ya usalama wa taifa, kumekuwa na mikakati mbali mbali ya kumdhuru na miongoni mwa hayo ni hatua ya mkewe Josephine Mushumbushi, kujeruhiwa kwa risasi akiwa na mimba, lengo likiwa ni kumnyamazisha.
“Wanafikiri kwa kututisha tutaweza kunyamaza…hilo haliwezekani. Tulifanya hivyo katika suala la EPA, na kwa kuwa katika mapambano ya ukombozi ni lazima wengine wawe mbegu, sisi tuko tayari kufanywa mbegu,” alisema Dk. Slaa.
Mnyika alisema amekuwa akipata taarifa kutoka kwa watu walio serikalini wakimueleza sababu za kuandamwa kwake ni kauli yake Bungeni juu ya udhaifu wa taasisi ya urais. Alimtaja mtu aliyekabidhiwa jukumu hilo.
“Baada ya taarifa hizi nilishauriana na familia yangu pamoja na viongozi wangu, kwa pamoja tumekubaliana tusirudi nyuma kwa kuwa kwa imani yangu mwenye uwezo wa kuua ni Mwenyezi Mungu, ambaye ninamuachia hatima yangu,” alisema Mnyika.
Alisema kabla ya watu wa idara ya usalama wa taifa hawajamdhuru wanapaswa kupitia michango yake mbali mbali aliyoitoa bungeni, kwa kuwa kazi yake ni kutetea maslahi ya taifa badala ya kusimama na mafisadi.
Naye Godbles Lema, alisema baada ya kupata taarifa hizo za kutaka kudhuriwa alizidisha uangalifu katika mienendo yake na kubaini gari aina ya Toyota Carina likiwa na jukumu la kufuatilia nyendo zake.
Alisema baada ya kubaini hali hiyo ya kufuatiliwa katika maeneo tofauti na watu wale wale aliamua kuwauliza dhamira yao na kwamba watu hao hawakumjibu kitu zaidi ya kumuuliza: “Wewe ndiye mbunge wa Arusha uliye likizo?”
“Walianzia pale Serena Hotel, hata nilipobadilisha gari wakaamua kuliandama hilo nililochukua kwa mara ya pili. Niliwauliza dhamira yao hawakunijibu, na sasa kila asubuhi utawaona wako pale hotelini wananisubiri tu,” alisema Lema.