Katika mapambano ya ukombozi ni lazima wengine wawe mbegu, sisi tuko tayari kufanywa mbegu.”
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kimebaini mkakati
wa makusudi wa kuwadhuru viongozi wakuu wa chama hicho. Kimedai mpango
unaratibiwa na baadhi ya vigogo katika idara ya usalama wa taifa, kwa
lengo la kudhoofisha harakati za chama hicho kufichua ufisadi na
kudhoofisha serikali na chama kinachotawala.
Viongozi wanaolengwa katika mkakati huo ni Katibu Mkuu Dk. Willibrod
Slaa, Mbunge wa Ubungo John Mnyika na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbles
Lema.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema taarifa za uhakika
zilizoangukia mikononi mwa intelijensia ya chama hicho zinathibitisha
dhamira ya vigogo hao kuwadhuru viongozi wao. Mbowe aliwataka wananchi
wasisite kupigania haki yao, hata kama dhamira hiyo chafu ingefanikiwa.
Alisema mpango huo unaratibiwa na mmoja wa viongozi wa juu kutoka
Idara ya Usalama wa Taifa (jina linahifadhiwa). Vile vile, alimtaja
mmoja wa watu wanaofuatilia nyendo za Mnyika na kwamba mkakati wa kwanza
wa kumdhuru mbunge huyo ni kumuwekea sumu au kuvamiwa na watu
watakaodhaniwa kuwa ni majambazi.
“Katika siku za hivi karibuni kumejitokeza mambo tunayoamini
yamepangwa na Idara ya Usalama wa Taifa, na lengo lao kuu ni kudhoofisha
harakati za kuwatetea Watanzania juu ya madhila yanayofanywa na
serikali ya CCM. Wamekuwa wakiwafuatialia viongozi wetu kwa saa 24
wakidhani CHADEMA tunafanya mambo kwa siri,” alisema Mbowe.
Mbowe aliongeza kuwa idara hiyo inatumia ofisi na mamlaka yao vibaya
kwa kulinda usalama wa mafisadi badala ya kuangalia maslahi ya taifa, na
kwamba CHADEMA haitarudi nyuma katika kuwakosoa pale itakapokuwa
inabidi.
Alisema CHADEMA ina vyanzo vingi vya kupata habari, na kwamba inafanya
kazi na watu waadilifu serikalini. Alisema chama hakiwezi kukaa kimya
kinapopata taarifa za kudhurika kwa viongozi au wanachama wake, ili
itakapobidi hatua mwafaka zichukuliwe.
Alisema kwamba miongoni mwa sababu zinazoifanya serikali ihahe na
kutumia idara hiyo vibaya, ni mgomo wa madaktari ambao serikali
imeshindwa kuushughulikia, huku CHADEMA ikiibana iwasikilize madaktari
badala ya kuwatisha.
Baadhi ya wanapropaganda wa CCM wamekuwa wakidai kwamba CHADEMA ndiyo
inayochochea madaktari kugoma, badala ya kuishinikiza serikali isikilize
madai yao na kuwapa majibu mwafaka.
“Wametoa kauli zao bungeni kuwa tuko nyuma ya mgomo huo, na hata
walipomteka Dk. Ulimboka walimuuliza kama sisi tunahusika… Ninachoweza
kusema ni kwamba hatuhusiki na hatufurahishwi na mgomo kwa kuwa
wanaoumia ni wananchi wa kawaida, ila hatutasita kuwaunga mkono
wafanyakazi wowote wenye madai ya msingi ambayo serikali imeshindwa
kutekeleza,” alisisitiza Mbowe.
Alisema Kamati Kuu ya chama inakaa leo kujadili, miongoni mwa mambo
mengine, harakati hizo za usalama wa taifa dhidi ya CHADEMA.
Akizungumzia tishio hilo Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa, alisema
suala la yeye kufuatiliwa limeanza siku nyingi tangu akiwa Bungeni.
Alikumbusha jinsi watu hao walivyomwekea kinasa sauti chumbani mwake.
Alisema licha ya tukio hilo kuripotiwa polisi na vinasa sauti hivyo
kuchukuliwa, hadi leo hakuna taarifa zozote za kueleweka juu ya suala
hilo; na hata walipofuatilia katika maeneo husika hakukuwa na maelezo.
“Kama mnakumbuka baadhi ya vyombo vya habari viliandika orodha ya watu
wanaotaka kudhuriwa akiwamo Dk. Mwakyembe na mimi; hata baada ya tukio
lililompata Mwakyembe serikali bado imekaa kimya bila kueleza imefikia
wapi,” alisema Dk. Slaa.
Alisema kupitia idara hiyo ya usalama wa taifa, kumekuwa na mikakati
mbali mbali ya kumdhuru na miongoni mwa hayo ni hatua ya mkewe Josephine
Mushumbushi, kujeruhiwa kwa risasi akiwa na mimba, lengo likiwa ni
kumnyamazisha.
“Wanafikiri kwa kututisha tutaweza kunyamaza…hilo haliwezekani.
Tulifanya hivyo katika suala la EPA, na kwa kuwa katika mapambano ya
ukombozi ni lazima wengine wawe mbegu, sisi tuko tayari kufanywa mbegu,”
alisema Dk. Slaa.
Mnyika alisema amekuwa akipata taarifa kutoka kwa watu walio
serikalini wakimueleza sababu za kuandamwa kwake ni kauli yake Bungeni
juu ya udhaifu wa taasisi ya urais. Alimtaja mtu aliyekabidhiwa jukumu
hilo.
“Baada ya taarifa hizi nilishauriana na familia yangu pamoja na
viongozi wangu, kwa pamoja tumekubaliana tusirudi nyuma kwa kuwa kwa
imani yangu mwenye uwezo wa kuua ni Mwenyezi Mungu, ambaye ninamuachia
hatima yangu,” alisema Mnyika.
Alisema kabla ya watu wa idara ya usalama wa taifa hawajamdhuru
wanapaswa kupitia michango yake mbali mbali aliyoitoa bungeni, kwa kuwa
kazi yake ni kutetea maslahi ya taifa badala ya kusimama na mafisadi.
Naye Godbles Lema, alisema baada ya kupata taarifa hizo za kutaka
kudhuriwa alizidisha uangalifu katika mienendo yake na kubaini gari aina
ya Toyota Carina likiwa na jukumu la kufuatilia nyendo zake.
Alisema baada ya kubaini hali hiyo ya kufuatiliwa katika maeneo
tofauti na watu wale wale aliamua kuwauliza dhamira yao na kwamba watu
hao hawakumjibu kitu zaidi ya kumuuliza: “Wewe ndiye mbunge wa Arusha
uliye likizo?”
“Walianzia pale Serena Hotel, hata nilipobadilisha gari wakaamua
kuliandama hilo nililochukua kwa mara ya pili. Niliwauliza dhamira yao
hawakunijibu, na sasa kila asubuhi utawaona wako pale hotelini
wananisubiri tu,” alisema Lema.