Monday, July 9, 2012

Chadema yaukana mgomo wa madaktari


katibu mkuu wa chadema -Dr. Wilbroad Slaa

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimekanusha kuhusika kwa njia yoyote katika kuunga mkono mgomo wa madaktari nchini.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumzia masuala mbalimbali kuhusu chama hicho pamoja na kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kinachoanza leo.
Mbowe alisema pamoja na kutohusika na mgomo huo, lakini wanaunga mkono ushauri wa viongozi wa dini kuitaka Serikali kutafakari upya na kurudi mezani kwa ajili ya majadiliano.
Akifafanua zaidi kuhusu mgomo huo, Mbowe alisema zipo taarifa zisizo za kweli kuhusu chama hicho kuhusika katika mgomo wa madaktari zinazodai kuwa Chadema imekuwa na mazungumzo ya mara kwa mara na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka.
“Hatujawahi kufanya mazungumzo yanayohusu kuwatuma madaktari kugoma lakini ieleweke kuwa hatutosita kuitetea taaluma hiyo ya madaktari na hata walimu na tutaungana katika madai yao tukiitaka Serikali kutekeleza wajibu wake,” alisema Mbowe.
Kuhusu kauli ya viongozi wa dini kuitaka Serikali kutafakari na kurudi mezani ili kulipatia suluhu suala hilo la madaktari kwani fedha zilizowasomesha ni nyingi, alisema chama hicho kinaunga mkono kauli hiyo.
Mbowe pia alidai kuwepo kwa hofu na tishio la usalama wa maisha ya viongozi watatu wa chama hicho wakitishiwa kuumizwa, kuteswa ama kudhuriwa kwa njia mbalimbali.
Aliwataja viongozi hao ambao usalama wa maisha yao uko hatarini kuwa ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mbunge wa Ubungo John Mnyika na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa.
Alisema kwamba pamoja na vitisho hivyo Chadema haitoenda Polisi kushitaki .