TUME ya Kukusanya na Kuratibu Maoni kuhusu Mabadiliko ya Katiba, leo
inaanza rasmi kazi ya kukusanya maoni kupitia mikutano ya hadhara na
wananchi kwa awamu yake ya kwanza.
Katika awamu hiyo, Tume hiyo inaanza na mikoa minane ambayo ni
Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani na Shinyanga
na itafanya kazi kuanzia leo hadi Julai 30, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Katibu wa Tume hiyo, Assaa Rashid, katika Mkoa wa
Dodoma, itaanza na Wilaya ya Bahi; mkoani Kagera itaanza na Biharamulo;
Manyara itaanza na Mbulu na Pwani ni Mafia.
Alisema kwa Mkoa wa Shinyanga itaanza na Kahama na kwa Mkoa wa Tanga
ni Wilaya ya Lushoto. Kwa Zanzibar, itaanza kukusanya maoni katika Mkoa
wa Kusini Unguja katika Wilaya ya Kusini.
Rashid alisema katika kufanikisha ukusanyaji huo wa maoni kwa ufasaha
wajumbe wa tume hiyo na watumishi wa Sekretarieti wamejigawa katika
makundi saba.
Wakati akikabidhiwa ofisi za kufanyia kazi, Mwenyekiti wa Tume hiyo,
Jaji Joseph Warioba aliwataka kwa dhati wale waliowapendekeza wajumbe wa
tume hiyo kuwaacha wafanye kazi walioteuliwa kuifanya.
Aliwaonya wale wote waliopendekeza majina ya wajumbe hao wasitarajie
kuwa wajumbe hao watafanya watakavyo wao kwani tume hiyo ni ya
Watanzania na si watu wachache ambapo aliainisha majukumu ya tume hiyo
kuwa si kuandika Katiba, bali kukusanya maoni, kuyachambua na kuandika
rasimu ya Katiba.
Akimkabidhi funguo za jengo hilo la ghorofa 10 kuwa ofisi ya Tume
hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema pamoja na jengo
hilo, pia kwa maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete, tume hiyo itapatiwa
magari 30 kwa ajili ya kuiwezesha kiusafiri.
Rais Jakaya Kikwete alipotembelea ofisi za tume hiyo alisema hana
wasiwasi na uwezo wa wajumbe wa tume hiyo katika kuifanya kazi hiyo
vizuri na kwa ufanisi na kuwataka wajumbe hao kuwa huru katika kuifanya
kazi yao bila kuruhusu kuingiliwa na mtu yeyote.
Wajumbe 30 wa tume hiyo pamoja Jaji Warioba ni Makamu Mwenyekiti wa
tume hiyo, Jaji Mkuu mstaafu Augustine Ramadhani, Profesa Mwesiga
Baregu, Riziki Mngwali, Dk Sengondo Mvungi, Jesca Mkuchu na Said El-
Maamry.
Wengine ni Profesa Palamagamba Kabudi, Humphrey Polepole, Yahya
Msulwa, Esther Mkwizu, Maria Kashonda, Al-Shaymaa Kwegry, Richard Lyimo,
John Nkolo, Mwantumu Malale na Joseph Butiku.
Kutoka Zanzibar ni Dk Salim Ahmed Salim, Fatma Said Ali, Omar Sheha
Mussa, Raya Suleiman Hamad, Awadh Ali Said, Ussi Khamis Haji, Salma
Maoulidi, Nassor Khamis Mohamed, Simai Mohamed Said na Muhammed Yussuf
Mshamba.
Wajumbe wengine ni Kibibi Mwinyi Hassan, Suleiman Omar Ali, Salama
Kombo Ahmed, Abubakar Mohamed Ali, Ally Abdullah Saleh na wajumbe wa
Sekretarieti ni Assa Ahmad Rashid ambaye ni Katibu na msaidizi wake
Casmir Sumba Kyuki. Shughuli za tume hiyo zinaratibiwa na sekretarieti
hiyo.