WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema hawezi kuvumilia vitendo vya kinyama vinavyofanywa na baadhi ya watu wasiomjua Mungu na kwamba ataendelea kupigania haki za wanyonge hadi pumzi yake ya mwisho. Waziri Sitta aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa la Anglikana la Matakatifu Andrew Magomeni jijini Dar es Salaam. Alisema viongozi wa dini wamekuwa mstari wa mbele kuhamasisha watu kutenda mambo mema katika jamii lakini bado kumekuwa na vitendo vya kinyama, rushwa, ubaguzi ambavyo vinafanywa na baadhi ya watu wasiopenda maendeleo ya watanzania. “Mimi nikiwa kama kiongozi ambae nafanya kazi kwa kasi zaidi kama jina langu linavyosema kwamba ni mtu wa kasi na viwango siwezi kuvifumbia macho vitendo vinavyofanywa na watu wasipopenda maendeleo,” alisema Sitta na kuongeza; “Serikali haina budi kuwashukuru viongozi wa dini nchini kwani wao ndiyo wapo mstari wa mbele kukemea watu kuacha mambo maovu lakini hata viongozi wa Serikali nao wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kupigania haki za watanzania bila kujali masilahi yao binasfi,” alisema. Alifafanua kwamba yeye anafanya kazi bila kumuogopa mtu na kwamba hawezi kuvumilia kuona watu wakinyimwa haki zao, kutokana na rushwa na ubaguzi jambo ambalo alikubaliki kwa jamii na kwamba halileti picha nzuri kwa watanzania. “Jina langu ni Samuel Sitta ambapo tafsiri yake ni (Standard- Speed), yani ni mtu ambaye nafanya kazi bila kumuogopa mtu kwani kiwango changu ni cha hali ya juu na kwamba kupitia tafsiri hii inataendelea kupigania haki za wanyonge,” alisema. Waziri Sitta alibainisha kwamba mambo mengi katika nchi yanaepushwa na viongozi wa dini kwa kukemea maovu na kwamba la sivyo kungezidi kutokea mambo yasiyofaa kwa jamii. “Viongozi wetu wa dini zote hapa nchini wapo mstari wa mbele kukemea mambo maovu na kwamba kazi yao hii inawasaidia hata Serikali kupambana na mambo yasiyofaa kwa jamii na kwamba wanatakiwa kuungwa mkono ilikusaidia kuwabadilisha watu wasio mjua mungu,” alisema na kuongeza; “Ukimpenda Mungu huwezi kushuhudia vitendo vya uonevu vikifanyika na kuona kama kitu cha kawaida kwani vitendo hivyo havimpendezi Mungu, sasa kutokana na mambo kama haya ambayo hayaleti picha nzuri kwa jamii nitahakikiksha na pambana navyo hadi mwisho wa pumzi yangu,”alisema. Aidha alisema kwamba Serikali haina budi kuwashukuru viongozi wa dini kwani wao wanatoa mchango mkubwa kuwasidia kupambana na maovu na kwamba taifa linaweza kubadilika na wanachi kutenda mambo mema kama viongozi hao wataungwa mkono. “Kwa sisi tunaotunga sheria tunafahamu kwamba sheria peke yake haitoshi kwani siku hizi mtu anaweza kuinunua haki kwa sababu watu hawamuogopi Mungu, jambo ambalo linasikitisha katika jamii, sasa ni vyema sote tukaungana kukemea mambo maovu ili yasitokee katika jamii yetu ya kitanzania,” alisema. Katika hatua nyingine, Waziri Sitta alisema kwamba viongozi na watumishi wengine wa Serikali wanaweza kuiga mfano wa Waziri wa Uchukuzi Dk Harson Mwakeymbe kwani ni kiongozi anayetetea masilahi ya wananchi. “Dk Mwakyembe licha ya kuwa kiongozi ni rafiki yangu mkubwa na kwamba navutiwa na utendaji wake wa kazi kwani sizani kama kuna kiongozi anaweza kupanda daladala kuangalia suala la nauli au kusafiri na gari moshi kama anavyofanya Mwakyembe,” alisema. |