Serikali yakiri kutoa fedha pungufu Singida
OFISI ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imekiri kuwa katika kipindi cha mwaka 2008/09 haikupeleka katika Halmashauri ya Singida Sh 302 milioni zilizokusudiwa.
Badala yake Serikali imesema kiasi kilichopelekwa huko ni Sh 96 milioni tu jambo ambalo ni kinyume na utaratibu na sheria za nchi.
Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri wakati akijibu swali la Tundu Lissu (Singida Mashariki-Chadema) ambaye alitaka kujua ni kiasi gani cha fedha kilipelekwa katika halmashauri hiyo.
Mbunge huyo pia alitaka kujua kiasi gani ambacho ni asilimia 20 kilipelekwa katika Kata za Jimbo la Singida Mashariki na akataka iundwe tume huru ya kuchunguza fedha hizo ambazo hazikufika huko.
Naibu Waziri alisema katika kipindi hicho, Serikali ilipanga kupeleka katika vijiji vya Halmashauri ya Wilaya ya Singida asilimia 20 ambazo kisheria zilikuwa ni 320 milioni lakini jumla ya Sh 205 milioni hazikupelekwa huko.
Mwanri alisema kutokana na fedha kutopelekwa katika vijiji, Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa iliagiza halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa fedha hizo zinapelekwa katika maeneo husika haraka iwezekanavyo.
Kuhusu fedha kutofika katika vijiji vilivyokusudiwa, Mwanri alisema hilo lilitokana na akaunti nyingi za vijiji kufungwa na hivyo halmashauri ikatuma fedha katika akaunti za kata zao.
Hata hivyo alisema ni kosa kwa mujibu wa sheria fedha kutofika katika vijiji husika na akamwagiza Mkuu wa Mkoa wa Singida kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa fedha hizo zinapelekwa huko haraka.