Serikali yakiri kutoa fedha pungufu Singida
OFISI ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)
imekiri kuwa katika kipindi cha mwaka 2008/09 haikupeleka katika
Halmashauri ya Singida Sh 302 milioni zilizokusudiwa.
Badala yake Serikali imesema kiasi kilichopelekwa huko ni Sh 96 milioni tu jambo ambalo ni kinyume na utaratibu na sheria za nchi.
Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri wakati akijibu swali la
Tundu Lissu (Singida Mashariki-Chadema) ambaye alitaka kujua ni kiasi
gani cha fedha kilipelekwa katika halmashauri hiyo.
Mbunge huyo pia
alitaka kujua kiasi gani ambacho ni asilimia 20 kilipelekwa katika Kata
za Jimbo la Singida Mashariki na akataka iundwe tume huru ya kuchunguza
fedha hizo ambazo hazikufika huko.
Naibu Waziri alisema
katika kipindi hicho, Serikali ilipanga kupeleka katika vijiji vya
Halmashauri ya Wilaya ya Singida asilimia 20 ambazo kisheria zilikuwa
ni 320 milioni lakini jumla ya Sh 205 milioni hazikupelekwa huko.
Mwanri alisema kutokana na fedha kutopelekwa katika vijiji, Kamati ya
Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa iliagiza halmashauri hiyo
kuhakikisha kuwa fedha hizo zinapelekwa katika maeneo husika haraka
iwezekanavyo.
Kuhusu fedha kutofika katika vijiji
vilivyokusudiwa, Mwanri alisema hilo lilitokana na akaunti nyingi za
vijiji kufungwa na hivyo halmashauri ikatuma fedha katika akaunti za
kata zao.
Hata hivyo alisema ni kosa kwa mujibu wa sheria
fedha kutofika katika vijiji husika na akamwagiza Mkuu wa Mkoa wa
Singida kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa fedha hizo
zinapelekwa huko haraka.