Saturday, July 7, 2012

Serikali, madaktari wazidi kuvutana

Sasa yawashtaki ili wachukuliwe hatua
SERIKALI imewashtaki katika Baraza la Madaktari Tanzania, madaktari wanafunzi wa vitendo walioshiriki kwenye mgomo wa madaktari uliofanyika nchini kwa tuhuma za kuhatarisha maisha ya wagonjwa na kukiuka maadili ya taaluma yao.
Kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, madaktari wanafunzi hao zaidi ya 200 waliandikiwa barua zenye kumbukumbu namba MP. 72763 wakishtakiwa kwa baraza hilo ili liwachukulie hatua za kinidhamu ikiwemo kuwafutia usajili wao endapo watabainika kutenda kosa kilaatuma.
Kwa nyakati tofauti madaktari wanafunzi hao waliotimuliwa hospitalini hapo na uongozi wa MNH walipokea barua hizo za Julai 2, 2012 na kutakiwa kwanza kutoa taarifa kwa baraza la madaktari baada ya kupata barua zao.
Hata hivyo, jana ilikuwa ni siku ya mwisho kwa madaktari wanafunzi hao kuripoti wizarani baada ya kuwepo kwa agizo la kufanya hivyo lililotolewa na MNH mwanzoni mwa wiki.
Kwa mujibu wa kila barua waliyopewa madaktari hao ambayo pia imesainiwa na P.A.Chando kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, madaktari hao walikuwa katika mgomo kati ya Juni 23 hadi Juni 29 mwaka huu.
Imeelezwa kuwa walipelekwa kufanya kazi MNH kwa ajili ya kuboresha taaluma yao katika mafunzo ya vitendo lakini wizara imepokea malalamiko kwamba walikuwa hawafanyi kazi katika kipindi hicho na badala yake walikuwa wakishiriki mgomo.
Barua hiyo imefafanua kuwa kitendo hicho cha kushiriki mgomo si tu kilihatarisha maisha na usalama wa wagonjwa, bali pia kimekwenda kinyume na taratibu za taaluma hiyo ya utabibu.
Hatua ya kuwashtaki kwenye baraza hilo, imetokana na baraza hilo kuhusika katika usajili wa madaktari wanafunzi hata hivyo wizara imelitaka kufanya uchunguzi wa kina wa madai hayo na kuchukua hatua za nidhamu.
Wakati hayo yakiendelea, huduma katika hospitali hiyo ya Taifa na Kitengo cha Mifupa cha hospitali hiyo (MOI) zimeendelea kudorora kwa wagonjwa wengi kukosa huduma baada ya madaktari kuendelea kugoma.
Mgomo unaoendelea sasa unaelezwa kwamba ni mshtuko uliowapata madaktari baada ya kupokea taarifa za hali mbaya ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka, anayepatiwa matibabu nchini Afrika Kusini.
Dk. Ulimboka alitekwa, kupigwa na kutelekezwa kwenye msitu wa Pande ulioko nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam hivi karibuni, jambo lililoibua maswali mengi hadi serikali kutuhumiwa kuhusika.
Licha ya uongozi wa MHN kuendelea kuwahadaa watanzania kwamba huduma katika hospitali hiyo zimerejea, hali hiyo imeonekana tofauti.
Ofisa Uhusiano wa MNH, Aminieli Eligaeshi, alikataa kuzungumza na waandishi wa habari waliohoji sababu za kuendelea kuwepo kwa mgomo, badala yake alisema atatuma taarifa kwa vyombo vya habari kupitia barua pepe.
Gazeti hili lilitembelea baadhi ya wodi za hospitali hiyo na kukuta idadi ndogo ya wagonjwa waliodai kwamba wanahudumiwa na wauguzi huku askari wakilinda mlango wa mapokezi ya dharura ambao haukuwa na wagonjwa.
Kuhusu afya ya Dk. Ulimboka, mmoja wa madaktari hao aliyetaka jina lake lisichapishwe gazetini alisema juhudi za madaktari zinaendelea huko Afrika Kusini ili kunusuru maisha ya mwenyekiti huyo.