Saturday, July 7, 2012

Madaktari waliogoma watakiwa kujieleza

MADAKTARI waliokuwa kwenye mafunzo kwa vitendo wakagoma hivi karibuni wameanza kuripoti katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na kuagizwa kwenda wajieleze mbele ya Baraza la Madaktari kutokana na kushiriki mgomo.
Akizungumza jana, Msemaji wa Wizara hiyo, Nsachriss Mwamwaja, alisema kwa nyakati tofauti ndani ya wiki hii, madaktari hao wameripoti wizarani tayari kujua utaratibu unaofuata baada ya mgomo, suala linalodaiwa kuwa kinyume na misingi ya taaluma hiyo.
Awali Wizara hiyo juzi, ilitoa agizo kwa mdaktari hao nchi nzima waripoti hapo baada ya kushiriki mgomo unaoendelea katika baadhi ya maeneo nchini ili kuelezwa utaratibu mwingine.
“Hadi leo (jana) kuna idadi kubwa ya madaktari walioripoti hapa, hatua hiyo inatoa nafasi nyingine kwao kwenda kujieleza mbele ya Baraza la Madaktari, kutokana na hatua yao ya kushiriki mgomo huo,” alisema Mwamaja.
Alisema baada ya Baraza kumaliza kupokea maelezo ya madaktari hao, litapeleka ripoti yake wizarani na kumkabidhi Waziri mwenye dhamana kwa ajili ya hatua zingine.
Hali ya Ulimboka Akizungumzia hali ya Dk Stephen Ulimboka anayeendelea na matibabu Afrika Kusini, Katibu wa Chama cha Madaktari Nchini (MAT), Dk Rodrick Kabangila, alisema hali yake ni nzuri na anaendelea na matibabu kama kawaida huku akiponda ‘uvumi’ uliozagaa mitaani kuwa amefariki dunia.
“Hatujui hizi taarifa zimetoka wapi, nafikiri zinasambazwa na baadhi ya watu wasiompenda na kumtakia mema, ila ukweli maendeleo yake ni mazuri hata leo tunavyozungumza, tumepata taarifa zake,” alisema Dk Kabangila bila kueleza kama alizungumza na Ulimboka au watu wengine wa karibu yake.
Alisema tangu afikishwe nchini humo hali yake imekuwa ikiendelea kuimarika siku hadi siku, tofauti na kauli zinazotolewa na watu mitaani ana hali mbaya.
Juzi taarifa zisizo rasmi za kubadilika ghafla kwa hali ya Dk Ulimboka zilisababisha madaktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kurejea kwenye mgomo na kuacha wagonjwa bila huduma. Jana ulishuhudiwa umati wa wagonjwa hasa wa Moi wakirudishwa nyumbani huku sababu ikitolewa kuwa madaktari hawapo.
Mmoja wa madaktari alisema chanzo cha mabadiliko ya madaktari hao ni taarifa zilizowafikia mapema asubuhi, kuwa Dk Ulimboka ana hali mbaya na kwamba hajitambui.
“Kweli, tulisharejea kazini na kuanza kutoa huduma, lakini tumepata taarifa kuwa Dk Ulimboka anapumulia mashine na hajitambui, hili limetuchanganya sana,” alisema daktari huyo bila kutaka kujitambulisha.
Aidha, chanzo kingine hospitalini hapo kilithibitisha kuwapo kwa taarifa za hali ya Dk Ulimboka kuzidi kuwa mbaya na baada ya taarifa hizo kusambaa, madaktari waliokuwa kazini walitawanyika.
Msemaji wa taasisi hiyo, Jumaa Almasi alipoulizwa kuhusu hali hiyo, hakuzungumza chochote zaidi ya kusema wagonjwa wanatibiwa na huduma zinaendelea kama kawaida.
Dk Kabangila alikiri kusikia tetesi za hali ya Dk Ulimboka kubadilika na kuwa mbaya huku wengine wakidai amefariki dunia jambo ambalo aligoma kulithibitisha.
“Naomba nisizungumze chochote kuhusu hali ya Dk Ulimboka … sina uhakika na hayo na mimi pia nimeyasikia, ila taarifa niliyonayo tangu jana jioni (juzi) hali yake ilikuwa inaendelea hivyo hivyo,” alisema Dk Kabangila bila kufafanua