Tuesday, June 26, 2012

Mbunge ataka walioua mashirika wanyongwe

MBUNGE wa Nkasi Kaskazini, Ali Keisy Mohamed (CCM) ametaka walioua mashirika ya umma wakamatwe, wanyongwe.
Mbunge huyo amesema bungeni mjini Dodoma kuwa, walioua mashirika ya umma ni wauaji kwa kuwa matendo yao yamesababisha wananchi wapoteze maisha kwa kukosa huduma.
Mohamed amesema, kuna sheria mbaya nchini zinazolinda wezi na kwamba, na kwamba, kama walioua mashirika ya umma wamekufa, pingu ziwekwe kwenye makaburi yao.
“Adhabu yao kali ndugu zangu ni kuwanyonga…wale wote waliofilisi mashirika ya umma wafungwe, kama amekufa pingu ziwekwe kwenye kaburi lake” amesema na kutaka mikataba ichunguzwe.
Mbunge huyo amesema, kama Polisi na Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) wameshindwa kuwakamata mafisadi, wachawi wapewe hiyo kaz, wapige ngoma ili wahusika walete fedha walizoiba.
Mohamed amehoji kama wala rushwa hawajulikani, na ametaka Takukuru nao wachunguzwe. Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, amesema, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda awaagize Takukuru wachunguze tuhuma kwamba kuna Watanzania sita wenye shilingi bilioni 303 katika benki za Uswisi.
Zitto amesema bungeni kuwa, Takukuru wachunguze watuhumiwa ni akina nani, na wamepata vipi fedha hizo, na ikithibitika wamezipata isivyo halali, fedha hizo zirudishwe nchini.
Mbunge wa Viti Maalum, Maryam Msabaha (Chadema), amesema bungeni kuwa, waliohujumu uchumi wa nchi wafungwe na wafilisiwe.
Wakati huohuo, Kessy amesema, uamuzi wa Serikali kutumia chenchi ya fedha zilizotumika kununulia rada kununua vitabu ni ufisadi.
Mbunge huyo amesema bungeni kuwa, fedha hizo zipelekwe kwenye halmashauri zitumike kununua madawati. Kessy amehoji, walioingia mkataba wa kununua rada wapo wapi?
“Huu ni ufisadi mwingine...wana masikio hawasikii, wana pua hawanusi, huu ndiyo mwisho”amesema bungeni wakati anachangia bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu.
Mbunge wa Ngorongoro, Kaika Telele (CCM), naye amepinga uamuzi wa kutumia chenchi ya rada kununua vitabu, ametaka fedha hizo zitumike kununua madawati na kujenga nyumba za walimu.

source: http://www.habarileo.co.tz/index.php/habari-za-kitaifa/