WAKATI mgomo wa madaktari nchi nzima ukiingia siku ya pili
jana, wanataaluma hao wameonekana kusalitiana kwa kutokuwa na msimamo
wa pamoja, kwani maeneo mengine yote huduma zimeendelea kama kawaida,
isipokuwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Madaktari hao wametangaza mgomo usio na kikomo kwa lengo la
kuishinikiza serikali kutimiza mahitaji yao, ikiwemo kuboresha
mazingira ya kufanyia kazi pamoja na kuwapandishia mishahara.
Licha ya mgomo huo kuanza kuleta madhara kwa wagonjwa katika siku ya
kwanza juzi, kwa madaktari kutofanya kazi katika hospitali mbalimbali
nchini, jana hali hiyo ilikuwa tofauti kwani sehemu nyingi huduma
ziliendelea kutolewa kama kawaida.
Tanzania Daima ilitembelea baadhi ya hospitali za serikali za jijini
Dar es Salaam za Amana, Mwananyamala na Temeke na kushuhudia wagonjwa
wakiendelea kupatiwa matibabu kama kawaida isipokuwa katika Hospitali ya
Muhimbili pekee ndiko huduma zilikuwa zikisuasua.
Madaktari katika hospitali hiyo jana walisitisha huduma zote zikiwemo
zile za dharura kwa wagonjwa, huku wale bingwa pekee ndio walikuwa
wakifanya kazi, ambapo baadhi ya wagonjwa waliruhusiwa kurudi nyumbani
hasa katika vitengo maalumu.
Baadhi ya wananchi wanaouguza ndugu zao hospitalini hapo, waliliambia
gazeti hili kuwa, iko haja ya serikali kufanya mazungumzo na madaktari
hao ili kuokoa maisha ya wagonjwa wasio na hatia.
Juma Saidi, Magdalena Joseph na Khalfan Juma ni baadhi ya wananchi
waliothibitisha kuwa hali ya Muhimbili ni mbaya kutokana na mgomo huo
wa madaktari usio na kikomo.
“Yaani hapa kama huna fedha mgonjwa wako atakufa, hatuoni madaktari
wala nini, na huduma zinasuasua, ukiwafuata wanakwambia ‘subiri
tunakuja’, yaani hata kuona wamevaa makoti yao tu hakuna, wapo wapo
tu,” alisema Magdalena.
Dk. Mwinyi awaangukia tena
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Husein Mwinyi amesema kuwa
bado anawasihi madaktari kutogoma na badala yake wakae wamkubalie kumpa
nafasi ya kukaa naye meza moja ili watatue matatizo yanayowakabili.
Akizungunza na Tanzania Daima jana mjini Dodoma, alisema kuwa hadi
jana hakupata taarifa za madaktari kugoma isipokuwa wale wa Muhimbili
na Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
Hata hivyo alisema kuwa, walioripotiwa kugoma ni wale madaktari wa
mafunzo kwa njia ya vitendo, lakini hospitali nyingine wanaendelea kama
kawaida.
Dk. Mwinyi alisema kuwa, kuna taarifa kuwa wapo baadhi ya madaktari
ambao wanawashinikiza wenzao kugoma, na kuwatishia endapo
hawatakubaliana na matakwa yao.
Alisema kutokana na taarifa hizo, serikali imeagiza waganga wakuu wa
hospitali na zahanati kuhakikisha wanakuwa karibu na vyombo vya usalama
ili kuweza kuwadhibiti wale ambao wataonekana kuleta fujo.
Aidha, Dk. Mwinyi alisema kuwa pamoja na madktari kugoma, lakini bado
anawashauri kukaa meza moja kufanya majadiliano na ikibidi kuondoa
kesi katika Mahakama ya Usuluhishi.
“Mimi nakubaliana na madaktari, nataka waboreshewe maslahi yao na
wafanye kazi katika mazingira mazuri, na ndiyo maana natamani wangenipa
nafsi ya kuongea nao kwanza,” alisema.
http://www.freemedia.co.tz/daima/habari
|