WAKATI mgomo wa madaktari nchi nzima ukiingia siku ya pili jana, wanataaluma hao wameonekana kusalitiana kwa kutokuwa na msimamo wa pamoja, kwani maeneo mengine yote huduma zimeendelea kama kawaida, isipokuwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Madaktari hao wametangaza mgomo usio na kikomo kwa lengo la kuishinikiza serikali kutimiza mahitaji yao, ikiwemo kuboresha mazingira ya kufanyia kazi pamoja na kuwapandishia mishahara. Licha ya mgomo huo kuanza kuleta madhara kwa wagonjwa katika siku ya kwanza juzi, kwa madaktari kutofanya kazi katika hospitali mbalimbali nchini, jana hali hiyo ilikuwa tofauti kwani sehemu nyingi huduma ziliendelea kutolewa kama kawaida. Tanzania Daima ilitembelea baadhi ya hospitali za serikali za jijini Dar es Salaam za Amana, Mwananyamala na Temeke na kushuhudia wagonjwa wakiendelea kupatiwa matibabu kama kawaida isipokuwa katika Hospitali ya Muhimbili pekee ndiko huduma zilikuwa zikisuasua. Madaktari katika hospitali hiyo jana walisitisha huduma zote zikiwemo zile za dharura kwa wagonjwa, huku wale bingwa pekee ndio walikuwa wakifanya kazi, ambapo baadhi ya wagonjwa waliruhusiwa kurudi nyumbani hasa katika vitengo maalumu. Baadhi ya wananchi wanaouguza ndugu zao hospitalini hapo, waliliambia gazeti hili kuwa, iko haja ya serikali kufanya mazungumzo na madaktari hao ili kuokoa maisha ya wagonjwa wasio na hatia. Juma Saidi, Magdalena Joseph na Khalfan Juma ni baadhi ya wananchi waliothibitisha kuwa hali ya Muhimbili ni mbaya kutokana na mgomo huo wa madaktari usio na kikomo. “Yaani hapa kama huna fedha mgonjwa wako atakufa, hatuoni madaktari wala nini, na huduma zinasuasua, ukiwafuata wanakwambia ‘subiri tunakuja’, yaani hata kuona wamevaa makoti yao tu hakuna, wapo wapo tu,” alisema Magdalena. Dk. Mwinyi awaangukia tena Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Husein Mwinyi amesema kuwa bado anawasihi madaktari kutogoma na badala yake wakae wamkubalie kumpa nafasi ya kukaa naye meza moja ili watatue matatizo yanayowakabili. Akizungunza na Tanzania Daima jana mjini Dodoma, alisema kuwa hadi jana hakupata taarifa za madaktari kugoma isipokuwa wale wa Muhimbili na Hospitali ya Mkoa wa Dodoma. Hata hivyo alisema kuwa, walioripotiwa kugoma ni wale madaktari wa mafunzo kwa njia ya vitendo, lakini hospitali nyingine wanaendelea kama kawaida. Dk. Mwinyi alisema kuwa, kuna taarifa kuwa wapo baadhi ya madaktari ambao wanawashinikiza wenzao kugoma, na kuwatishia endapo hawatakubaliana na matakwa yao. Alisema kutokana na taarifa hizo, serikali imeagiza waganga wakuu wa hospitali na zahanati kuhakikisha wanakuwa karibu na vyombo vya usalama ili kuweza kuwadhibiti wale ambao wataonekana kuleta fujo. Aidha, Dk. Mwinyi alisema kuwa pamoja na madktari kugoma, lakini bado anawashauri kukaa meza moja kufanya majadiliano na ikibidi kuondoa kesi katika Mahakama ya Usuluhishi. “Mimi nakubaliana na madaktari, nataka waboreshewe maslahi yao na wafanye kazi katika mazingira mazuri, na ndiyo maana natamani wangenipa nafsi ya kuongea nao kwanza,” alisema.
http://www.freemedia.co.tz/daima/habari |