Monday, June 25, 2012

Dany Mrwanda atua Simba na mkwara mzito


DORIS MALIYAGA
DANNY Mrwanda amesema yeye ni mtu wa vitendo zaidi na hataki maneno na amewaambia mashabiki wa Simba wasubiri vitu vyake uwanjani, lakini sasa anasaka jezi ya kuitumia baada ya namba saba anayoipenda kumilikiwa na Uhuru Suleiman.

Mshambuliaji huyo aliyekuwa akikipiga Hoang Anh Gia Lai ya Vietnam, juzi Alhamisi alifika katika mazoezi ya Simba yaliyofanyika Uwanja wa Sigara jijini Dar es Salaam na kupokewa kwa shangwe na mashabiki wa timu hiyo waliokuwapo uwanjani hapo. Hata hivyo hakufanya mazoezi.

Alisema: "Nimerudi Simba klabu iliyonilea, mara zote nilipopata timu nje, niliondokea hapa. Sina cha zaidi, ninawaahidi mashabiki wangu na Simba kwa ujumla juu ya kurudi kwangu, lakini ninawataka wasubiri kazi yangu uwanjani, nitafanya kazi kwa vitendo na si kuzungumza, wenyewe wananijua."

Mrwanda anayetarajia kufunga ndoa hivi karibuni na ambaye alishindana dau na Yanga aliongeza: "Unajua katika timu tunacheza watu 11, sitakuwa peke yangu, lakini kwa bidii yangu na ushirikiano wa wenzangu naamini tutafanikiwa kuipa Simba mafanikio."

Akiwa uwanjani hapo alipewa jukumu la kuchagua jezi ya mazoezi, zililetwa namba tofauti ikiwemo 23 na 5, lakini pia alipewa uhuru wa kuchagua nyingine kati ya 9 aliyokuwa akiitumia Gervais Kago, 11 na nane anayotumia Mwinyi Kazimoto.

Akizungumzia jezi atakayotumia, Mrwanda alisema: "Nilikuwa naitumia namba saba na ndiyo naipenda, lakini si unaona anaitumia bwana mkubwa hapo (Uhuru) kwa sababu zipo 11 na 9 nitachagua moja kati ya hizo."

Alifika uwanjani hapo akisindikizwa na marafiki zake, Nizar Khalfan na Pius Kisambale aliyeachwa na Yanga.