Huku hali ya mshikemshike
ikiendelea kushuhudiwa katika jengo la Westgate lenye maduka,
ufyatulianaji risasi umesikika ndani ya jengo hilo lenye maduka na
mikahawa zaidi ya themanini.
Wapiganaji wa Al shabaab wamewateka nyara raia
ambao idadi yao haijulikani. Walikuwemo ndani ya jengo wakiendelea na
shughuli zao kuanzia Jumamosi mchana wakati wapiganaji wa Al shabaab
walipowavamia na kuanza kufyatua risasi kiholela.Inaarifiwa wapiganaji hao wanaoaminika kuwa wanachama wa Al Shabaab ni kati ya kumi na kumi na watano na bado wangali ndani ya jengo hilo.
Ripoti zinasema kuwa ufyatulianaji mkubwa wa risasi umesikika katika jengo hilo kwa takriban dakika 15.
Harakati za kuendelea kumaliza operesheni hiyo zinaendelea lakini hali ya mateka walio ndani ya jengo hilo inaendelea kudorora.
Helikopta za polisi zinazunguka juu ya jengo hilo pamoja na ndege za kijeshi kushika doria. Vikosi vya usalama vinaendelea na operesheni kujaribu kuwanusuru waathiriwa wakati hali ikiwa ni ya ati ati katika eneo la shambulizi.
Awali jeshi la Kenya lilisema limeweza kudhibiti jengo hilo lote ingawa bado limetaja hali kuwa tete mno hasa katika kujaribu kuwaokoa mateka waliosalia ndani ya jengo hilo.
Ripoti zinasema kuwa watu 69 wamefariki katika shambulizi hilo la Al Shabaab kufikia sasa huku 175 wakijeruhiwa. Baadhi wametibiwa na kuondoka hospitalini. Baadhi ya majeraha waliyopata ni majereha ya risasi na kutokana na guruneti ambalo Al shabaa waliwarushia wale waliokuwa ndani ya mikahawa siku ya Jumamosi.
Kundi hilo limekiri kutekeleza shambulio hilo kutokana na hatua ya kenya kupelekeka majeshi yake nchini Somalia ili kukabiliana na wapiganaji hao.
Wakati huo huo makamu wa rais wa Kenya William Ruto amepewa ruhusa na mahakama ya ICC kurudi Kenya kuhudhuria shambulio la westgate
Chanzo: BBC-Swahili