Thursday, June 6, 2013
Kunyonyana ndimi kunachangia maambukizi ya Ukimwi?
Kubusiana kwa kunyonyana ndimi kunaweza kuchangia maambukizi ya virusi vya UKIMWI?
Uwezekano wa kuambukizwa virusi vya UKIMWI kwa kunyonyana ndimi ni mdogo sana.Kwa kubadilishana mate wakati wa kubusiana tu, haiwezekani maambukizo ya virusi vya UKIMWI kutokea. Lakini kama mmoja kati ya wapenzi ana vidonda au michubuko mdomoni, uwezekano wa kuambukizana huongezeka.
Je, nikinywa vidonge vya kuzuia mimba nitajikinga na UKIMWI?
Hapana. Vidonge vya kuzuia mimba vinazuia mwanamke kupata mimba, lakini siyo kinga ya UKIMWI. Ukijamiiana na mtu mwenye virusi vya UKIMWI unaweza kuambukizwa wakati wa kujamiiana kwa kupitia mwingiliano wa majimaji ya mwili, kama shahawa na majimaji ya ukeni.
Je, ni kweli kwamba mtu anaweza kufanya ngono na mtu mwenye VVU bila kupata maambukizo?
Ndiyo. Uwezekano ni kama ifuatavyo:
Endapo hali yake ya kinga asilia haijaharibika; na pia hana magonjwa ya ngono, michubuko, vidonda, n.k. hatari ni ndogo
Hatari ya kupata maambukizo ni kubwa zaidi mwanzoni mwa maambukizo na kipindi cha UKIMWI moto
Endapo kuna idadi ndogo sana ya virusi kwa muathirika, hatari ni ndogo.
Na kama ngono ilifanyika salama k.m. kondom ilitumika.
Je, ni mara ngapi mtu afanye ngono uzembe hadi apate VVU?
Hakuna idadi ya ngono uzembe ambayo ni salama, waweza kufanya ngono mara moja na kupata VVU, na mwingine akafanya ngono zaidi ya mara moja bila kupata VVU.
Je, ni njia zipi ambazo haziwezi kusababisha uambukizo wa virusi?
Kuna njia kadhaa ambazo hazienezi virusi vya UKIMWI. Nazo ni kama zifuatazo;
Kula chakula katika chombo kimoja na mtu mwenye UKIMWI
Kuchangia choo kimoja
Kulogwa
Kupiga chafya kwa mgonjwa mwenye UKIMWI
Kumbusu shavuni mtu mwenye virusi vya UKIMWI
Je, ukigusana na maiti mwenye VVU unaweza kupata uambukizo?
Endapo utagusana na majimaji yatokayo kwenye maiti yenye VVU uwezekano upo wa kupata uambukizo kama virusi vingali hai.
Kwa nini UKIMWI unawaathiri waafrika sana kuliko wazungu?
Hapa kuna mambo mawili ya kuzingatia:
Jamii ya kiafrika haijapokea kwa dhati na kuzingatia njia mbalimbali za kuzuia maambukizi ya VVU kama ilivyo kwa jamii ya kizungu.
Huduma bora za afya kwa waathirika kama dawa za kupunguza makali na dawa za kutibu magonjwa nyemelezi hupatikana zaidi kwa wazungu kuliko kwa waafrika.
Je, kama nina UKIMWI ni mabadiliko gani yatatokea mwilini mwangu?
Mabadiliko yanayoweza kutokea katika mwili wa mtu mwenye UKIMWI baada ya virusi kuangamiza walinzi (chembechembe hai nyeupe za damu) . UKIMWI MOTO na dalili zake ni kama zifuatazo:
Mwili kudhoofika na kupungua uzito kwa asilimia kumi (10%) au zaidi
Homa za kila mara
Kuharisha mfululizo kwa zaidi ya wiki nne
Vidonda sehemu za siri na mdomoni
Kuvimba tezi
Majipu mwili mzima
Saratani (kansa) ya ngozi
Utando mweupe mdomoni
Ukurutu
Ugonjwa wa ngozi, n.k
Je, mtu mwenye kuonekana na afya nzuri anaweza kuwa na virusi vya UKIMWI?
Ndiyo, mtu anayeonekana na afya nzuri anaweza kuwa na virusi vya UKIMWI. Katika hatua ya mwanzo baada ya kuambukizwa mtu anakuwa na virusi vya UKIMWI kwenye damu lakini haonyeshi dalili zozote za kuumwa.
Hatua hii inaweza kuchukua zaidi ya miaka 10! Hii ni hatari sana, kwa sababu kama unajamiiana na mtu mwenye kuonekana na afya nzuri, lakini ndani ya mwili tayari anavyo virusi vya UKIMWI, naweza kukuambukiza.
Siyo rahisi kumtambua mtu mwenye virusi vya UKIMWI, hasa akiwa katika hatua ya mwanzo baada ya kuambukizwa. Ni kwa njia ya kupima damu kliniki tu, unaweza kuwa na uhakika kama virusi anavyo au hajavipata. Kwa hiyo, kujamiiana bila kujikinga kwa kutumia kondomu i n a w e z e k a na kuhatarisha maisha yako, hata kama mpenzi wako ni mtu mwenye kuonekana na afya nzuri.
Je, ni kweli kwamba kujamiiana na bikra kunatibu UKIMWI?
Hapana! Si kweli kwamba unaweza ukapona VVU/UKIMWI kwa kujamiiana na bikra. Hadi sasa hakuna tiba ya maambukizi ya VUU. Ukweli ni kwamba kama umeathirika na VVU/UKIMWI na ukajamiiana na bikra bila kinga unahatarisha afya na maisha ya bikra huyo.
Je, vile vijidudu vya UKIMWI hukaa wapi katika mwili wa binadamu na mabadiliko gani yanatokea katika mwili ukishavipata?
Virusi hivi vinapatikana katika chembechembe nyeupe, kwenye majimaji ya mwili, hasa katika damu, shahawa, majimaji ukeni na maziwa ya mama anayenyonyesha. Chembechembe nyeupe za damu hupendwa na vijidudu vya UKIMWI kwa kujilisha na kuzaliana humo.Kwa hiyo, mara virusi vya UKIMWI vikiimgia mwilini, huzaliana na kuongezeka ndani ya chembechembe nyeupe za damu hatimaye chembe chembe hupasuka.Virusi huachiwa huru na kushambulia chembechembe nyingine nyeupe. Kadri chembechembe nyingine zinavyozidi kupasuka na kuachia virusi vya UKIMWI, idadi yake mwilini hupungua na mwili huanza kupungua nguvu.
Kuna tofauti gani kati ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI wenyewe?
Virusi vya UKIMWI kwa kifupi vinaitwa VVU.Virusi vya UKIMWI ni virusi vinavyoleta upungufu wa kinga mwilini(UKIMWI).UKIMWI kwa upande mwingine ni ugonjwa pale dalili zake zinapoanza kuonekana wazi.
Tofauti kati ya VVU na UKIMWI ni kwamba mtu mwenye virusi vya UKIMWI, bado anaweza kuwa mtu mwenye kuonekana na afya nzuri.Virusi vipo katika damu yake, lakini, havijaanza kuzishambulia chembechembe nyeupe. Kwa upande mwingine, mtu mwenye UKIMWI tayari mwili wake ni umepungua kinga na unashambuliwa na magonjwa mbalimbali na tayari ameanza kuugua ugonjwa huu.
Je, watu wote wenye virusi vya UKIMWI watapata UKIMWI?
Ndiyo, baada ya muda fulani kila mtu mwenye virusi vya UKIMWI ataanza kuugua UKIMWI. Lakini muda kati ya kuambukizwa Virusi na kuanza kuugua unatofautiana.Wengine wanaishi muda mrefu zaidi. Kwa wastani watu wazee wazima wanaishi kwa miaka 10 kabla ya kupata dalili za awali. Watoto wanaopata virusi kabla ya umri wa miaka mitano na kwa wastani waendelea kiishi mwaka mmoja hadi mitatu.
Hakuna jibu la ujumla la ni miaka mingapi ataishi tena mtu aliyeambukizwa virusi vya UKIMWI. Idadi ya miaka ya kuishi baada ya kuambukizwa inategemea vitu vingi, kama kinga asilia inayo mkinga mtu, hali ya lishe mwilini, idadi ya virusi vilivyoingia mwilini, kujikinga na kutibu mapema na kwa ukamilifu maradhi mengine mara tu yanapojitokeza.
Je, mtu mwenye kuonekana na afya nzuri, anaweza kuwa na virusi vya UKIMWI?
Ndiyo, mtu anayeonekana na afya nzuri anaweza kuwa na virusi vya UKIMWI. Katika hatua ya mwanzo baada ya kuambukizwa mtu anaweza kuwa na virusi vya UKIMWI kwenye damu lakini haonyeshi dalili zozote za kuumwa. Hatua hii inaweza kuchukua zaidi ya miaka 10, hii ni hatari sana kwa sababu kama unajamiiana na mtu mwenye kuonekana na afya nzuri, lakini ndani ya mwili tayari anavyo virusi vya UKIMWI, anaweza kukuambukiza.
Siyo rahisi kumtambua mtu mwenye virusi vya UKIMWI, hasa akiwa katika hatua ya mwanzo ya baada ya kuambukizwa. Ni kwa njia ya kupima damu kwenye kliniki tu,unaweza kuwa na uhakika kama ameshaambukizwa au la. Kwa hiyo kujamiiana bila kujikinga kwa kutumia kondomu inawezekana kuhatarisha maisha yako, hata kama mpenzi wako ni mtu mwenye kuonekana na afya nzuri.
Je, dalili za kuugua UKIMWI ni zipi?
Baada ya virusi vya UKIMWI kuangamiza walinzi wa mwili, yaani chembe chembe hai nyeupe za damu, uwezo wa mwili kupambana na magonjwa hupungua. Ina maana kwamba magonjwa mengine yanaweza kuushambulia na mwili kutoweza kujilinda.
Mara nyingi mtu anapungua sana uzito, anapatwa na homa za mara kwa mara, anaweza kuharisha mfululizo au anaweza kuwa na vidonda sehemu za siri au midomoni. Lakini ukipata dalili moja kati ya hizi, usiamue mara moja kwamba umepata UKIMWI.Yapo magonjwa mengi yanayoonyesha dalili sawa sawa na hizi. Unashauriwa kumwona daktari ambaye atakupa ufafanuzi wa kitaalamu.
Je, ni tabia zipi zinazochangia kuenea kwa virusi vya UKIMWI?
Virusi vya UKIMWI kwa kiasi kikubwa vinaenea kwa njia ya kujamiiana. Mtu akiwa na wapenzi wengi, uwezekano wa kuambukizwa unaongezeka, kwasababu kila mpenzi anaweza kuwa chanzo cha kupata virusi.Vilevile mtu akifanya mapenzi yasiyo salama, yaani kuingiliana kimwili (ukeni au sehemu ya haja kubwa) bila kutumia kondomu anahatarisha masiha yake.
Pia kuchelewa kutibu magonjwa mengine ya zinaa, kunachangia kuenea kwa virusi vya UKIMWI. Kwa mfano kama mtu anaugua ugonjwa wa zinaa, vijidudu vya UKIMWI vinaweza kuingia mwilini kwa urahisi zaidi kwa sababu ya vidonda sehemu zake za siri.
Matumizi ya madawa ya kulevya pamoja na pombe yanaweza kuchangia kufanya maamuzi yasiyo sahihi katika matendo ya ngono.
Je, mwanaume akitoa uume nje ya uke kabla ya kumwaga shahawa anaweza kuambukizwa UKIMWI na anaweza kumwambukiza mwenzie?
Ndiyo, hata akitoa uume nje ya uke kabla ya kumwaga shahawa anaweza kumwambukiza UKIMWI mwenzie. Ni hatari kwa mwanamke na pia kwa mwanaume, kwa sababu vijidudu vimo ndani ya majimaji ukeni na uumeni. Hasa kama mmoja ana vidonda au michubuko midogo sehemu za siri, UKIMWI unaenea kwa urahisi.
Kutoa uume nje ya uke kabla ya kumwaga shahawa siyo njia salama ya kujikinga na UKIMWI.
Je, nikijamiiana na mtu mwenye UKIMWI bila kutumia kondomu, nitapata UKIMWI?
Uwezekano wa kuambukizwa VVU ukijamiiana na mtu mwenye virusi vya UKIMWI bila kutumia kondomu ni mkubwa sana. Kwa sababu kujamiiana ni mahusiano ya kimwili kwa karibu, ni hatari sana kujamiiana na mtu mwenye virusi vya UKIMWI bila kutumia kondomu.
Mpaka leo, kondomu ni njia pekee ya kuzuia kuambukizwa VVU wakati wa kujamiiana. Kama kondomu inatumiwa sawasawa na kila unapojamiiana na mtu mwenye virusi vya UKIMWI, uwezekano wa kuambukizwa ni mdogo sana. Kutumia kondomu sawasawa ina maana kutumia kondomu mpya, kuiweka vizuri uumeni na kuitoa kabla ya uume kulegea.
Je, nikijamiiana kwa njia ya sehemu ya haja kubwa au mdomoni na mtu mwenye virusi vya UKIMWI, nitaambukizwa virusi hivyo?
Ndiyo, kuna hatari kubwa ya kuambukizwa UKIMWI wakati wa kujamiiana kwa njia ya haja kubwa au mdomoni na mwenye virusi vya UKIMWI.
Ngozi ya ndani ya haja kubwa ni laini sana na uwezekano wa kupata michubuko wakati wa kujamiiana ni mkubwa, kwa sababu hakuna majimaji kama ukeni yanayorahisisha uume kuingia. Kwa virusi vya UKIMWI ni rahisi sana kuingia mwilini mwa mwanamke kupitia kwenye michubuko.Vile vile mwanaume anaweza kuambukizwa kama damu kutoka kwenye michubuko ya mwanamke inagusana na mwili wake. Kwa hiyo ni hatari kwa wote wawili kuambukizana. Watu wote wanashauriwa kutotumia njia hizi za kujamiiana, ila watumie kondomu kwa kuzuia kuambukizwa magonjwa ya zinaa, pamoja na UKIMWI.
Je, nitaweza kupata virusi vya UKIMWI nikijamiiana na msichana au mvulana wa umri mdogo?
Ndiyo, utaweza kuvipata virusi vya UKIMWI.Uwezekano wa kuambukizwa hautegemei umri wa mpenzi wako lakini, unategemea afya yake. Kama huyu msichana au mvulana tayari ameshapata virusi vya UKIMWI na unajamiiana naye utaweza kuambukizwa.
Mara nyingi huwezi kufahamu kama mtu ana virusi vya UKIMWI au hapana, kwasababu katika hatua ya mwanzo baada ya kuambukizwa hakuna dalili zozote za kuugua. Vile vile ni tabia mbaya sana kushawishi wasichana na wavulana wadogo kujamiiana. Kwa usalama na faida ya wote, mnashauriwa kuacha mapenzi na wasichana au wavulana wadogo.
Je, mapenzi salama ni yapi?
Mapenzi salama ni yale yanayofanyika bila ya wasiwasi wa kupata mimba zisizotarajiwa, magonjwa ya zinaa na UKIMWI. Mapenzi salama yanaweza kuwa ni vitendo vya kumaliza hamu za kimapenzi bila sehemu za siri za mwanamke na mwanaume kukutana. Au kama sehemu hizo zinazokutana basi tahadhari inachukuliwa wakati wa kuingiliana kimwili.
Vitendo vya kumaliza hamu bila kujamiiana ni kupiga busu, kukumbatiana, kunyonyana ndimi, kushikana mikono na kupiga punyeto. Matendo haya yote ni salama kabisa kuhusiana na mimba zisizotarajiwa, magonjwa yanayotokana na kujamiiana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Ili kuhakikisha mnafanya mapenzi salama wakati mnahusisha mwingiliano kati ya uume na uke, lazima mchukue tahadhari.Tahadhari mojawapo ni uaminifu katika mapenzi, lakini inabidi muwe na uhakika kwamba wote wawili hamjaambukizwa magonjwa wakati mnapojamiiana kwa mara ya kwanza. Tahadhari nyingine ni kutumia kondom. Kondom inazuia mimba pamoja na magonjwa ya ngono.
Je, ni kweli kwamba ukubwa wa kondom haufai kwa wanaume wote?
Duniani kuna kondom za ukubwa mbalimbali.Kwa wastani ukubwa wa kondom unafaa kwa wanaume, watu wazima karibu wote. Mara chache sana kondom ni ndogo kwa wanaume fulani, lakini wakati mwingine wanaume wanaringa tu wakidai kuwa kondom haziwatoshi kwa kuwa wana uume mkubwa. Wengine hutoa kisingizio hicho kwa sababu hawataki kutumia kondom.
Kwa upande wa vijana hali ni tofauti. Mara nyingi kondom ni kubwa sana ukilinganisha na ukubwa wa uume wao. Hapa Tanzania kondom ndogo zaidi kuliko wastani hazipatikani. Kwa vijana pamoja na kuwa na uume mdogo, ni vizuri zaidi wangeacha kujamiiana na badala yake watumie njia nyingine za kumaliza hamu ya kutaka kujamiiana kama vile kukumbatiana na kubusiana.
Kwa nini kondom itumike mara moja tu?
Kondom inapaswa itumike mara moja tu kwa kila mshindo wakati wa kujamiiana, kwa sababu ikitumika mara mbili au tatu uhakika wa kuzuia mimba wala uambukizo wa magonjwa ya zinaa utatoweka. Kondom isifuliwe bali mara baada ya kutumika itupwe kwenye choo cha shimo au ichomwe moto. Kondom zimetengenezwa kwa kutumiwa mara moja tu.
Kwanini mara nyingine kondom hupasuka wakati wa kujamiiana?
Kupasuka kwa kondom mara nyingi kunasababishwa na kondom kutowekwa vizuri uumeni. Ni muhimu sana kutoa hewa ndani ya kondom wakati wa kuivalisha uumeni. Kwa sababu ile hewa uumeni inaweza kusababisha kondom kupasuka wakati wa kujamiiana.
Vilevile sio vizuri kupaka mafuta kama vaselini juu ya kondom ili kurahisisha kitendo cha kujamiiana. Mafuta kama vaselini yanadhoofisha uimara wa kondom na yanarahisisha kondom kupasuka. Mafuta yanayowekwa kwenye kondom yanahifadhi uimara wa kondom na ni aina maalumu ya mafuta.
Ni muhimu kukumbuka kwamba mwanaume akivaa kondom vizuri, uwezekano wa kondom kupasuka ni mdogo sana.
Je, mbegu za kiume zinaweza kupita kwenye kondomu?
Hapana, mbegu haziwezi kupita kwenye kondom. Kondom zimetengezwa ili kuzuia mbegu za kiume kufikia ukeni wakati wa kujamiiana. Kwa sababu shahawa haziwezi kupita kwenye kondom. Kondom ni njia nzuri ya kuzuia mimba, maambukizo ya magonjwa ya zinaa pamoja na UKIMWI.
Watu wengine wanasema kwamba kuna mashimo madogo kwenye kondom yanayorahisisha mbegu pamoja na vijidudu vya magonjwa ya zinaa kupita. Huu ni uongo. Ukitaka kuwa na uhakika kwamba kondom mpya haina mashimo, chukua kondom moja ijaze maji. Hayatavuja kabisa. Baada ya kujaribisha itupe kondom ndani ya choo cha shimo au ichome moto, lakini usiitumie wakati wa kujamiana!
Je, hayo mafuta kwenye kondom ni ya nini? Yana madhara yoyote?
Mafuta yanayowekwa kwenye pakiti ya kondom ni mafuta maalum na yana kazi ya kuhifadhi kondomu mpaka siku yake ya kutumika. Bila mafuta haya kondom isingekuwa imara, ingekauka na isingekuwa nyumbufu vya kutoshaVilevile mafuta haya yanalainisha mpira ili kurahisisha uvaaji na matumizi yake. Kwa watu wengi mafuta haya hayawaletei matatizo yoyote. Watu wachache sana ambao ngozi zao ni nyepesi kuathirika wanapata matatizo ya kuwashwa na ngozi baada ya kutumia kondom. Muwasho huo sio wa kudumu. Watu wa namna hii wanashauriwa kunawa na sabuni ya kawaida baada ya kujamiiana.
Kuna uvumi kwamba mafuta yaliyomo ndani ya pakiti ya kondom yana vrusi vya UKIMWI. Hii siyo kweli kabisa, mafuta hayo yanawekwa kwa ajili ya kuhakikisha uimara wa kondom tu.
Je, mwanamke anajisikiaje akijamiiana mwanaume aliyevaa kondom au aliye peku?
Hatuwezi kusema mwanamke husikia raha gani akijamiiana na mwanaume aliyevaa kondom au na mwanaume asiyevaa kondom. Kila mtu ana upendeleo wake, lakini jambo la msingi katika kujamiiana ni hisia, hali ya kuelewana katika mapenzi na kiwango cha msisimko. Wanawake wengine wanapendelea kujamiiana na mwanaume aliyevaa kondom kwa sababu hofu ya kupata mimba au kuambukizwa magonjwa ya zinaa haipo. Wanawake wengine wanapendelea kujamiiana bila kondom. Lakini, pamoja na hatari ya kupata mimba, siku hizi kujamiiana bila kondom kuna hatari ya kuambukizana magonjwa ya zinaa na UKIMWI. Kwa hiyo ni vizuri zaidi kutomwamini mtu yeyote mpaka mpimwe kliniki wote wawili kuwa ni wazima wa afya.
Je, nikitumia kondom kila mara ninapojamiiana sitaaambukizwa magonjwa ya zinaa?
Vijidudu vya magonjwa haya vipo ndani ya shahawa.Hivyo ukitumia kondom kila unapojamiiana, siyo rahisi kupata magonjwa ya zinaa, kwa sababu shahawa haipiti kwenye kondom.Kwa hiyo ukitumia kondom kwa njia sahihi, usalama upo.
Nifanyeje kujiepusha na vishawishi vya mpenzi wangu vinavyoweza kunifanya nisitumie kondom?
Mara nyingine siyo rahisi kujiepusha na vishawishi vya kujamiiana bila kutumia kondom kutokana na msukumo wa mpenzi wako. Lakini kumbuka kwamba siyo rahisi kutambua mwenye magonjwa ya zinaa na mara nyingi huwezi kujua kama mpenzi wako hana ugonjwa wowote wa zinaa au hata virusi vya UKIMWI. Huwezi kufahamu ni watu wangapi ameshajamiiana nao maishani mwake na mpenzi wako vilevile hawezi kufahamu kama wewe umeshajamiiana na mtu mwingine. Kila unapojamiiana kuna uwezekano wa kuambukizwa magonjwa ya zinaa. Kwa hiyo jadiliana na mpenzi wako na mkubaliane juu ya umuhimu wa kutumia kondomu wakati wa kujamiiana kwa nia ya kuwakinga wote wawili. Kama mpenzi wako anakuambia kwamba hana ugonjwa kama huo, mwambie kwamba hana uhakika wa kufahamu kutokuwa na virusi vya UKIMWI bila kupimwa damu. Na kama mmoja kati yenu hajapimwa, basi uwezekano wa kuwa na virusi upo. Usikubali kushawishiwa kutotumia kondom, kwa sababu unaweza kuhatarisha maisha yako.
Je, ni kweli matumizi ya madawa ya kulevya huchangia maambukizi ya VVU na magonjwa mengineyo ya zinaa?
Madawa ya kulevya yenyewe hayasababishi UKIMWI na magonjwa ya zinaa. Lakini utumiaji wa madawa ya kulevya hurahisisha kupata na kuenea kwa magonjwa haya. Madawa haya hudhoofisha mwili na kinga ya mwili. Hivyo basi hurahisisha virusi vya magonjwa kuingia mwilini mwa mtumiaji kiurahisi.
Matumizi ya madawa ya kulevya huwafanya watumiaji kusahau hatari za kuwa na wapenzi wengi pamoja na kufanya mapenzi na watu wasiowafahamu hali za afya zao. Hujisahau kufanya mapenzi salama kwa kutumia kondom. Vilevile husahau majukumu yao kama vile kwa mke, watoto na familia nzima kwa ujumla.
Madawa ya kulevya yanayoingia mwilini kwa njia ya sindano husababisha uwezekano mkubwa wa kuenea kwa virusi vya UKIMWI (VVU) kwa watumiaji pindi wanapochangia sindano kujidungia madawa hayo mwilini. Pia madawa ya kulevya huchangia kuenea kwa virusi vya UKIMWI kwa kuwa watumiaji hujiingiza katika biashara ya ngono ili kuweza fedha za kununulia madawa hayo.
Kwa nini watu wanaotumia madawa ya kulevya hukonda?
Madawa ya kulevya huharibu ufanyaji kazi wa kawaida wa mfumo wa mwili hasa tumbo na utumbo wa watumiaji hushindwa kufyonza virutubisho vidogo vidogo kama vile vitamini, madini kutoka kwenye chakula na kwenda kwenye mfumo wa damu. Hiki ndicho kinachowafanya wakonde. Isitoshe, hupunguza uwezo wa mwili kujikinga na maradhi na hivyo huuweka mwili katika hatari ya kuambukizwa na magonjwa likiwemo gonjwa hatari la UKIMWI.
Kondomu ni nini?
Kondomu ni kifuko kilichotengenezwa
na mpira laini
ambacho hutumiwa wakati
wa kufanya ngono. Huvishwa kwenye
uume uliosimama hivyo manii yanavyotoka
kwenye uume huo wakati mwanaume
anapofikia mshindo huzuiwa
humo. Kondomu hutumika kama njia
ya kuzuia ujauzito na pia hutumika kuzuia
maambukizi yakiwemo ya VVU
(virusi vinavyosababisha UKIMWI),
kwa sababu huzuia uke usipate majimaji
yatokayo kwa mwanaume na pia huzuia
uume usipate majimaji ya mwanamke.
Kondomu zimetengenezwa kwa mpira
unaonyambulika kirahisi kutosha karibu
kila uume. Pia zipo kondomu za kike
ambazo huingizwa kwenye uke kabla
ya kufanya ngono.
Kondomu zilivumbuliwa lini?
Kondomu za kwanza zilitumika
miaka elfu kadhaa iliyopita.
Ushahidi unaonyesha kuwa
hata wakati wa Wamisri kondomu zilikuwepo.
Yapata miaka 3000 iliyopita walikuwa
wakitumia kifuko cha kitambaa
kujikinga na magonjwa yanayoambukiza
kwa ngono. Picha zinazoonekana katika
michoro ya mapango ya miaka ya 2000
iliyopita huko Ufaransa zinaonyesha
kuwa kondomu zilikuwa zikitumiwa
katika eneo hilo. Kondomu zilizokuwa
zikitumiwa nyakati hizo zilikuwa zimetengenezwa
kwa vitu visivyokuwa vya
kawaida kama vile mafuta ya hariri, karatasi,
vibofu vya samaki au magamba
ya kobe. Baadaye, kondomu zilitengenezwa
kwa kifuko na kufungwa kwa
utepe.
Je ni kweli kwamba duniani kote watu hutumia kondomu?
Kuna mamilioni ya watu dunianiwanaotumia kondomu. Inakadiriwa kuwa kati ya kondomu bilioni 6 na 9 husambazwa kila mwaka duniani. Watu wa umri tofauti, walio na wasio na ndoa wanatumia kondomu kwa ajili ya kupanga uzazi. Kimsingi kondomu hutumika kwa sababu kuu mbili: kujikinga dhidi ya mimba zisizotakiwa na kujikinga dhidi ya magonjwa yaambukizwayo kwa ngono ukiwemo VVU/UKIMWI.
Watu wangapi hutumia kondomu?
Duniani, matumizi ya kondomu hutofautiana sana kutoka eneo moja hadi lingine na kutoka nchi moja kwenda nyingine. Inakadiriwa kuwa asilimia tano ya wanawake walioolewa na walio katika umri wa kuweza kuzaa wanatumia kondomu. Nchini Botswana, asilimia 11 ya watu wote wenye ndoa hutumia kondomu kwa ajili ya uzazi wa mpango, wakati Korea Kusini ni asilimia 15 na Singapore ni asilimia 22. Nchini Tanzania ni asilimia 2.7 tu ya wenye ndoa ambao huzitumia. Kiwango cha matumizi ya kondomu kwa uhusiano usiyo wa ndoa ni kikubwa zaidi. Kwa mfano, nchini
Mexico asilimia 63 hutumia kondomu, wakati Paraguay ni asilimia 79. Theluthi
mbili ya vijana wa Ujerumani hutumia kondomu wakifanya ngono kwa mara ya kwanza. Tanzania ni asilimia 22 tu ya vijana waliosema kuwa walitumia kondomu wakifanya ngono kwa mara yao ya kwanza. Japan ina kiwango kikubwa zaidi cha matumizi ya kondomu. Wajapani wana historia ndefu ya matumizi ya
kondomu. Hivi sasa, kondomu inakubalika sana nchini Japan na kuna unyanyapaa kidogo dhidi ya kifaa hicho. Karibu nusu ya wanandoa wote hutumia kondomu, na asilimia 78 ya wanaopanga uzazi wa mpango huchagua kondomu kama njia yao pendwa ya uzazi wa mpango. Nchini Uholanzi, vijana wanaofikia balehe
hupata taarifa mbalimbali na elimu ya ujinsia na uhusiano wakiwa bado na
umri mdogo. Matokeo yake ni kwamba kwa mwaka 2000, asilimia 68 ya vijana
walioanza ngono walitumia kondomu kila tendo la ngono, wakati asilimia 27
walitumia kondomu na vidonge. Matumizi ya kondomu katika kujikinga
na maambukizi ya VVU yanategemea sana msukumo wa kisiasa na upatikanaji wa habari unaochangia mabadiliko ya tabia. Kwa mfano, mwaka 1990 VVU/
UKIMWI ulipewa kipaumbele nchini Thailand. Wizara ya Habari ilizindua
kampeni kubwa ya kuhamasisha matumizi ya kondomu. Kampeni ya “Mpango
wa kondomu 100%” ilifanya kuwa kondomu ni lazima kwa machangudoa
na wateja wao. Mpango huo ulikuwa na msukumo kutoka serikalini, watumishi
wa afya, Asasi zisizo za Kiserikali (NGOs), vyombo vya habari, wenye
madanguro na umma wote kwa ujumla. Matokeo yake matumizi ya kondomu
kwenye madanguro yalipanda kutoka asilimia 14 mwaka 1988 hadi kufikia 95
mwaka 1995, na maambukizi mapya ya VVU yalikadiriwa kushuka kwa zaidi ya
asilimia 80 mwaka 2002.
Je, ni kweli kwamba kondomu nyingine ni kubwa kwa wengine wakati wengine kwao ni ndogo?
Kwa kawaida kondomu hutosha wanaume wote, kwa sababu imetengenezwa kwa mpira unaonyumbulika kulingana na ukubwa wa uume. Hata hivyo, kuna saizi tofauti za kondomu. Kwa wastani
saizi moja ya kondomu inatosha wanaume wote wazima na waliobalehe. Ni mara chache sana utakuta kondomu zilizo ndogo au kubwa sana kwa wanaume wengine. Waliofikia balehe ambao pia uume wao ni mdogo kutumia kondomu, wanashauriwa kutoingiliana kimwili na badala yake watumie njia nyingine kuonyesha hisia zao za kingono, kama vile kukumbatiana na kupigana mabusu. Saizi moja inatosha wote.
Je, kuna tofauti ya matumizi ya kondomu kwa mwanaume aliyetahiriwa na yule asiyetahiriwa?
Hakuna tofauti kubwa ya matumizi ya kondomu kati ya mwanaume aliyetahiriwa na asiyetahiriwa. Isipokuwa, mwanaume ambaye hajatahiriwa hushauriwa kuvuta nyuma govi kabla ya kuvaa kondomu. Kondomu hupunguza msuguano wa govi hilo wakati wa ngono, hali ambayo baadhi ya wanaume ambao hawajatahiriwa huona kwamba hilo huwapunguzia raha wakati wa ngono. Kwa upande mwingine wanaume wengine wanafurahia kwamba kondomu huwaongezea muda wa uume wao kubaki umesimama.