Friday, June 7, 2013

Kim: Natarajia ushindi kesho

 
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Kim Poulsen amesema anatarajia kupata matokeo mazuri katika mechi dhidi ya Morocco itakayochezwa kesho mjini Marrakech.

Stars itavaana na miamba hiyo ya soka kutoka Kaskazini mwa Afrika, katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia itakayofanyika Brazil mwakani.

Akizungumza kwa simu kutoka Marrakech jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema wachezaji wote wako katika hali nzuri na kocha Kim anawahimiza kupata ushindi katika mechi ya kesho.

“Wachezaji wote wako vizuri, hata Erasto Nyoni ambaye hakucheza kwenye mechi ya kujipima nguvu na Sudan kule Addis Ababa, yuko vizuri na kocha anatarajia kumpanga kwenye kikosi cha kwanza katika mechi ya Jumamosi (kesho),” alisema Wambura akimkariri Kim.

Alisema kocha Kim amekuwa akiwahimiza mara kwa mara wachezaji kukumbuka usemi wao kwamba wawafunge Morocco mara mbili, nyumbani na ugenini.

“Leo (jana) timu haitafanya mazoezi kesho (leo) ndio itakuwa na mazoezi mepesi kabla ya mechi Jumamosi,” alisema Wambura na kusisitiza kuwa timu ipo katika hali ya ushindi.

Stars ilianza safari ya Marrakech wiki iliyopita ambako ilikwenda Addis Ababa nchini Ethiopia ambako iliweka kambi kwa zaidi ya wiki moja na kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan.

Mechi hiyo iliyochezwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Addis Ababa, timu hizo hazikufungana. Stars iko kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele katika kuwania kufuzu fainali hizo kwani ina pointi sita nyuma ya Ivory Coast katika Kundi la C. Ivory Coast ina pointi saba.

Morocco ina pointi mbili, wakati Gambia ina pointi moja, zote zikiwa zimeshuka dimbani mara tatu.

Endapo Stars itamaliza ya kwanza kwenye kundi hilo, itaungana na washindi wa makundi mengine na kuwa timu 10, ambazo zitapangwa timu mbili kukutana katika mechi ya nyumbani na ugenini na washindi kwa mechi hizo tano, ndio watakuwa wawakilishi wa Afrika katika fainali za Brazil mwakani.