Mkazi wa kijiji cha Litou wilaya ya Liwale Nuru Mohamedi Kipeleka (34),amejifungua kichakani baada ya zahanati kufungwa kutokana na wahudumu wa zahanati hiyo kuteuliwa kuwa makarahani wa sensa.
Tukio hilo lilitokea jana wakati Kipeleka alipopatwa uchungu na familia yake kuchukua uamuzi wa kumpeleka kwenye zahanati ya kijiji ya Kiangara.
Akizungumza na gazeti hili baba wa binti huyo Mohamedi Kipeleka, alisema sababu zilizopelekea mtoto wake kujifungua njiani, ni kukosekana kwa mganga kwenye kwenye zahanati hiyo baada ya wahudumu wa afya kuteuliwa kuwa makarani wa sensa.
Kipeleka alisema baada ya kufika kwenye zahanati hiyo alikuta imefungwa , na alipouliza wakazi wa maeneo hayo aliambiwa waganga wamekwenda kwenye zoezi la sensa mtaani.
Alisema baada ya kukuta zahanati imefungwa walilazimika kurudi nyumbani ndipo mwanae alipopatwa na uchungu na kujifungulia kichakani.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa kijiji hicho aliyefahamika kwa jina la Mtepeka alikanusha kuwepo kwa tatizo hilo, na kwamba zahanati iko wazi na inawahudumu ambao ni, Abasi Makanga,Abdallaa Likiwa na Aberamani Kenyu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Sensa wilaya ya Liwale Alfredy Mmbaga, alikanusha kusikia tukio hilo, na kuongeza kwamba hajui kama kuna vituo vya afya na zahanati vilivyofungwa kwa sababu ya waganga wake kuteuliwa kuwa makarani wa sensa wilayani humo.
“Taarifa hii ni mpya kwangu kwani ndiyo kwanza naipata kwako, hivyo siwezi kuzungumza chochote” Alisema Mmbaga.