Mkufunzi wa masuala ya Uzazi wa Mpango kutoka kampuni ya T-Marc, Grace Dibibi akielekeza jambo kuhusu njia bora za uzazi wa mpango kwa wafanyakazi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), (hawapo pichani) katika ofisi zao zilizopo eneo la Tazara, Dar es Salaam jana.
WANAWAKE nchini wamehadharishwa juu ya matumizi ya dawa za kujichubua, kwani husababisha madhara yakiwamo ya kukoma kwa hedhi kabla ya umri.
Dawa hizo za mkorogo, zinaweza kusababisha kukoma hedhi kwa mwanamke mwenye umri wa hata miaka 30 hadi 35, tofauti na kawaida ya miaka 45.
Hayo yalibainishwa jana na mkufunzi wa taasisi isiyo ya Serikali ya T- MARC, Grace Dibibi alipowasilisha mada kuhusu Uzazi wa Mpango kwa wafanyakazi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Dar es Salaam jana.
Pia alihadharisha wanawake juu ya tabia ya kusafishwa vizazi mara kwa mara, kwani nayo husababisha kutojijenga ukuta ndani ya viungo vya uzazi na hivyo kushindwa kushika ujauzito.
Dibibi alisema wanawake wanatakiwa kuwa makini ili kupanga uzazi na kuzaa kwa muda wanaotaka, huku akisisitiza kuwa dawa za uzazi wa mpango ni salama, bali zenye vichocheo zinazoweza kusababisha madhara kwa baadhi ya wanawake.
Kuhusu suala la wanawake kuchelewa kuzaa baada ya kutumia njia za uzazi wa mpango, alishauri kuonana na madaktari wanawake na kuwaelezea historia ya familia kabla ya kutumia njia hizo.
“Kuna watu kwenye familia huzaa mtoto mmoja, lakini wanapozaa tu huanza njia za uzazi wa mpango bila ushauri wa wataalamu,” alieleza mkufunzi huyo.
Alisema njia hizo zote za uzazi wa mpango, hutumiwa isipokuwa ya kufunga uzazi, kwani takwimu zilizopo zinaonesha kuwa ni wanaume watatu tu nchini ndio walifungwa uzazi na wote wanatamani kurudishiwa.
Alisema kwa wanawake ni asilimia 20 ndio waliofunga, hasa wasomi, lakini akasema hajui sababu ya wasomi kupenda njia hiyo.
Mhamasishaji wa taasisi hiyo, Shani Pius alisema wanawake wengi hawapendi kutumia kondomu za kike kwa madai kuwa zina hatua nyingi za kufuata wakati wa kuzivaa kutokana na umbo lake, jambo ambalo linakera wapenzi wao.
Alisema mara nyingi kondomu hizo hutumiwa na wanawake wanaofanya biashara ya mapenzi ili kujikinga pale wanaume wanapokuwa wabishi, lakini si kwa wapenzi wa kawaida.