Wednesday, September 5, 2012
Mamia wamzika mwandishi aliyeuawa
MWENYEKITI wa Klabu ya Waandishi wa Habari ya Mkoa wa Iringa (IPC), Daudi Mwangosi aliyeuawa kwa kupigwa kwa bomu la machozi, amezikwa jana saa 7.30 mchana kijijini kwake Busoka wilayani Rungwe, mkoani Mbeya.
Wakati maziko hayo yakifanyika, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alisema ameunda tume huru kuchunguza mauaji ya Mwangosi, ambaye pia alikuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten.
Tume hiyo itakayoongozwa na Jaji mstaafu Stephen Ihema, ina wajumbe wengine wanne wakiwemo wanahabari Pili Mtambalike kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Theophil Makunga kutoka Jukwaa la Wahariri (TEF).
Mbali na wanahabari hao, wengine ni Naibu Kamishna Isaya Mungulu kutoka makao makuu ya Polisi na Kanali Wema Wapo kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Akieleza kuundwa kwa tume hiyo, Nchimbi alisema ameiagiza ije na taarifa ambayo itaaminiwa na wananchi ndio maana ameteua wajumbe kutoka TEF, MCT na wataalamu wa mabomu kutoka ndani ya JWTZ na iongozwe na Jaji.
Hadidu za rejea Dk Nchimbi alisema tume hiyo inatakiwa kujibu maswali sita ambayo hayajapata majibu.
Alitaja maswali hayo kuwa ni nini chanzo cha mauaji ya Mwangosi, na kama kuna ukweli kuwa kuna uhasama kati ya polisi wa Iringa na waandishi wa habari wa mkoani humo.
Swali la tatu ambalo Nchimbi alisema tume hiyo inatakiwa kuja na jibu ni kama kweli kuna waandishi watatu wa mkoani Iringa ambao wako kwenye orodha ya kuuawa na polisi hao na swali la tano ni kama nguvu iliyotumiwa na polisi Nyololo, alikouawa Mwangosi, ilikuwa sahihi.
Waziri huyo alisema swali lingine ni kama kuna utaratibu kwa vyama vya siasa kukata rufaa kama haviridhiki na uamuzi wa Polisi na kama kuna uhusiano mbaya kati ya polisi na baadhi ya vyama vya siasa hapa nchini.
Alisema tume hiyo inatakiwa impe majibu ndani ya siku 30 na iwapo watahitaji msaada wa kitaalamu kutoka nje ya nchi, Serikali iko tayari kuagiza wataalamu hao, ili waisaidie ili mradi tu wapate majibu yenye kuridhisha.
Alipoulizwa kama yuko tayari kumsimamisha Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda ili kupisha uchunguzi huo, Dk Nchimbi alisema ndani ya tume hiyo kuna Naibu Kamishna wa Polisi; hivyo kamanda huyo ambaye cheo chake ni Kamishna Msaidizi hana ubavu wa kuharibu uchunguzi huo.
Kuhusu askari aliyempiga bomu Mwangosi kama anashikiliwa na polisi au bado yuko nje, Dk Nchimbi alisema atachukua hatua mara baada ya tume hiyo au ile ya Polisi, iliyoundwa na Mkuu wa Polisi, IGP Said Mwema kukamilisha uchunguzi wake.
Tume ya Mwema inaongozwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba. Aidha, Dk Nchimbi alisema hakuna kitu cha kusherehekea wala kushabikia wakati aliyeuawa ni binadamu.
“Ripoti mojawapo ikitoka kati ya tume hizo mbili, hatua zitaanza kutekelezwa kwani zitakuwa na baadhi ya majibu ya maswali haya,” alisema Nchimbi. Dk Nchimbi kujiuzulu?
Kuhusu kama atajiuzulu iwapo ripoti itabaini kuwa polisi ndio waliofanya mauaji hayo, Dk Nchimbi alisema “Nikijiuzulu mtampata wapi waziri kama mimi? (kicheko) Shauri yenu…lakini nawahakikishieni kuwa ukweli utaanikwa wazi.”
Akijibu swali kwamba polisi wanatumiwa kukikandamiza Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kwa manufaa ya CCM, Dk Nchimbi alisema hataruhusu hali ya namna hiyo na akasisitiza kuwa polisi wamekuwa wanatekeleza agizo la Msajili wa Vyama vya Siasa la kupiga marufuku mikutano ya kisiasa katika kipindi hiki cha Sensa ya Watu na Makazi.
Alipotolewa mifano ya namna ambavyo wanachama wa CCM wamekuwa wakifanya mikutano yake bila kuingiliwa na Polisi, Dk Nchimbi alisema alipata taarifa hizo na akamjulisha Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama ambaye alimhakikishia kuwa hakuna mkutano wa hadhara unaofanywa na chama chake badala yake wanafanya vikao vya ndani.
“Mikutano ya ndani haikupigwa marufuku, kilichokatazwa ni mikutano ya hadhara na ninaomba wenzetu wawe wastahimilivu kwani zimebaki siku nne tu za sensa,” alisema Dk Nchimbi.
Vitisho vya mauaji Katika mazungumzo yake pia, Dk Nchimbi alimlaumu Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kuwa ni mmoja wa watu waliosababisha mauaji hayo kwani Septemba mosi, siku moja kabla ya mauaji hayo, alimwandikia IGP ujumbe unaoonesha kuwa walidhamiria kufanya vurugu.
Alinukuu ujumbe huo unaodaiwa kuandikwa na Dk Slaa; “IGP nasubiri simu yako, wajulishe polisi wako waandae risasi za kutosha na mabomu ya kutosha. Mtakuwa na karamu ya mauaji na kisha mtasherehekea, mjiandae kwenda Mahakama ya The Hague. Ni afadhali tufe kuliko manyanyaso haya, Dk Slaa.”
Waziri huyo alisema anamshangaa IGP Mwema kwa nini polisi hawajamkamata Dk Slaa na kumhoji kwani ujumbe wake aliotuma unaashiria kutaka kuanzisha vurugu kama ilivyotokea huko Nyololo.
Maziko ya Mwangosi Mamia ya wakazi wa kijiji hicho, wanasiasa wa CCM na Chadema na waandishi wa habari kutoka mikoa ya Iringa na Mbeya walishiriki katika maziko hayo yaliyoratibiwa na waandishi wa habari.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais asiye na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya na Dk Slaa walishiriki maziko hayo ambayo nusura yatawaliwe na hisia za kisiasa kabla IPC kwa kushirikiana na waandishi wengine kuidhibiti hali hiyo.
Katibu Msaidizi wa IPC, Francis Godwin aliwatahadharisha wanasiasa wa vyama hivyo kwamba Mwangosi atazikwa kama mwandishi wa habari japokuwa aliuawa katika tukio lililohusisha shughuli za kisiasa.
Katika rambirambi zao, IPC walitoa kwa familia ya marehemu Sh 750,550 huku Klabu ya Waandishi mkoani Mbeya (MPC) ikitoa kiasi kama hicho ambacho sehemu yake kubwa ilitumika kufanikisha shughuli ya maziko hayo.
Dk Slaa alisema watabeba jukumu la kumsomesha mtoto wa kwanza wa Mwangosi. Mtoto huyo ambaye hata hivyo jina lake halikupatikana mara moja yupo kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Malangali, wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Naye Profesa Mwandosya alisema atabeba jukumu la kuwasomesha watoto wengine wa marehemu huku akiahidi kufuatilia ahadi za watu wengine katika kuisaidia familia ya Mwangosi kwa kuwa marehemu huyo ni ndugu yake wa jirani.
Wengine waliochangia familia ya Mwangosi ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa (Chadema), Chiku Abwao aliyetoa Sh 100,000.