Wednesday, September 26, 2012
CCM yajivua ‘gamba’
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, amesema katika kuhakikisha CCM inazidi kuwa na uhai na kupata ushindi katika uchaguzi mkuu mwaka 2015, Kamati Kuu ya Chama hicho imeamua kuwaengua wagombea wakongwe na kutoa nafasi kwa vijana.
Pamoja na hayo, habari za ndani za vikao vya chama hicho vinavyoendelea mjini hapa, zimebainisha kuwa Mwenyekiti huyo katika kuhakikisha mizizi ya ufisadi inakatwa ndani ya chama hicho, baadhi ya vigogo wakiwamo wabunge wagombea, majina yao yamekatwa huku wengine wenye majina makubwa wakipendekezwa kuendelea.
Akifungua kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho, mjini hapa jana jioni, Rais Kikwete alisema katika uchaguzi wa mwaka huu, chama hicho kimebahatika kupata wagombea wengi wasomi na wengi wao wakiwa vijana jambo ambalo linatia matumaini.
“Jana (juzi) CC tulimaliza saa 6.30 usiku, kazi tuliyofanya ni kubwa na tumefurahi kwamba safari hii pamoja na kupata wagombea wengi wakiwamo wasomi, wengi ni vijana, kwenye Kamati hii tumeamua kuwapa nafasi zaidi vijana na wenzetu wakongwe wakapumzike,” alisema Rais Kikwete.
Alisema kati ya vijana wasomi waliojitokeza kuwania nafasi ndani ya chama hicho, wamo walio vyuoni jambo linalotia moyo kuwa bado CCM iko hai ambapo alibainisha wazi kuwa chama chochote cha siasa kikikosa mwamko wa vijana lazima kitakuwa na matatizo.
“Napenda nieleweke kuwa hatuwezi kuwa na chama cha watu wazima pekee, chama chenye mfumo huo hakitakuwa na mfumo mzuri wa uongozi, tumefanya hivi ikiwa ni fursa ya kukipa chama chetu uhai na taswira mpya lakini kubwa zaidi ushindi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014 na Uchaguzi Mkuu 2015,” alisisitiza.
Alisema katika uchaguzi huo wa ndani wa chama, wanachokitarajia ni kupata timu ya viongozi wenye uadilifu, shupavu, hodari na wenye kukitetea chama, kwa maana nyingine alisisitiza kuwapo timu ya ushindi wa chama na si ushindi wa mtu.
“Na nasisitiza, hatutaki kiongozi mwenye ndimi mbili, maana nasikia kuna watu wanatishia eti wakikatwa huku kwenye ugombea wanakwenda vyama vingine, nasema hivi, wenye nia hiyo waende kwa sababu hadi kufikia kutishia hivyo ina maana tayari wana nafasi huko, tunawatakia kila la heri,” alisisitiza.
Aliwataka wagombea watakaoshindwa kwenye uchaguzi huo kutokata tamaa, kwa kuwa kushindwa kwao leo hakumaanishi hawawezi, bali ni kutokana na nafasi finyu lakini pia umuhimu wa mabadiliko na kutumia usemi kuwa kuvunjika kwa koleo si mwisho wa uhunzi. “Hata Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere (Julius) alisema chama kwanza utu baadaye.”
Aidha, Mwenyekiti huyo alizungumzia suala la baadhi ya wagombea wa chama hicho kudaiwa kutoa rushwa hali ambayo inageuza uchaguzi huo kama biashara na kuwa wagombea wa namna hiyo hawafai kwa kuwa hawajiamini, wala kuthamini chama, bali uongozi na kuwahakikishia kuwa safari hii Takukuru haitakuwa mbali nao na wakikamatwa wasimlaumu.
“Sheria ya rushwa inaanzia kwenye chama, najua wapo watu ambao wanakifanya chama chetu kisemwe sana, nawaomba sana tutumie fursa hii kubadilika na kukipa chama chetu heshima,” alisema.
Kikwete alionya wagombea ambao wamesababisha uchaguzi wa CCM kugeuka vurugu za silaha na kuwatanabaishia kuwa wamekifedhehesha chama hicho.
“Watu mnafikia hatua ya kutumia mishale, bastola na mikuki, kugombea NEC tu mnashikiana silaha kweli? Jamani uchaguzi si vita.” Wakati NEC ikianza, Katibu Mkuu wa chama hicho, Wilson Mukama alisema idadi halisi ya wajumbe wa NEC ni 216 na waliohudhuria ni 196.