• Sumaye, Lowassa, Chenge wakimbia kundi la kifo
WAKATI leo ndiyo siku ya mwisho kuchukua na kurejesha fomu za kuwania uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya wilaya, mkoa na taifa, mpambano wa kuwania nafasi hizo umekuwa ni vita kali iliyojikita katika kulipizana visasi, chuki na kuibua makundi ya urais mwaka 2015.
Mnyukano mkali upo katika kuwania uongozi wa jumuiya za chama hicho ambazo ni Umoja wa Vijana (UVCCM), Wanawake (UWT) na Wazazi.
Nafasi zingine za wajumbe wa NEC ambazo zimekuwa na ushindani mkubwa ni kupitia kapu maalumu, maarufu kwa jina la ‘Kundi la Kifo’ ambalo safari hii lina viti 10 Bara na 10 Visiwani.
Ushindani uliopo katika kundi hilo, umesababisha baadhi ya vigogo ambao wamekuwa na kawaida kuwania NEC kupitia kundi hilo, kukimbia na safari hii wanaomba nafasi hizo kupitia wilaya zao.
Baadhi ya vigogo waliokimbia kundi la kifo na wanaotajwa kutaka kuwania urais mwaka 2015 ni pamoja na mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye.
Sumaye ameachukua fomu ya NEC wiki iliyopita wilayani Hanang, akichuana vikali na Mbunge wa Hanang, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu.
Uamuzi wa Nagu ambaye amepata kuwa meneja kampeni wa Sumaye katika mbio za urais mwaka 2005, umewashangaza wengi kwani wadadisi wa masuala ya siasa nje na ndani ya CCM, wanaamini kuwa mafanikio yake kisiasa, yametokana na waziri mkuu huyo mstaafu.
Wakati Sumaye akikimbilia Hanang, Lowassa naye amekimbilia wilayani kwake Monduli ambako amechukua fomu ya NEC.
Mwingine aliyekimbilia wilayani, ni Mwanasheria Mkuu mstaafu na Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge.
Vigogo wengine waliokimbia kundi hilo ni Kapteni John Komba na Christopher Gachuma.
Duru za siasa ambazo gazeti hili imezipata, zinasema kuwa vigogo hao wameamua kukimbilia wilayani kukacha kundi la kifo baada ya CCM kufanya mabadiliko ya katiba ambapo kundi hilo litakuwa na viti kumi tu badala ya 20.
“Kundi la kifo safari hii lina viti kumi tu badala ya 20, na mara nyingi kumekuwa na kura za kiitifaki. Uwezekano wa kushindwa ni mkubwa mno, lakini pia ukipata kwa kura chache na kama una malengo ya kisiasa kwa 2015, haikupi nafasi nzuri. Ndiyo maana wazee wameona watokee kwenye wilaya zao,” alisema mmoja wa viongozi wa CCM.
Sababu nyingine inayotajwa vigogo hao kukimbia kundi la kifo, ni kutokana na ukweli kwamba endapo sekretarieti yote itaamua kugombea, nafasi sita kati ya kumi zinaweza kuchukuliwa nao, hivyo waombaji wengine wakalazimika kupigana vikumbo kuwania nafasi nne.
Mnyukano nafasi za mikoa
Mnyukano mkali upo katika nafasi za wenyeviti wa mikoa.
Mkoani Shinyanga, Mwenyekiti anayetetea kiti chake, Khamis Mgeja ameshikwa shati na hasimu wake kisiasa, Mbunge wa Kahama, James Lembeli.
Kabla hata ya zoezi la kuchukua fomu, mahasimu hawa walikuwa wakirushiana maneno, huku Mgeja akimfananisha Lembeli sawa na sisimizi ambaye hawezi kumyima usingizi.
Mkoani Dar es Salaam, Mwenyekiti wa sasa, John Guninita amekaliwa kooni na mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa, Ramadhani Madabida wakati Dodoma Adam Kimbisa anachuana na mkongwe William Kusila.
Aidha, kazi ipo mkoani Mwanza ambako Mbunge wa zamani wa Ilemela, Antony Diallo ameamua kuchukua fomu kumkabili mwenyekiti wa sasa, Clementi Mabina na mkoani Mara Makongoro Nyerere yuko jino kwa jino na Kisieri Chambili.
Wenyekiti Jumuiya ya Wazazi
Katika uchaguzi huo, unaotarajiwa kufanyika Novemba, Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono amerejea tena kuwania nafasi ya mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa.
Katika uchaguzi uliopita, Mkono aligombea kiti hicho, lakini jina lake lilienguliwa na NEC kwa sababu ambazo hadi sasa hazijajulikana.
Mkono anachuana na Mbunge wa Bukoba Vijijini, Joson Rweikiza, Matha Mlata na Salum Chicago.
Kwa upande wa UWT, Waziri Sofia Simba anaoneshana kazi na Mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango. Tayari wagombea hao wanaopewa nafasi kubwa, wameanza tambo za kisiasa.
Kazi ipo pia wilayani Nzega ambako Mbunge wa Nzega, Khamis Kingwangala na hasimu wake kisiasa, Hussein Bashe watachuana kuwania NEC kupitia wilaya hiyo.
source: Tanzania daima.