KWAMBA askari polisi mjini Morogoro juzi walimuua kwa risasi kijana mmoja na kujeruhi wengine wawili wakati walipokuwa wakidhibiti maandamano ya wafuasi wa Chadema, ni taarifa ambazo zimetusikitisha sana na kutoa picha kwamba nchi yetu hakika bado ina safari ndefu kuelekea kwenye demokrasia ya kweli na utawala bora.
Tunasema nchi yetu bado ina safari ndefu kufikia vigezo vya demokrasia na utawala bora kutokana na matukio mengi makubwa tunayoshuhudia mara kwa mara katika sehemu kadhaa nchini. Aghalabu yamekuwapo matukio ya vifo na uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu unaotokana na matumizi mabaya ya silaha na madaraka kwa upande wa Jeshi la Polisi. Mifano ya hali hiyo ya kusikitisha ni nyingi, lakini yatosha tu kusema hapa kwamba jeshi hilo kwa kiasi kikubwa limeshindwa kuelewa dhana ya ulinzi wa raia na haki ya mtu kuishi, ikiwa ndiyo dhima na dira kuu inayoliongoza jeshi hilo.
Yapo maeneo ambayo jeshi hilo limefanya vizuri na sisi tumekuwa msitari wa mbele kulimwagia sifa kila linapostahili kupongezwa. Lakini jeshi hilo limelaumiwa kwa mambo mengi ambayo hatuwezi kuyaorodhesha yote katika safu hii kutokana na ufinyu wa nafasi. Moja ya malalamiko makubwa ambayo yamekuwa yakielekezwa kwa jeshi hilo ni jinsi ambavyo limekuwa likivinyanyasa vyama vya upinzani na kuegemea kwa chama tawala. Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa siasa za vyama vingi nchini, Jeshi la Polisi limekuwa halionekani kuvitendea haki vyama vya upinzani na limekuwa linavunja sheria ya mwaka 1992 ambayo ilianzisha vyama hivyo.
Kwa mfano, jeshi hilo limekataa kuelewa au kutambua kwamba sheria hiyo ya vyama vya siasa haitoi mamlaka kwa jeshi hilo kutoa vibali kwa vyama hivyo kufanya shughuli za siasa, yakiwamo maandamano, mikutano ya ndani na ya hadhara na shughuli nyingine zozote za kisiasa. Sheria inasema kuwa, ili shughuli hizo zifanyike kwa amani na utulivu, lazima vyama hivyo vilitaarifu rasmi Jeshi la Polisi ndani ya saa 48 kabla ya kufanyika kwa shughuli hizo ili jeshi hilo litoe ulinzi. Lakini katika hali ya kushangaza, jeshi hilo limejipachika mamlaka ya kuratibu shughuli za vyama hivyo kwa kutoa au kukataa kutoa vibali vya kufanyika kwa shughuli hizo.
Swali ambalo limekuwa likiulizwa na wananchi wengi ni kuhusu sababu za jeshi hilo kutoa vibali pasipo pingamizi kwa vikundi vinavyoandamana au kufanya mikutano ya hadhara kuipongeza Serikali na viongozi wake? Kama kweli ajenda ya jeshi hilo siyo ya siri na inaendeshwa kwa dhamira safi, inakuwaje halifanyi hivyo kwa vyama vya upinzani ambavyo vimesajiliwa kisheria au vikundi vya wanaharakati vinavyotetea haki za kijamii? Inakuwaje basi vyama vya upinzani na vya kiharakati vikataliwe kuendesha shughuli zake kwa kisingizio cha kutokuwapo polisi wa kutosha kulinda shughuli hizo, lakini polisi wa kusha, tena wenye magari yaliyosheheni silaha za kivita wanapatikana kuzuia shughuli hizo zisifanyike?
Badala ya kulikemea jeshi hilo kwa kuvunja sheria na kukandamiza demokrasia, chama tawala na Serikali yake mara zote vimekuwa vikikaa kimya, huku vikichekelea pembeni na kuliacha jeshi hilo likitekeleza kile kinachodaiwa na vyama vya upinzani kwamba ni kutekeleza maagizo kutoka juu. Pengine ndiyo sababu kila mara jeshi hilo linaposababisha vifo vya raia kwa kisingizio cha kudhibiti maandamano ambayo hayana vibali vya polisi, Serikali hujitokeza na kulipongeza jeshi hilo kwa kusimamia sheria.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa jana. Akizungumzia tukio la Morogoro ambapo juzi mji huo na viunga vyake viligeuka uwanja wa mapambano, ambapo polisi waliua mtu mmoja kwa risasi wakati wakidhibiti maandamano ya wafuasi wa Chadema, Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi alisema polisi walikuwa wanatekeleza wajibu wao, huku akiwataka viongozi wa vyama vya siasa kufuata sheria.