Thursday, August 30, 2012
Mwisho wa kuhesabiwa sensa leo
OFISI ya Takwimu ya Taifa (NBS) imesema watu ambao watakuwa hawajahesabiwa hadi leo, wawasiliane na viongozi wao wa mitaa, vitongoji na vijiji.
Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Mawasiliano na Uhamasishaji wa NBS, Said Ameir alisema ofisi yake imetenga siku tano ili watu wote wawe wamehesabiwa.
Alifafanua, kama itatokea kuna watu hawajahesabiwa, watumie siku tatu zilizobaki kuanzia leo kuhakikisha wanafanya hivyo.
Alitaka waishio mijini wawasiliane na wenyekiti wa serikali za mitaa na wanaoishi vijijini wawasiliane na wenyeviti wa vitongoji na vijiji kwa msaada zaidi.
Ameir alifafanua kuwa pamoja na kuwa makarani wa sensa watapita, swali lao litabaki lile lile kuwa ni watu wangapi walilala ndani ya kaya hiyo usiku wa kuamkia Agosti 26.
Alikumbusha wananchi wahakikishe ambao hawakulala katika nyumba hizo usiku huo, hawahesabiwi kwani watakuwa wamehesabiwa walikotoka. Kuhusu matumizi ya dodoso fupi na dodoso refu, Ameir alisema katika kaya moja ni dodoso moja tu linatumika.
“Katika kaya ambako makarani wenye dodoso fupi wamepita, mwenye refu haruhusiwi kupita na pale alipopita mwenye refu mwenye fupi haruhusiwi kupita,” alifafanua. Alisema dodoso fupi linatumika kwa asilimia 70 ya kaya zinazohesabiwa wakati refu linatumika kwa asilimia 30 tu katika eneo moja.
Aliongeza kuwa fupi lina maswali 32 wakati refu lina maswali 62. Kuhusu taarifa za upungufu wa vifaa katika baadhi ya mikoa, Ameir alisema amesikia habari hizo lakini vifaa zaidi kwenye sensa ni madodoso ambayo alisema ofisi yake imehakikisha yapo mengi katika mikoa yote ili kusiwepo na tatizo hilo.
“Sisi unaposema vifaa ina maana ni madodoso, ukiacha sare za makarani, kwa hiyo tumejiimarisha kuhakikisha hakuna upungufu wowote,” alisema ofisa huyo. Ameir alitoa mwito kwa wananchi ambao hawajahesabiwa kuvuta subira kwani nia ya Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anahesabiwa. Upungufu Dodoma Hata hivyo, Dodoma, makarani wa sensa walilazimika kudurufu madodoso ili kuendelea na kazi baada ya kuishiwa. Hali hiyo ya upungufu wa vifaa ilijitokeza mapema katika maeneo ya Uwanja wa Ndege na Majengo, ambako makarani walilazimika kusitisha kazi kwa muda.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi alikiri upungufu huo na kusema tatizo hilo limetatuliwa kutokana na vifaa hivyo kuwasili kutoka Dar es Salaam na vilitarajiwa kusambazwa katika maeneo yenye upungufu. Alisema wilaya ya Kondoa ilikuwa na upungufu mkubwa.
Wakimbia nyumba Mkoani Dar es Salaam katika wilaya ya Kinondoni, licha ya kwamba kazi ya sensa ilifanyika vizuri kwa kiwango kikubwa, lakini zipo nyumba mbili ambazo hazijahesabiwa kutokana na wahusika kukimbia.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Jordan Rugimbana alisema hayo alipozungumza na gazeti hili kuhusu mwenendo wa sensa katika wilaya hiyo na kuzitaja nyumba hizo kuwa zipo maeneo ya Ununio na Mtambani.
Alisema katika nyumba hizo, makarani walipofika hawakukuta wahusika na kulazimika kushirikiana na wenyeviti wa mtaa, kujua ni nani waliokuwa wakiishi katika nyumba hizo.
Rugimbana alisema kwa ujumla kazi ya sensa katika wilaya hiyo ilikwenda vizuri ingawa mwanzoni kulikuwepo na upungufu wa vifaa ambapo NBS ilipoelezwa, ilishughulikia na sasa hakuna tena upungufu.
“Asilimia 80 ya makarani wamemaliza kushughulikia kaya kwa kaya sasa wanafanya majumuisho tu kujua ni wapi walikoacha kuhesabu,” alisema Rugimbana.
Aidha, alisema yapo matukio kadhaa yaliyowafikia, kwamba kuna baadhi ya watu wanakataa kuhesabiwa kwa kigezo cha dini, lakini alimshukuru Rais Jakaya Kikwete kwani hotuba yake ilileta mwelekeo mzuri wa kuelewa na kujiunga na sensa.
“Ipo baadhi ya misikiti ambayo waumini wao walikuwa wakiambiwa wasishiriki lakini wameshiriki,” alisema Rugimbana bila kuitaja.
Kadhalika, alisema zilikuwapo kaya 12 zilizoripotiwa katika maeneo ya Sinza, Mtambani na Mivumoni, ambazo hazikutaka kuhesabiwa, lakini polisi walipofika, kaya 10 walikubali kuhesabiwa huku mbili wakikosekana katika makazi yao. Imeandikwa na Shadrack Sagati na Lucy Lyatuu Dar na Sifa Lubasi, Dodoma.