Friday, August 31, 2012

Dk. Slaa amvutia pumzi Sitta


KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema anamvutia pumzi Spika mstaafu wa Bunge, Samuel Sitta, juu ya kauli yake kuwa chama hicho hakina viongozi wa kutosha kufanya kazi ya serikali.

Sitta ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, alitoa kauli hiyo juzi wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera, alipotembelea ofisi za chama chake, akisema CHADEMA haina kiongozi zaidi ya Dk. Slaa.

Sitta alikwenda mbali zaidi akisema kuwa CHADEMA ina viongozi wenye uzoefu wa kuongoza kumbi za muziki na kwamba Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, ni mjuzi wa disko za usiku.

Akizungumza na Tanzania Daima mjini Iringa jana, akiwa katika mwendelezo wa Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), Dk. Slaa, alisema tuhuma hizo ni nzito na lazima azipitie kwa umakini ili aweze kuzitolea maelezo.

“Nimesoma juu ya hizo taarifa na kama Sitta ninayemheshimu, amefikia kumuita mwenyekiti wetu mtaalamu wa kuongoza disko, si kauli nyepesi, hiyo ngoja tuichambue na leo au kesho tutatoa tamko zito juu ya hilo,” alisema Dk. Slaa.

Aliongeza kuwa Sitta ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki alitoa kauli hiyo akiwa katika jukwaa la siasa, hivyo naye anatafakari kama amjibu akiwa jukwaani au aitishe mkutano na waandishi wa habari.

Polisi waikaribisha M4C

Katika hatua nyingine, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (SACP), Michael Kamuhanda, amesema hawatakuwa na sababu ya kuzuia mikutano ya CHADEMA baada ya shughuli za sensa kumalizika.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamuhanda alisema tangu siku ya kwanza CHADEMA walipoingia mkoani humo hali ya utulivu ilikuwa ni nzuri na hakukuwa na matatizo yoyote mabaya waliyosababisha.

“Tunajua watafanya mkutano wao Septemba 2, mwaka huu, wilayani Mufindi, hatuna sababu ya kuzuia hilo labda ijitokeza sababu ya kiusalama, kwa kuwa hata Dk. Slaa nimezungumza naye na akaniambia wako salama na amefurahia walivyopokewa kifalme katika mkoa huu,” alisema Kamuhanda.

Akizungumzia sababu ya kuimarisha ulinzi, Kamanda Kamuhanda alisema hatua hiyo inatokana na hali halisi ya kisiasa kwa sasa na kwamba polisi wana wajibu wa kuchukua tahadhari kuhakikisha usalama unakuwepo.

Alipoulizwa kama jeshi hilo linatumiwa na viongozi wa CCM katika kuhakikisha mikutano ya CHADEMA haifanikiwi, Kamuhanda alisema si kweli kwani hata baadhi ya viongozi wa CCM wakiwamo wabunge wa mkoa huo hajawahi kukutana nao.

Tangu kuingia kwa viongozi kadhaa wa CHADEMA mkoani Iringa, jeshi hilo limekuwa katika tahadhari kubwa kwa hofu kuwa wanaweza kufanya mikutano kabla ya sensa ya watu na makazi kumalizika.