KIZA kimetanda juu ya siku rasmi ya kurejea kwa Dk Stephen Ulimboka nchini baada ya kuelezwa kuwa licha ya hali yake ya afya kuimarika matibabu yake yanatarajia kuwa ya muda mrefu.
Hivi karibuni ulitokea uvumi kuwa Dk Ulimboka ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari angerejea nchini siku yoyote ya mwezi ujao baada ya afya yake kuimarika.
Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin Chitage aliliambia gazeti hili jana kuwa habari za kuwa Dk Ulimboka angerejea nchini hivi karibuni hazina ukweli wowote kwakuwa matatizo yake yanahitaji matibabu ya muda mrefu.
“Dk Ulimboka anaendelea vizuri, lakini anahitaji kuendelea na matibabu zaidi nchini Afrika ya kusini, habari ya kuwa anaweza kurejea nchini kwa siku za hivi karibuni hazina ukweli wowote, kwani kwa sisi tunaoelewa taratibu za matibabu anayopatiwa hilo haliwezekani kwa sasa”, alisema Dk Chitage.
Alisema taarifa hizo hazina ukweli wowote na kwamba suala la matibabu yake si la muda mfupi,” alisema.
Dk Chitage alisisitiza kuwa DK Ulimboka ambaye alisafirishwa nje ya nchi kutokana na hali yake kubadilika ghafla baada ya figo kushindwa kufanya kazi anasitahili kuendelea na matibabu kwa muda zaidi ya hapo alipofikia.
Kabla ya kusafirishwa nje ya nchi, aliyekuwa kiongozi wa jopo la madaktari lililokuwa likimtibia Dar es Salaam, Profesa Joseph Kahamba alikaririwa na gazeti hili alisema mwenyekiti huyo alipata maumivu makali katika sehemu zote za mwili.
Katika hatua nyingine mmoja ya vyanzo vya habari vya kuaminika vilieleza kuwa afya ya Dk Ulimboka inaimarika, lakini kwa sasa suala la kurejea nchini bado kwa kuwa anaendelea na matibabu.
“Katika shambulio lile alipata matatizo makubwa katika sehemu za figo na macho, ingawa hali yake imezidi kuimarika bado matibabu yake hayawezi kuwa ya muda mfupi na yenye kumwezesha kuruhusiwa kurudi nyumbani kwa siku za hivi karibuni”kilisema chanzo hicho cha habari..
Dk Ulimboka alisafirishwa nje ya nchi baada ya Jopo la Madaktari Bingwa lililokuwa likimtibu likiongozwa na Profesa Joseph Kahamba kutoa ripoti kuwa hali yake imebadilika ghafla na kwamba angehitaji kusafirishwa nje kutokana na baadhi ya vipimo na matibabu kutokuwapo nchini.
Pia Profesa Kahamba aliwahi kukaririwa na gazeti hili akisema Dk Ulimboka katika shambulio lile alipata majeraha katika sehemu zote za mwili huku aking’olewa meno mawili na kucha za vidole vyake kunyofolewa.
Madaktari kushitaki serikali (MCT)
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Dk Ulimboka, viongoziwa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Jumuiya ya Madaktari na Madaktari waliofukuzwa kazi na wengine kusitishiwa usajili wa leseni zao za muda walikutana jijini Dar es Salaam jana na kupitisha azimio la kuishtaki Serikali na Baraza la Madaktari mahakamani.
Umuzi huo ni matokeo ya ushauri uliotolewa na wanasheria kwa madaktari hao waliopendekeza hatua mojawapo ya kuchukua kuwa ni kulifikisha suala hilo mahakamani.
Mwakilishi wa Madaktari hao, Dk Frank Kagoro, alilimbia gazeti hili kuwa wamefikia hatua ya kwenda mahakamani kudai haki baada ya kugundua kuwa hatua waliyochukuliwa haikuwatendea haki.
“Tumekubaliana kutekeleza usahuri wa wanasheria wetu, tunafikiria kufungua kesi mahakamani kupinga kitendo kilichofanywa na Serikali cha kufukuza baadhi ya madaktari kutokana na mgomo na (MCT) kusitisha leseni za muda kwa baadhi yetu”, alisema Dk Kagoro.