Monday, July 30, 2012
Rushwa Bungeni yatia doa taifa
KITENDO cha Bunge kukabiliwa na tuhuma za rushwa kutokana na baadhi ya wabunge kudaiwa kuhusika pamoja na kutetea ufisadi katika Shirika la Umeme (Tanesco), kimetajwa kuwa ni hatari kwa nchi na zinahitajika hatua za haraka kuwawajibisha wahusika.
Kutokana na tuhuma hizo za kuhongwa na kujiingiza katika vitendo vya rushwa kwa baadhi ya wabunge, watu wa kada tofauti wakiwemo wasomi waliozungumza na gazeti hili, baadhi yao wameshauri itungwe sheria ya kuwasimamisha ubunge watakaobainika kujihusisha na rushwa, kutetea uozo na mafisadi.
Aidha, viongozi wa chama wamesema hawatasita kuwachukulia hatua wanachama wao wabunge watakaobainika katika sakata hilo.
Hata hivyo, ipo Sheria ya Kinga na Madaraka ya Bunge ambapo wanaobainika kuhusika kupokea rushwa, wanaweza kuadhibiwa kwa kufukuzwa bungeni au kufungwa miaka mitatu jela.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Dk Benson Bana aliyesema yanayojitokeza bungeni kuhusu tuhuma za rushwa na kuhongwa, inadhihirisha wazi kuwa jamii ya watanzania ina mmomonyoko mkubwa wa maadili.
“Chombo kikubwa kama hiki kinatuhumiwa kuhusika na rushwa tena si mara moja, ni hatari kabisa kwa nchi yetu na si jambo zuri na inaonesha wazi kuwa baadhi ya wabunge hawana uadilifu,” alisema Dk Bana.
Alisema inafahamika wazi kuwa Bunge ni sehemu ya jamii hivyo kinachotendeka ndani ya chombo hicho kina akisi namna jamii ya kitanzania ilivyo, jambo ambalo linaibebesha sifa mbaya Tanzania.
Hata hivyo, alimpongeza Spika wa Bunge Anne Makinda kwa kuvunja Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini.
Alimpongeza pia Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) kwa kujitoa katika kamati yake ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa baada ya baadhi ya wajumbe wake kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.
“Ndio maana katika kulitafutia ufumbuzi jambo hili, nashauri iundwe Sheria itakayombana mbunge yeyote atakayethibitika kula rushwa au kutetea waziwazi uozo na kukumbatia ufisadi na ikiwezekana adhabu iwe kufukuzwa kabisa ubunge,” alisisitiza.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi ya CCM, Nape Nnauye, alisema chama hicho hakitosita kumchukulia hatua mbunge yeyote wa chama hicho atakayebainika kuhusika na rushwa au kuhongwa kutetea jambo lisilo na manufaa kwa Watanzania.
“Nimesikitika kuona tuhuma za baadhi ya wabunge wetu kuhongwa ili wafanye maamuzi ndivyo sivyo( bila kujali itikadi zao) zinaongezeka kila kukicha. Kama hawa wanaomudu kupata walau mahitaji muhimu ya binadamu kwa kipato chao halali wanahongwa, vipi watumishi ambao mshahara wao wa mwezi ni posho ya mbunge ya siku moja wafanyeje? Tunakwenda wapi?,” alihoji Nape.
Naye Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu, alitaka suala hilo la tuhuma za hongo na rushwa kwa wabunge lichukuliwe hatua zaidi kwa kuchunguzwa ili kubainika ukweli ulipo.
Akitoa maoni yake Waziri Kivuli wa Wizara ya Nishati na Madini, John Mnyika, alisema uamuzi wa Spika kuvunja kamati ya nishati ni sahihi lakini amechelewa.
Hata hivyo, Mnyika alisema uamuzi huo pekee hauwezi kurejesha heshima ya Bunge hilo wala kushughulikia uzembe na udhaifu ulioko ndani ya chombo hicho na kwenye serikali ikiwa hautaambatana na hatua nyingine za ziada na za haraka.
Aidha alitaka Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imalize kazi yake kwa dharura ili majina ya wahusika yatajwe ndani ya Bunge na Bunge lijadili kupitisha maazimio ya hatua za ziada za kuchukuliwa na vyombo huru vya kiuchunguzi na hatimaye watakaothibitika kuvunja sheria wafikishwe mahakamani.
“Pamoja na hatua hizo, Kamati za vyama nazo zichukue hatua kwa wabunge wake watakaotajwa ili kudumisha misingi ya uadilifu na uwajibikaji kwa maslahi ya umma,” alisema Mnyika.
Pia Mnyika alisema uzembe mwingine na kashfa za wabunge zisingeendelea kutokea iwapo Bunge hilo lingeyafanyia kazi mapendekezo yanayotolewa ndani ya Bunge hilo, akitolea mfano mapendekezo ya sakata la Richmond na sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Jairo.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah alipoulizwa kuhusu namna ambavyo taasisi yake inafanyia kazi tuhuma hizo zilizoibuliwa bungeni, alimtaka mwandishi wa habari hizi aandike anavyotaka.
“Nyie waandishi mna matatizo kila siku kwenye vipindi vyetu tunatangaza kuwa tunapata taarifa kupitia maeneo mbalimbali, na kuzifanyia kazi, sasa unanipigia simu na kuniuliza hili ili nisemeje, unataka nikujibu nini?” alihoji.
Juzi bungeni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alibainisha kuwa wapo baadhi ya wabunge wamehongwa ili kumwajibisha yeye na Katibu Mkuu wake Eliakim Maswi na kuwafananisha wabunge hao kama Mobutu.
Pamoja na hayo, Profesa Muhongo alianika bungeni humo kuwa yupo mmoja wa wabunge ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini amekuwa akifanya biashara na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kuliuzia matairi chini ya viwango.